Mkurugenzi Mtendaji na Rais wa Taasisi ya Mwalimu Julius Nyerere, Mzee Joseph Butiku, ametoa wito kwa Watanzania na vyama vya siasa nchini kudumisha utamaduni wa kuaminiana, kuheshimiana na kuweka mbele maslahi ya taifa kupitia mazungumzo badala ya upinzani usio na tija.
Mzee Butiku amebainisha kuwa mfumo wa utatuzi wa mambo kwa Waafrika siku zote unajikita katika msingi wa maridhiano (consensus) kupitia mazungumzo na kukubaliana, tofauti na utamaduni wa upinzani wa kisiasa uliorithiwa kutoka nje.
Mzee Butiku amesisitiza kuwa ni muhimu kwa jamii na makundi yote ya kisiasa kutambua na kuheshimu nafasi ya Urais, akiikumbusha jamii kuwa nchi inaweza kuwa na Kiongozi Mkuu mmoja pekee kwa wakati mmoja.
"Tuna Rais mmoja tu, na narudia tena, tuna Rais mmoja. Kila mtu hawezi kugeuka na kuwa Rais. Rais aliyechaguliwa ni mmoja na ni binadamu anayefanya kazi kubwa ya kuifanyia nchi hii maendeleo. Hata kama kuna kasoro zozote zinazojitokeza, hizo ni sehemu ya kazi tunayopaswa kushirikiana kuirekebisha ili kusogeza nchi mbele," -Amesema Mzee Butiku