SUMAYE TULIA USOME MCHEZO
CHADEMA ingeambia nini watu?
How come? Mtu atoke CCM na kujiunga Chadema mwaka 2015 halafu baada ya miaka minne tu atoshe kuwa Mwenyekiti wa Chadema iliyoanzishwa mwaka 1992?
Edward Lowasa alipotoka CCM alipewa nafasi ya ugombea Urais kimkakati, na kweli alipata kura nyingi kuliko wagombea wote wa Urais, dola ikamdhulumu. CHADEMA haikukosea kumpa Lowasa nafasi ya ugombea Urais lakini ingekosea sana kumpa nafasi ya uongozi mkubwa ndani ya Chama. Maana yake hata kama Lowasa angeingia ikulu bado chama kingekuwa mikononi mwa wanaChadema. Na huwezi kuwa Rais bila chama. Ni karata za siasa ambazo watoto wadogo hawawezi kuzicheza.
Hadi anaondoka Chadema, Lowasa alikuwa akitajwa kama mjumbe wa kamati kuu na mgombea Urais wa mwaka 2015, ndio maana kuondoka kwake hakujawa na madhara yoyote kwa Chadema.
Vipi kama Lowasa angesubiri kipindi cha uchaguzi agombee nafasi ya uongozi wa kitaifa wa Chama, angepata? Sidhani.
Itoshe kusema Mh. Sumaye aliaminiwa na wanachama kiasi cha kupewa nafasi ya uongozi wa kanda ya Pwani, lakini hakuaminiwa kiasi cha kupewa uwenyekiti wa Chama - Taifa. Na ndio maana wanachama wa Pwani wakaamua kumkataa mara tu alipotaka kujifanya anatosha zaidi ya uongozi wa kanda.
Demokrasia sio kuchaguliwa tu, ni pamoja na kukataliwa pia. Huwezi kusifu Demokrasia kwa sababu ya kuchaguliwa tu, isifu pia unapokataliwa.
CHADEMA ni chama kikubwa, chenye wanachama na wafuasi wengi, na pia maadui wengi wakiongozwa na CCM. Itakuwa kosa la kimkakati kwa Chadema yote kuwa chini ya mgeni kutoka CCM, hata dunia itashangaa sana.
Rai yangu kwa Mh. Sumaye, asifikiri amedhulumiwa wala asidhani Chadema hakuna Demokrasia. Demokrasia ipo ila imemkataa. Wanachadema wamejeruhiwa sana wakati huu na hawako tayari kuchezea nafasi ya uwenyekiti-Taifa, hiyo ndio nafasi pekee ambayo CCM wakiweza kuihujumu watavua nguo kwa shangwe. Inawezekana kabisa Sumaye akawa na nia njema, hilo anajua yeye, lakini kwa siasa za sasa Chadema haina nafasi ya kufanya majaribio kwenye uwenyekiti wa Taifa. Atulie, ausome mchezo.