Wakuu poleni kwa upambanaji.
Binafsi mimi kuna mda huwa nikitulizaga kichwa changu huwa naanza kujiuliza maswali mengi sana kuhusu mimi (binadamu) na ulimwengu kiujumla (Universe).
Maswali kama sisi (binadamu) ni kina nani,tumetoka wapi asili yetu, kwanini tupo (dhumuni la kuishi), mwisho wetu ama hatima yetu ni nini, Ulimwengu wa vitu je kama sayari, nyota, galaxies zimekuwepo vipi na nini hasa mwisho wake.
Hapo juu ni baadhi tu ya maswali ambayo huwa naiuliza sana akili yangu ikiwaga katika hali ya utulivu.
Lakini cha kusikitisha ni kwamba, katika maswali yote hayo ambayo huwa najiuliza, sijawahi kupata jibu la uhakika kuniridhisha kuhusu hayo maswali yangu.
Nimekuwa nikifanya bidii kubwa sana kupata majibu ya maswali yangu kupitia usomaji wa majarida au vitabu vihusuvyo historia,sayansi, dini na Falsafa lakini kote bado sijapata majibu ya kuniridhisha tofauti na kuambulia majibu ya kinadharia tu ambayo yana strength kiasi chake lakini pia yana weakness sehemu nyingi tu.
Na nikiri wazi tu kuwa katika usomaji wangu wa nadharia hizo zote (historia, sayansi, dini, falsafa) sehemu ambayo nimeanza kuiamini kunipa majibu ya maswali yangu ni kwenye DINI.
Nikiwa na maana nimeanza kuamini kwamba uwepo na sisi tuliohai na visivyo hai hapa ulimwenguni ni matokea ya Uumbaji ya nguvu kubwa sana inayoitwa MUNGU/ALLAH kama ambavyo dini nyingi zinaelezea nguvu hiyo.
Na leo maswali yangu yanajikita huko kwenye hiyo nguvu (Mungu) maana nimeanza kuiamini lakini pia kila nisomapo BIBLIA (mimi mkristo) inanipa maswali chungu nzima.
Sasa leo swali langu limejikita kwenye UKAMILIFU wa MUNGU.
Naombeni wasomaji mnielewe kuwa sina maana ya kukufuru (maana mara nyingi niulizapo maswali kuhusu MUNGU huwa naambiwa nakufuru) bali mimi nataka kujifunza zaidi kumuhusu huyu Mungu.
Dini nyingi (hasa Ukristo na uislamu) zimekuwa zikimwelezea Mungu kuwa ni Mkamilifu sana,mwenye nguvu nyingi sana, uwezo na akili zake hazichunguziki, hashindwi na chochote n.k.
Je hilo lina ukweli ? kupitia Biblia mimi nimeanza kudhani kwamba huenda kweli Mungu ana nguvu nyingi sana ila siyo zote, ana uwezo mkubwa sana ila siyo uwezo wote,ana maarifa mengi sana ila siyo maarifa yote, ana ukamilifu mwingi sana ila siyo ukamilifu wote n.k
Nasema haya ni kutokana na maswali yafuatayo :
1. Kama Mungu ana ukamilifu wote, kwanini sasa alimuumba malaika (Lucifer/shetani) alafu badae akaja kumuasi?
Kama Shetani/Lucifer aliasi maana yake ni kwamba Mungu alimuumba huyu kiumbe akiwa na madhaifu kadhaa na ndiyo maana alishindwa kuitii amri/mamlaka ya muumbaji wake.
Kama Mungu angelikuwa na ukamilifu wote, basi malaika wote wangelikuwa wameumbwa katika namna ya utii pekee, uasi usingetokea na huo uasi unadhihirisha kwamba Mungu aliwaumba hawa malaika wakiwa na udhaifu flani, hawakuwa na uimara wote.
2. Uumbaji wa Eva (Hawa) unaonesha kulikuwa na madhaifu pia.
Katika Biblia takatifu kwenye kitabu cha mwanzo, kuna mistari inaeleza kuwa "Mungu alimpa usingizi mzito Adam, alafu akabandua sehemu ya ubavu wake na kumfanya/kumuumba mwanamke (Hawa/Eva)".
Alafu Mungu akamwambia Adam kuwa huyu mwanamke atakuwa msaidizi wako
Lakini ni huyo huyo mwanamke ambae shetani (kwenye umbo la nyoka) alienda kumdanganya akachukua matunda ya mti walioambiwa asile yeye akala na akampelekea na mumewe (Adam) pia akala.
Lakini Mungu alivyomuuliza Adam kwanini umekula matunda ya mti ambao nilikwambia usile, Adam alijibu kuwa "Ni huyo mwanamke uliyenipa ndiye aliyeniletea nikala".
Tukio hili linadhihirisha kuwa Mungu alimpa Adam msaidizi (Hawa) ambae ni dhaifu sana na ndiyo maana alisababisha dhambi ikaenda hadi kwa Adam.
Na huenda kama Mungu angelikuwa amempa Adam msaidizi imara asiye na madhaifu basi ile dhambi ya kula tunda ingeepukika.
Uko wapi sasa ukamilifu wote wa Mungu ikiwa aliweza kuwaumba malaika dhaifu (ambao walikuja kumuasi) na pia bado akampa Adam msaidizi dhaifu kabisa ambaye alisababisha dhambi imwendee hadi Adam?
Kwa leo naombeni comment zenu zinifunze kuhusu hilo tu (La ukamilifu wa Mungu) alafu mengine nitauliza siku nyingine, na mengine nitakuwa nauliza humo humo kwenye comments zenu.
NB: Naamini Mungu yupo, kutokana na baadhi ya vitu ninavyoviona ulimwenguni (hasa uumbaji/creation) ambapo kuna baadhi ya vitu hasa sayansi inakosa majibu ya kuridhisha, ila shida yangu kubwa ni sifa za Mungu ambazo anapewa na wanadamu naona kama zinashindwa kujidhihirisha kwenye baadhi ya mambo.
Karibuni mnifunze.
Hongera! Kwa maswali nyeti, makini na yenye nguvu mno tena si maswali dhaifu bali maswali yenye mantiki
Vladmir Putini
Kwa kuanza kujibu hoja zako nianzie hapa, Ukamilifu wa Mungu, na ukamilifu wa kibinadamu ni vitu viwili tofauti kabisa , tuanzie hapa kwenye hoja ya uumbaji, Mungu alipowaumba malaika , ukweli wa mambo ni huu, alijua mwisho wa viumbe hao hadi mwanzo wao nikusema yeye huanza na mwisho kisha mwanzo.
Hivyo basi Mungu aliwaumba hao malaika kwa makusudi kabisa ,sio kwa bahati mbaya mfano huo wa jibu hilo hebu soma kisa cha farao uone vile Mungu anavyotenda kazi ,, anasema Swahili Union Version KUT. 4:21 BWANA akamwambia Musa, Hapo utakaporudi Misri, angalia ukazifanye mbele ya farao zile ajabu zote nilizozitia mkononi mwako; lakini nitaufanya mgumu moyo wake, naye hatawapa ruhusa hao watu waende zao. Zingatia sana maneno ya Mungu kumbe ugumu wa Moyo wa farao aliufanya Bwana mwenyewe nikusema Utendaji kazi wake unashangaza sana.
Pia ukiendelea kusoma vema utangundua wazi hata ADAMU NA MKEWE HAWA. MUNGU anasema mwenyewe kwamba aliwaumba wakiwa wakamilifu kabisa Mungu hakuumba kinyonge wa dosari , hivyo basi , kuna Jambo la msingi uliweke moyoni hapa , uasi wa Adamu na Hawa ni Ni shirikisho lisilo la kawaida, waliloshirikishwa bila wao kujua hasa kwa kina , maana yake ni nini? Ni hii,, Lucifer aliyekuwa wa pili kwa cheo mbinguni alipoasi alihakikisha anapata wafuasi, na hii sio tu ka jamii ya kibinadamu No hata jamii ya malaika, sasa kwa malaika kuasi Ukamilifu wa MUNGU , unakoma?
Hasha haukomi, ikumbukwe kuwa Mungu aliwaumba malaika na wanadamu akawapa uhuru wa kuchagua , kuamua na kutenda watakavyo hiyo sifa ni yake mwenyewe , ndio maana mwanadamu au malaika alipoamua kuchagua kile alichokiona bora Mungu hakuingilia badala yake aliacha ili kutimiza haki yote , Malaika sio roboti wala mwanadamu sio roboti hasha , hatuko understand control. Kila unachokifanya umeamua mwenyewe na ndio maana umepata muda wa kuuliza na kutafakari ,na huo ndio ukamilifu wa Mungu.
Na ikumbukwe pia ukisema ukamilifu ni lazima urejee lugha ya kiswahili kwa umakini mfano ukamilifu ni kinyume cha kisicho kikamilifu, mwanadamu sio mkamilifu ila Mungu tu ,, mfano wake ili ikaebsawa . Mwanadamu asipovaa viatu na akatembe juu ya makaa ya moto au miiba hawezi kuwa salama ila Mungu ni yule anafanya kinyume cha hapo. Mwanadamu akifa, hawezi lolote, Mungu akifa katika kifo bado ana mamlaka juu ya kifo,, soma hii itakusaidia rafiki...Swahili Union Version YN. 10:17 Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena.
Zingatia sana maneno ya Yesu, uhai wake ni yeye mwenyewe ndiye anayeutoa na kuutwaa tena, jambo hilo mwanadamu wala kiumbe hakiwezi na huu ndio ukamilifu hasa. Kwa sasa nikomee hapa asante.