Hivi kwanini kila mradi, shirika au kampuni zinazoyumba katika awamu hii mnasema sababu ya kuyumba huko ni upigaji? Yaani mnataka kutuaminisha kwamba kila kitu katika nchi hii kilichokuwa kinastawi kabla ya awamu hii ni matokeo ya dili za ujanja ujanja na kwamba kwavile katika awamu hii dili hizo hazipo tena basi ndo sababu ya kuyumba.
Kwa maoni yangu huku ni kupotosha ukweli. Mathalani inawezekanaje kutuaminisha kuwa kulikuwa na dili za upigaji katika "kulistawisha" shirika la NHC wakati hakuna ripoti zinazoonesha upigaji huo iwe ya CAG, TAKUKURU au kamati yoyote ya Bunge? Mkurugenzi wa shirika hili Ndg Mchechu aliondolewa na Rais. Hata hivyo "mtumbuaji" hakueleza sababu ya kumuondoa mkurugenzi huyo kuwa ni ubadhirifu au utendaji usioridhisha kama afanyavyo kwa watumbuliwa wengine.
Lakini suala la msingi hapa siyo kujadili dili za upigaji za "watu wachache", bali ni ustawi wa shirika katika utawala huu. Hili ni shirika la umma, kwahiyo mwenye mamlaka na uwezo wa kuliendeleza au kiliua ni serikali. Itakuwa ni jambo la kushangaza sana kuona kwamba dili za upigaji za watu wacheche katika awamu zilizopita ziliweza kuliendeleza na kustawisha biashara za NHC, lakini mipango na mikakati halali ya serikali ya awamu ya tano inashindwa. Je, tulaumu dili za upigaji za watu wachache zilizostawisha shirika huko nyuma au tulaumu mipango na mikakati halali ya serikali ya awamu hii iliyoshindwa kustawisha shirika? Au tuseme shirika limetelekezwa na serikali ya awamu hii kwavile liliendelezwa kifisadi huko nyuma? Kama ni hivyo, je hatua hiyo ya kulitelekeza shirika ina tija gani kwa taifa?