Kwa kawaida inafahamika kwamba ikitokea Waziri Mkuu amejiuzulu, na Baraza zima la Mawaziri linavunjwa.
Swali langu ni kwamba, Ikiwa Waziri Mkuu atajiuzulu na wakati huo pakiwa na Naibu Waziri Mkuu, Je Baraza la Mawaziri litavunjwa ama halitovunjwa kwasababu tayari patakuwa na Naibu Waziri Mkuu?
- Tunachokijua
- Agosti 30, 2023, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alifanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri na Makatibu Wakuu.
Mabadiliko hayo yalihusisha uteuzi wa Naibu Waziri Mkuu, Mawaziri wanne, Naibu Mawaziri watano, Makatibu Wakuu watatu na Naibu Makatibu Wakuu watatu pamoja na kuwabadilisha Wizara baadhi ya Mawaziri na Makatibu Wakuu.
Kupitia taarifa Rasmi ya Ikulu iliyotolewa kwa umma, Rais Samia alimteua Dkt. Doto Mashaka Biteko kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, na kwamba katika nafasi yake ya Naibu Waziri Mkuu, Biteko atashughulikia uratibu wa shughuli za Serikali.
Uwepo wa cheo cha Naibu Waziri Mkuu kikatiba
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 haifafanui uwepo wa cheo hiki, pia hakuna kifungu kinachozungumzia moja kwa moja kuhusu cheo cha Naibu Waziri Mkuu.
Hata hivyo, Ibara ya 36 ya Katiba hiyo inampa Rais Mamlaka ya kuanzisha na kuwateua watu wa kushika nafasi za madaraka (Sheria ya 1984, Na.15 ib.9, Sheria ya 2000 Na.3 ib.6). Rejea:
"Ibara ya 36.
(1) Bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii na ya sheria nyingine yoyote, Rais atakuwa na mamlaka ya kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya namna mbalimbali katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano."
Aidha, kifungu cha 2 cha Ibara hii kinampa Rais madaraka ya kuteua watu wa kushika nafasi za madaraka ya viongozi wanaowajibika kuweka sera za idara na taasisi za Serikali, na watendaji wakuu wanao wajibika kusimamia utekelezaji wa sera za idara na taasisi hizo katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, nafasi ambazo zimetajwa katika Katiba hii au katika sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge kwamba zitajazwa kwa uteuzi unaofanywa na Rais.
Hivyo, kwa kurejea vifungu hivi vya Katiba, Rais anayo mamlaka ya kufanya uteuzi wa Nafasi ya Naibu Waziri Mkuu, japokuwa nafasi husika haijatajwa moja kwa moja kwenye katiba.
Historia ya Nafasi hii nchini
Dkt. Doto Mashaka Biteko anashika nafasi ya Uongozi ambayo mara ya mwisho ilitumikiwa mwaka 1994 na Hayati Augustino Mrema.
Pia, Balozi Dkt. Salim Ahmed Salim ambaye amewahi kuwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, alihudumu katika nafasi hiyo mwaka 1986 hadi 1989 chini ya Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi.
Katika historia ya Tanzania, nafasi hii imewahi kukaliwa na watu watatu pekee hadi sasa.
Kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri baada ya kujiuzulu kwa Waziri Mkuu
Nafasi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetajwa Kikatiba kwenye Ibara ya 51 (Sheria ya 1992 Na. 20, ibara 9) na kwamba atakuwa na madaraka juu ya udhibiti,usimamiaji, utekelezaji wa siku hata siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Pia, Waziri Mkuu atakuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni.
Aidha, Ibara ya 54 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inataja uwepo wa Baraza la Mawaziri ambapo Waziri Mkuu ni sehemu ya Baraza hili pamoja na wajumbe wengine ambao ni Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Rais wa Zanzibar na Mawaziri wote.
Pamoja na Mambo mengine, Ibara ya 57 (2) ya Katiba hii inataja mazingira yanayoweza kusababisha kukoma kwa Baraza la Mawaziri ikiwemo nafasi ya Waziri Mkuu kuwa wazi kwa kujiuzulu au sababu nyingine yoyote.
Baada ya Rais Samia kumteua Biteko, mijadala mingi imeibuka ikijadili nini kitatokea kwa baraza la Mawaziri iwapo Waziri Mkuu anajiuzulu, Rais atavunja Baraza hilo?
JamiiForums imezungumza na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa aliyefafanua kuwa Waziri Mkuu ndie Kikatiba anafungamanishwa na sharti la kuvunjwa kwa Bunge na Naibu Waziri Mkuu hawezi kuzuia na likivunjwa likiundwa upya Naibu Waziri Mkuu kama bado ana sifa za uteuzi naye atateuliwa tena.
Dkt. Doto Mashaka Biteko, Naibu Waziri Mkuu
Aidha, Msigwa amebainisha kuwa tofauti na Waziri Mkuu, Naibu wake hahitaji kuidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya uteuzi wake na kwamba kwa kuwa Waziri Mkuu ni Mbunge na Msimamizi Mkuu wa shughuli za siku kwa siku za serikali, Naibu Waziri Mkuu ni lazima atokane na kundi mojawapo la wabunge waliopo Kikatiba na anapaswa kufanya majukumu kama yatakavyosomeka kwenye Hati/Instrument inayoanzisha ofisi yake.
Dkt. Doto Mashaka Biteko alizaliwa Desemba 30, 1978, ni mwanasiasa na mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alichaguliwa kuwa mbunge wa Bukombe kuanzia mwaka 2015 na kabla ya Kuteuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu alikuwa anahudumu kama Waziri wa Madini.