SEHEMU YA 2:
Inaendelea.....
...Mwenyeji wangu hakupatikana hadi kunakucha. Usiku huo ilibidi nijilaze mle mle stand ya mkoa. Na hata asubuhi nilipomtafuta, alipongundua ni mimi, mtandao ukaanza kuzingua. Mara hanisikii vizuri. Simu hakupokea tena, na mimi nikaamua kuachana nae.
Nilitoka nje ya stand,nikawa natembea tembea tu bila kujua naenda wapi. Mida ya mchana nikajakustukia nipo eneo linaitwa Tabata. Njaa kali, sina hela. Kiufupi sina kitu chochote cha thamani. Nikaingia kwa mama ntilie, nikamlilia shida nione kama atanisaidia, akagoma. Nikamwambia hata nifanye kazi yoyote nipate hata ukoko. Akanijibu, kazi zipo, ila msosi wote una order yani hadi huo ukoko. Nikaishia kunywa maji kisha nikaondoka.
Usiku ukapita bila kula chochote zaidi ya maji. Kesho yake ikakata tena bila chochote. Kwanza sina sehemu maalumu, natembea tu bila kujua naenda wapi, cha msingi naenda mbele. Ilipofika siku ya pili usiku, nikaona kabisa hapa nakufa. Maana mwili haukuwa na nguvu hata kidogo, ukiomba msaada unaishia kupewa maji, tena na yenyewe ni baada ya kuulizwa maswali kibao.
Sijui akili au ujasiri ulitoka wapi, ila nakumbuka kuna sehem inaitwa Vingunguti, njiani niliokota kava la simu jeusi. Baada ya kuwa na lile kava, nikatafuta kiroba cha unga kilocho tupu, ndani nikakiweka mawe kadhaa na mabox, alaf nikaingia kwa mama ntilie. Nikauliza chai ipo? Akasema ipo, chapati nazo zipo? Akajibu zipo. Huku natetemeka na moyo unadunda kuliko maelezo, nikamwambia " Naomba chai ya maziwa na chapati 5"
Zikaletwa, nikazipiga, nikaongeza na chai. Chapati zilipoisha na chai ipo nusu. Nikatoa kava la simu na kujifanya naongea na simu huku nasogea nje ya kibanda, hapo ule mzigo wangu nimeuacha pale ndani. Nikasimama mlangoni huku naongea "Me nishafika, na mzigo ninao hapa, njoo na usafiri unichukue maana nataka kuondoka"... Nilipoona yule mama ntilie hanifatilii, nikazidi kusogea mbele, nilivyokata kona tu, nilitoka mbio sio za nchi hii. Sijui kule ilikuwaje,na sikuwahi kurudi tena.
Kulipokucha nikaendelea kutafuta kibarua. Nikafanikiwa kupata kwa wale wafyatua tofali kwa mashine. Zikifyatuliwa tu,unabeba fasta na kwenda kupanga sehemu. Speed,uzito wa tofali,inama inuka jumlisha kuwa sijapata msosi wa uhakika kwa siku kadhaa...nilipatwa na kizunguzungu nikaanguka na tofali la watu. Bosi aliwaka kichizi. Akasema nimlipe. Sina hela,ikabidi nimwambie kwa uungwana akate hela yake ktk posho yangu alaf anipe iliyobaki ambayo nastahili kupata kwa kazi ambayo nishafanya. Boss akasema makubaliano ni ufanye kazi siku nzima,kwa muda huu mchache uliofanya sina cha kukulipa,kwanza ushanitia hasara,SEPA.
Ikabidi niondoke.
•••••••••• ••••••••••••• •••••••••••••• •••••••••••••••••
Mungu si Athumani, katika kuendelea kujielezea kwa watu niliokuwa nakutana nao nilibahatika kupata kazi ya kusimamia ng'ombe wa mzee mmoja maeneo ya tabata. Dar majani hakuna, unayatafuta kwa tabu sana, alafu mzee akawa anasumbua malipo. Sema hakuna jinsi, si nilikimbia kusoma Vishazi?.
Nakumbuka siku moja katika pita pita natafuta sehemu ya kukata nyasi, nikakuta Don mmoja bomba la maji limepasuka nje ya fensi yake, na maji yanavuja sana. Akaniita na kuniuliza kama namfahamu fundi bomba yoyote maeneo yale.. Bila kuvunga ikabidi nijifanye fundi bomba. Yule Don akaniambia sasa hapa inabidi uwe na konekta , tunazipataje? Nikaropoka "itabidi tununue, moja inauzwa 7000" ila kiukweli hata sikuelewa hizo konekta ndio nini na bei sijui. Jamaa akasema mbona unataja bei kubwa hivyo? Ngoja nikuelekeze sehemu wanapouza kwa 6000. Akanielekeza kisha akanipatia hela. Ila kabla sijaondoka akaniuliza ninapokaa. Nikamuelekeza akapajua.
Baada ya kununua zile konekta, nikarudi, nikachimba sehemu iliyopasuka. Ili niweze kupaunga, ikabidi nikate bomba. Presha na wingi wa maji vikanizidia, nikaanza kutetemeka pale. Kila nikitaka kuziba, maji hayo. Yule Don ikabidi aniulize "Hivi ww ni fundi kweli?.. Na jibu nini kwa mfano? Bahati nzuri simu yake ikaita, aliongea kidogo alaf akaondoka eneo lile. Hapo na mm akili ikarudi, maana kusimamiwa kulinitoa mchezoni. Nikapata wazo la kutumia moto kutanua bomba, alaf nikayazungushia na mifuko ya nailoni, mwisho nikabana na mpira . Maji yakaacha kutoka,zile konekta nikaweka mfukoni maana sikuzitumia. Nikafukia, nikamuita yule Don, akapaangalia na kuridhishwa ila akasema hela nifate kesho ili aangalie kama kweli zoezi limefanikiwa kwa 100%.
Kesho yake mapema sana, yule Don akaja home pale kumuulizia fundi bomba (mimi). Inaonekana usiku presha ya maji ilizidi pakafumuka. Sasa yule mzee ninayekaa nae anashangaa mimi kuitwa fundi bomba. Ikabidi amwambie ukweli yule Don kuwa mimi sio fundi. Hapo nishasemwa sana. Ikabidi aitwr fundi kweli, nikawarudishia konekta zao. Sema yule Don akaniambia ukiwa na shida unasema, sio unajitwika majukumu sio yako utakuja kupata matatizo mjini hapa, akanipa elfu 5 nikasepa..
Nikaendelea na kazi ya kulisha mifugo kwa yule mzee. Ila mkewe alikuwa na nongwa sana. Ukiacha kazi za mifugo,alikuwa ananipa kazi ya kufulia nguo wanae, kudeki, kumwagilia bustani, kusafisha mtaro uliokuwa nje ya nyumba. Pia kuna siku akataka nimfulie nguo zake yeye sidiria, nguo za kulalia na tight. Niligoma kufua, akaongea sana. Na kumbuka akatoka kwa hasira. Sijui alisahau nini ndani , akarudi na kunikuta napiga deki, nilipomuona na mm ndio nikamwaga sabuni ya unga na maji kwenye zile malumalu. Kaja na hasira, alipiga mwereka sio wa nchi hii,alijibamiza chini hadi nikamuonea huruma. Usiku wa siku hiyo ndio ilikuwa siku ya mwisho mimi kufanya kazi na kulala kwenye nyumba hiyo...