Tuendelee sasa..
.....Maana yule Mzee aliporudi, kabla hata sijamsalimia aliniuliza namdai kiasi gani? Tukapigiana hesabu akanipa changu alaf akaniambia "Fanya haraka utoke nataka kufunga geti tulale"
Sikujifikiria sana, kama niliweza kuondoka kwetu sembuse hapa? Nikabeba vyangu nikatoka. Hapo ilikuwa majira kama ya saa tatu usiku. Nikajichanganya mtaani. Niwe muwazi, pamoja na kukaa sana Dar ila watu wake sijawahi kuwaelewa. Kila mtu ni mjanja mjanja na anajua kila kitu,hakuna siku niliyotoka nje usiku nikakuta watu wamelala,mda wote wanapirika pirika tu. Pia hata mtu usiyemdhania anaweza akakuibia au kukudhurumu. Nasema hivi kwasababu ya kilichonikuta nilivyorudi mtaani. Nilikuwa natembea mdogo mdogo lengo ikiwa nielekee sehemu inaitwa Kariakoo maana niliambiwa huko kuna kila kitu japo sikuwahi fika. Kutokana na kubana bajeti sikutaka kupanda gari maana hela yenyewe ya ngama.
Kuna sehemu kule Dar panaitwa kwa Mnyamani. Maeneo yale nilikutana na watu kama wa 5 wakiwa wameshika fimbo, wanajiita sungusungu. Walinisimamisha na kuanza kunihoji, muda ule. Nikajaribu kutoa maelezo yangu, ila hawakutaka kunielewa. Watu wa Dar wanaongea haraka haraka sana hadi wakaanza kunichanganya. Naongea neno moja, wao washao gea 10.
Sijawahi kuona sungusungu anamsachi mtu, wala kumpiga mtu. Wakachukua hela zangu, bahati nzuri sikuziweka zote pamoja, nikabaki na kiasi kidogo. Waliponiacha, nikatembea hadi sokoni buguruni, nilipoona watu wengi wengi, nikaweka kambi pale kwa mzee aliyekuwa anauza kahawa. Kulipokucha nikapata kibarua cha kushusha matikiti. Hapo kidogo nikapata vijihela. Sikwenda tena kariakoo, nikaweka kambi hapo. Mida ya mchana, kazi hakuna ikabidi nitulie kwenye kijimgahawa cha mama mmoja hivi huku nakunywa soda maana hawaruhusu kukaa bure. Wakati nainywa soda yangu taratibu ili isiishe, kwenye tv kulikuwa na kipindi cha maswala ya shule (nishakisahau jina) ila channel ni Star Tv. Yani kile kipindi cha siku hiyo kama kilinilenga mimi, maana somo lilikuwa Kiswahili, maswala ya sentensi sentensi. Yule ticha alikuwa anafundisha maswala ya kutunga sentensi za "...nge..." Mara nikamsikia ametoa mfano "Ningejua, nisingeondoka" . Ile sentensi ikanishtua sana. Nikamwambia yule mama mwenye mgahawa abadili channel "Maliza soda uende" ilo ndio jibu alilonipa
Kimoyo moyo nikafikiria " Ningeenda kidato cha tano, nisingekuwa hapa" Nikajikuta napakumbuka nyumbani kwa wazee. Ikanipelekea kulikumbuka tukio moja ambalo lilitaka kuwagombanisha mama na baba. Ilikuwa ni kama wiki mmoja baada ya kudondosha kibox cha kondom darasani, kwavile nilipewa suspension ya wiki 3. Nilivyorudi nyumbani mzee alisema kwa wiki 3 zote itakuwa zamu yako kuchunga mbuzi.
Sasa siku hiyo tuko machungoni na na watoto wengine, tukaokota kiberiti cha gesi. Kule machungoni tukawa tunawasha majani alafu tunazima kwa kukanyaga. Sasa kuna muda tukawasha, ile tunazima, kukanyaga jani likapeperushwa na upepo, moto ukawaka na kwingine. Kila tukijitahidi kuzima, moto unapepea. Moto ukatanda kote, mbuzi zikaanza kukimbia ovyo. Kuona vile na sisi tukakimbia kuzifata mbuzi huku tunarudi nyumbani. Wanakijiji wakaitana, wakaushambulia moto na kufanikiwa kuuzima japo ulishaunguza eneo kubwa kiasi. Mzee mzima nikarudi nyumbani, moja kwa moja chumbani nikazuga kulala. Kumbe wakati tunakimbia na mbuzi kuna bibi mmoja alikuwa anaokota kuni alituona. Kwenye mkutano wa kijiji akatutaja tuliosababisha moto. Siku hiyo mzee alinipiga fimbo sio za nchi hii. Baadae namsikia anamuuliza mama " Hivi mama nanii, huyu ni mwanangu kweli??" Bi mkubwa nae akawaka "Nitolee wehu wako hapa, angalia lipua la mwanao alaf nenda kajiangalie kwenye kioo kama hujawahi kujiangalia" faza akawa mpole, maana kama ni pua tu, kweli tunazo.
Pia wakati nasubiria majibu ya kidato cha nne, kuna demu nilikuwaga nae ila akaja kunipiga chini baada ya kumpata mwenye hela. Miezi kadhaa akadaka mimba, ila yule jamaa akaikana. Kijiji chote kilikuwa kinanionaga na yule dem, habari zikasambaa mimba yangu. Demu nae akashikiria pale pale kuwa mimba yangu. Nilijitahidi sana kukataa , ila watu akiwemo faza hawakunielewa. Japo baadae sana ilikuja kugundulika kuwa mimba haikuwa yangu.
Hayo matukio yote nilikuwa nayakumbuka wakati nipo kwenye ule mgahawa pale buguruni. Nikamalizia soda nikatoka.
**** **** ***** ***** *****
Nilikomaa sana pale buguruni kwa muda mrefu, nafanya kazi pale na kujiegesha mule mule. Nakumbuka siku moja nilikuwa nimekaa na wabeba mizigo wenzangu tunapiga story. Akatokea jamaa akawa anatupa story za migodini, kuwa unafanya kazi kwa tabu ila ukitusua unasahau msoto. Jamaa alikuwa anafanyia kwenye migodi za Msumbiji, kuna eneo linaitwa Mtipweshi (kama sijakosea kulitamka). Story yake ilinivutia, nikajisemea, sibebi mizigo tena hapa, naenda Msumbiji
...............