CHOKOCHOKO ZA MWENYEKITI WA CCM MKOA WA MWANZA NA CHOKOCHOKO ZA MWENYEKITI WA CHADEMA MKOA WA NJOMBE KUHUSU KATIBA MPYA!
Mheshimiwa Anthony Diallo ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza. Alikuwa Mbunge wa Ilemela kupitia CCM na aliwahi pia kuwa Waziri katika Wizara kadhaa! Lakini sasa amekataa 'kunyamala'. Ameamua kuiasi kauli ya Mkuu mmoja wa Mkoa aliyesema kuwa wastaafu wakae kimya kwa kuwa muda wao ulikuwa umekwisha, la sivyo wakisema, watatwangwa! Tarehe 9 Julai 2021, Diallo amenukuliwa na vyombo vya habari akilonga maneno mazito! Anasema kuwa huko nyuma waliwahi kumpa nafasi ya kuongoza nchi mtu aliyewahi kuwa na historia ya kutibiwa Milembe.
Kwa nafasi alizowahi kushika, Diallo alishiriki maamuzi makubwa katika nchi kupitia Ubunge, Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Ujumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM na Ujumbe wa Baraza la Mawaziri. Kwa sababu hiyo kauli zake sio za kupuuzia hata kidogo! Hata hivyo, Diallo hajatuambia ni lini walipitisha uamuzi huo wa kumpa mtu nchi aliyewahi kutibiwa Milembe na wala hajatuambia ni nani mtu huyo aliyepitishwa! Hizi ndizo 'chokochoko' zenye tija kwa Taifa. Lakini inaonekana wakubwa hawapendi kusikia 'maneno yenye kuleta chokochoko'. Je, Diallo atahojiwa kwa kuleta 'chokochoko' hizi kama alivyohojiwa Rose Mayemba yule Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Njombe? Je, Askofu Mwamakula atalazimika kumpazia sauti Diallo kama alivyompazia Mayemba?
Diallo ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza na Mayemba ni Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Njombe. Mmoja anaongoza Chama Tawala ngazi ya Mkoa na mwingine anaongoza Chama cha Upinzani ngazi ya Mkoa. Wote wanafanana kwa kuwa wote wametoa 'kauli zenye kulileta chokochoko' katika Taifa. Tofauti ni kuwa mmoja katumia mitandao ya kijamii na mwingine katumia televisheni. Mmoja aliwekwa chini ya ulinzi na kuhojiwa na Jeshi la Polisi na mwingine ndio kwanza Taifa linatafakari na kuchakata 'chokochoko' zake. Wote wawili wametoa 'chokochoko' zao katika muktadha wa mjadala kuhusu Katiba Mpya.
Pamoja na 'chokochoko' zake, Diallo anakoleza mjadala wa Katiba Mpya! Mjadala huo ndio 'chokochoko' kubwa zaidi. 'Chokochoko' hujadiliwa na hazikimbiwi. Kwa sababu hiyo, sisi Askofu Mwamakula hatutarajii kusikia Diallo anaitwa kuhojiwa kwa sababu ya 'chokochoko' hizo. Kama Chama cha Siasa kinaweza kupitisha jina la mtu mwenye 'rekodi ya kutibiwa Milembe' ili aongoze nchi na vyombo vya usalama vikaridhia au vikashindwa kubaini hilo, basi hiyo ndiyo 'chokochoko' kubwa zaidi inayofaa kujadiliwa sambamba na 'chokochoko' inayohusu Katiba Mpya!
Mwanakondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula