Ujasusi ni kitendo cha kitengo cha serikali au taifa kufanya upelelezi, utafiti, uchunguzi wa jambo fulani la kisiasa, kiuchumi, kiteknolojia au kijamii nje au ndani ya mipaka ya nchi husika kwa manufaa au matumizi ya nchi hiyo. Ujasusi unahusisha opereseheni mbalimbali za kuangamiza mfumo, mtu, miundombinu au kikundi hatarishi kwa maslahi ya nchi mmiliki wa kikundi cha ujasusi. Mataifa mengi yanamiliki na kugharimia vitengo vya kijasusi na vinatambulika kimataifa.
Ugaidi ni uwanaharakati wa kikundi cha watu wenye itikadi za kidini au kisiasa uliopitiliza, uliovuka mipaka ya matumizi ya nguvu ya hoja kufanya madai yao na kuamua kutumia nguvu ya silaha, vitisho, kuteka, kushambulia, kuua na hata kumiliki sehemu ya ardhi au nchi kwa lengo la kujitanua na kusambaza hoja na matakwa yao ndani na nje ya mipaka ya mataifa Ugaidi unapoanzia. Ugaidi ni uhalifu kimataifa ingawa baadhi ya nchi hufadhili ugaidi kwa kificho. Ugaidi huendeshwa kwa fedha haramu, za wizi au biashara haramu au za kificho na hata michango isiyo rasmi.