Kitendo cha kutishia kuua kwa bastola kilichotaka kufanywa na kijana mmoja ambaye mimi siamini kama ni sehemu ya usalana wa Taifa ni muendelezo wa matumizi ya nguvu bila kutumia sheria ulioasisiwa na Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam Paulo Makonda. Pamoja na ufinyu wangu juu ya uelewa wa sheria hicho kitendo ni kinyume cha sheria na hakikubaliki katika jamii ya kitanzania.
Baada ya kuona Video za matumizi ya nguvu za Paulo Makonda dhidi ya Clouds Media, tupo tuliosema kuwa kuachwa kwa kitendo hicho ni kitu cha hatari sana kwa Taifa kwani kitaset precedence kwa mamlaka zetu kuanza kawaida ya kutumia nguvu kama tulivyoona kwenye tukio la Nape. Ni matumaini yetu watanzania huyo kijana atakamatwa na kupelekwa mahakamani na apewe haki yake ili kutoa fundisho kwa wengine. Kama kijana huyo ataachwa, basi tujiandae na taifa la matumizi ya vyombo vya moto na solaha nyingine.
Aidha, kitendo hicho (kama aliyekifanya ni sehemu ya usalama wa Taifa) pia kinatoa taswira nyingine kwamba kumbe tatizo la nchi lipo kwenye Idara hii. Wengi tuko matarajio kwamba Idara hii ipo imara, haiyumbi na miongoni mwa najukumu yake ni kuhakikisha taifa linakuwa salama kwa kuweza kufanya forecasting ya mambo yote yatakayoondoa amani na usalama wa nchi yetu. Kwa kifupi kama nchi tuko katika kizaizai kikubwa sana kwani tumaini pekee sasa ni kwa ndugu zetu wa "mabakamabaka".
Tanzania ni kubwa kuliko yeyote, Tanzania ni kubwa kuliko Rais. Tungependa kuona Katiba inafuatwa, inalindwa na inatekelezwa. Haki na Ulinzi wa anaoupata Rais unatokana na Katiba, hivyo iwapo katiba haiheshimiwi, hakuna maana kwa vyombo vyetu kuwalinda wenye kuhatarisha umoja wa Taifa letu ambalo limekuwa kisiwa cha amani katika eneo hili la maziwa makuu.
Nimalizie kwa kutoa rai kwa bunge letu tukufu. Bunge ndio mamlaka pekee inayosimamia serikali. Yatosha kujifunza kwamba mbaya hana rafiki. Fanyeni kazi yenu ya kuisimamia na kuiwajibisha serikali. Sababu mnayo, Uwezo mnao, nguvu mnayo, watanzania wapo nyuma yenu, kilichobaki ni nia thabiti kwenu. Hakuna mtanzania mjinga atakayekataa "kuwarudisha tena mjengoni" iwapo mtafanya maamuzi yenye kulinda hadhi ya Tanzania. Msije kusema watanzania hatukuwaambia.
Mungu Ibariki Tanzania.