Stephen Ngalya Chelu
JF-Expert Member
- Oct 31, 2017
- 8,252
- 18,335
Nimefumba macho. Si kwa sababu nipo usingizini na wala si kwa sababu ni usiku wa giza totoro. Bali ni kwa sababu ya hofu, hofu ya kuiona leo. Hii ni kwa sababu jana ilifanya macho yangu yajawe na simanzi. Na kibaya zaidi ni kuwa, matumaini yangu ya kuiona leo yenye ahueni yanazidi kupotea kwa sababu historia inaninong'oneza kwa sauti thabiti kuwa siku zote leo huwa ni afadhali ya jana.
Nimefumba macho. Sioni chochote. Lakini haimaanishi kuwa natamani kuwa kipofu kwa maana ni heri kuhisi maumivu huku ukikiona kidonda kuliko kutokukiona kabisa.
Nimefumba macho. Sioni chochote. Lakini haimaanishi kuwa natamani kuwa kipofu kwa maana ni heri kuhisi maumivu huku ukikiona kidonda kuliko kutokukiona kabisa.
Mchoro 1: Nimefumba macho, lakini haimaanishi kuwa natamani kuwa kipofu
Nimefumba macho. Lakini matundu ya pua yangu yapo wazi. Pumzi inaingia na kutoka. Inapoingia natamani iyakusanye maumivu na mateso ya jana, iyasukume ndani ya mapafu, yakakae kifuani mwangu, yawe mzigo wangu peke yangu. Si kwa sababu nataka jina langu liandikwe kwenye kitabu cha mashujaa, bali ni kwa sababu nguvu za macho kuhimili kushuhudia maumivu na mateso zinapungua kila jua linapochomoza.
Nimefumba macho lakini masikio yapo wazi. Yanasikia sauti zile zile nilizozisikia jana. Tofauti pekee ni kuwa leo jogoo wa jirani hajasikika akiwika. Hajawika kwa sababu alichinjwa na kuliwa kwa madai kuwa alikuwa akiwika kwa sauti kubwa sana. Inasikitisha kuhukumiwa juu ya kile usichokuwa na hiari nacho. Lakini siku zote mwenye mali ndiye mwenye sauti kuliko yeyote.
Nimefumba macho. Lakini najihisi msaliti. Najihisi msaliti kwangu mwenyewe. Naam, na hata kwa wale ambao uwepo wao haupo bado. Moyo unanisukuma kutenda nilichokitenda jana lakini hisia zinanisinya kwa kunikumbusha madhila niliyoyapata. Lakini habari njema na mbaya ni kuwa, haijalishi ni nini kitashindana nao, siku zote moyo hushinda.
Nimefumbua macho
Sasa naiona dunia. Naiona dunia ikiwa kama nilivyoiacha jana. Tofauti pekee ni uelekeo wa upepo. Jana ulikuwa unavuma kwa kasi kubwa kuelekea kusini. Lakini leo unavuma taratibu kuelekea magharibi. Jambo hili halijabadili chochote. Naam, halijabadili chochote mbele ya macho ya wasioweza kufikiri.
Nageuza shingo yangu, macho yanasafiri umbali mrefu. Loh! Kumbe nilijidanganya maana dunia haipo vile kama nilivyoiacha jana. Imebadilika, imebadilika sana.
Ule mti niliouona jana ukiwa umenawiri, mti uliokuwa ukisifiwa kwa kutoa matunda matamu na kivuli mwanana, leo umeshambuliwa kwa shoka. Japo nauona ukiwa bado umesimama lakini ni wazi kuwa utadodondoka muda si mrefu kwa maana aliyepewa jukumu la kuukata amepumzika kwenye kivuli chake kabla ya kuimalizia kazi hiyo nzito aliyoianza.
Macho yangu yanaachana na mti mahututi na kutazama pembeni kidogo, mara nauona mti mdogo ambao sikuuona jana. Umezungushiwa fito, nadhani ni kwa ajili ya kuukinga na wanyama waharibifu. Ardhi yake imeshibishwa kwa maji na mbolea, mbolea iliyotokana na masalia yaliyooza ya mti uliokatwa juzi. Ama kwa hakika kwa kuutazana unaonekana ni mti wenye bahati njema. Lakini, ni nani aijuaye kesho? Ni nani ajua bahati hiyo njema itadumu kwa muda gani? Kwa maana hata huu ulio mahututi leo ulitendewa wema kama huo jana.
Mchoro 2: Ni nani aijuaye kesho?
Naingia kwenye tafakari. Ni kwa nini mti upandwe jana na ukatwe leo? au ni kwa sababu kuna mti mpya umepandwa leo? Je, kwani haiwezekani kuutunza mti wa jana hata kama unapanda mti mwingine leo? Je, mti wa jana hauna manufaa tena kwa kuwa kuna mti mpya leo? Je, itakuwaje kama mti uliopandwa leo ukafa kabla ya kutoa matunda na kivuli? Lakini mimi ni nani hata nihoji yasiyo yangu. Siku zote mwenye mali ndiye mwenye sauti kuliko yeyote.
Sasa naiona dunia. Namwona yule ombaomba niliyemwona jana, akiwa pale pale na mavazi yale yale aliyokuwa nayo jana na hata juzi. Tofauti ni kuwa jana alikuwa amekunja uso huku akiwa amelifunika bakuli lake la kuombea na leo uso wake umekunjuka kwa tabasamu huku bakuli lake akiwa amelifunua.
Jana alikunja uso na kufunika bakuli ili asijulikane kuwa yeye ni ombaomba. Sarafu alizopewa alizifunika na bakuli ili zisionekane. Alichosahau ni kuwa kinachomfanya aonekane ombaomba si bakuli lake wala mavazi yake chakavu, bali ubongo wake.
Leo anatabasamu. Anatabasamu kwa kila mpita njia. Naam, tabasamu ndiyo mbinu mpya aliyokuja nayo ili kujipatia tonge kwa maana amekaa sana mpaka miguu yake imesahau kusimama. Lakini ni kweli miguu yake imesahau kusimama? Sijui. Ila jambo moja ambalo nina uhakika nalo ni kuwa, unahitajika uongo mwingi sana ili kuuficha ukweli.
Mchoro 3: Amekaa sana mpaka miguu yake imesahau kusimama
Wapita njia wanamtupia tonge kila wafikapo karibu yake. Inaonekana wanampenda sana. Ndiyo, inaonekana wanampenda kwa sababu hawampendi. Inawalazimu kuonyesha wanampenda kwa sababu bila yeye hakuna wao. Ila ni nani wa kumpa ukweli huu? Hakuna. Hakuna wa kumpa ukweli huu kwa sababu ni ukweli anaoufahamu ila amechagua kuishi hivyo huku akisahau kuwa unyonge wake umegeuzwa daraja kwa wengine kujivika 'utu wema' mbele yake.
Jua halijafika hata nusu ya safari yake lakini macho yanakosa uvumilivu wa kuendeleo kuitazama leo. Niliwahi kusikia msemo kuwa, macho huona yanachochagua kuona. Naam, huo ni msemo tu kwa maana kama ingekuwa hivyo nisingechagua kuiona leo na badala yake ningechagua kuuona usingizi usio na ndoto katika jua la leo.
Naitazama leo huku moyo wangu ukiendelea kukatika vipande vipande. Wale niliowategemea wangeweza kuifanya leo iwe njema ni kama wameridhika na hali au wananufaika nayo. Pengine sikupaswa kufikiria kuhusu wao tangu mwanzo lakini tangu lini nyumba ikajengwa na tofali moja. Lakini pia ni hatia kuacha kufikiria kujenga nyumba kisa una tofali moja tu.
Mchoro 4: Naitazama leo huku moyo wangu ukiendelea kukatika vipande vipande
Natamani kufumba macho, lakini ni nani ataisimulia leo katika kesho yenye mpasuko? Ni nani ataisimulia leo katika kesho iliyojaa watu waliofumba macho leo? Ni nani ataisimulia leo katika kesho yenye kiu ya kujenga kesho njema?
Ni mimi.
Nimejitolea kuendelea kufumbua macho ili niione leo japo hisia zinanisinya kwa kunikumbusha madhila niliyoyapata jana. Lakini habari njema na mbaya ni kuwa, haijalishi ni nini kitashindana nao, siku zote moyo hushinda.
Nimefumbua macho.
Upvote
24