Ndoto ya Ujerumani kuitawala Ulaya imetimia?

Ndoto ya Ujerumani kuitawala Ulaya imetimia?

JumaKilumbi

JF-Expert Member
Joined
Sep 7, 2022
Posts
432
Reaction score
507
Na JumaKilumbi,
Septemba 22, 2022.

Ujerumani ni moja ya mataifa yanayofanania na harakati za ‘hustler’ yameanza tokea chini kabisa kwenye hadhi ya udhalili na ufakiri mpaka kufikia utajiri na ufadhili. Harakati zake hazikuwahi kuwa nyepesi, Hali bora ya maisha ya wananchi wake haikushuka kama miujiza toka mbinguni bali ni hesabu na mapenzi mema kwa taifa yasomithilika.
Kwa karne yote ya 20 Ujerumani imekuwa ikitaka kuitawala Ulaya, safari hiyo ndiyo tutaiangazia leo.

Ujerumani kabla ya 1871
Wakati Afrika tunatawaliwa na makampuni ya kizungu huku Machifu wetu wakisainishwa mikataba ya kidhalimu Ujerumani iligawanyika hadi kufikia nchi 37 tofauti, kila moja na Mtawala wake ikijiona bora kuliko mwingine.

Majirani zao Ufaransa na Austria walitumia mgawanyo huu kujinufaisha, walikula rasilimali zake wakashiba kweli kweli.
Baadhi ya wazalendo wa Kijerumani waligundua walipokosea, suluhu walioiona ni kuungana.

Lakini swali la kuungana lilikuwa gumu kupata jibu lake, Falme ya Austria ilipendekeza iundwe ‘Greater Germany’ (Großdeutsche Lösung) ambapo Jamii zote zinazozungumza kijerumani ziunganishwe pamoja chini ya Austria, ‘Ujerumani Kubwa’ hii ingejumuisha majimbo yote ya Falme ya Austria yaliyokaliwa na Wajerumani na hata yale yenye watu wengine kama waSlovak, waUkraine, waItalia, waCzech n.k Wazo hili liliungwa mkono na Wakatoliki wengi.

Wazo hili lilipingwa na Falme ya Prussia, ambayo ilipendekeza iundwe ‘Little Germany’ (Leindeutsche Lösung) ama ‘Ujerumani ndogo’ ambapo yangeunganishwa maeneo ya kaskazini tu huku Austria na majimbo yote ambayo hayakaliwi na Wajerumani yakiachwa nje. Walitaka Ujerumani ‘pure’ ya Wajerumani tu, na hoja hii iliungwa mkono na wajerumani waProtenstant.

Juhudi zilifanywa kuiunda Ujerumani moja, moja ya juhudi hizo ni Wanasiasa toka jamii mbalimbali za Wajerumani walikuja pamoja na kukubaliana kuunda Bunge kulijadili suala hili kwa mapana, katika makubaliano waliona yafaa kuunda ‘Ujerumani ndogo’ ambayo itahusisha jamii za Wajerumani wote ukiacha wale walio chini ya Falme ya Austria.

Mpango huu ulikamilika na wanasiasa hao walimteua Mfalme Frederick William IV wa Falme ya Prussia kuwa kiongozi wao, lakini alikataa.

Alikataa sababu ya kujua ukweli kuwa Falme ya Prussia haikuwa na uwezo kijeshi kutawala maeneo yote yale na haikuwa na uwezo kupambana na Falme ya Austria ambayo ilipambana kwa hali na mali kuona wazo la kuunda ‘Ujerumani ndogo’ katu haifanikiwi,

Kupitia sakata hili Otto von Bismarck alitumia fursa kujipatia imani ya Mfalme Frederick ambaye binafsi yake hakutaka vita na Austria.

Bismarck alifahamika Kuwa miongoni mwa watu waliotaka kuona Prussia inawachapa Austria vitani, lakini siku moja alisimama Bungeni na kupinga vikali hoja za waliotaka vita dhidi ya Austria, Mfalme alimpenda akampandisha cheo.

Otto von Bismarck, kama mwanasiasa nguli alivuta muda na kukuza jeshi la Prussia mpaka kuwa lenye nguvu, hapo akatafuta chokochoko na Falme ya Austria. Mwaka 1866 Jeshi la Falme ya Prussia liliingia vitani dhidi ya lile la Falme ya Austria ambapo jeshi la Prussia lilishinda na kuitia aibu Austria.

Baadae ilatokea vita dhidi ya Ufaransa, Prussia wakashinda kirahisi.
Ushindi wao huo ulizithibitishia falme nyingine za Ujerumani kuwa inawezekana na watakuwa salama chini ya Prussia.

Prussia ikafanikiwa kuziunganisha jamii za Wajerumani na kuunda ‘Ujerumani ndogo’ (leindeutsche Lösung).

HARAKATI ZA UJERUMANI KUITAWALA ULAYA KARNE YA 20
Tangu Ujerumani kuwa taifa mambo kadhaa yalibaki kuwa kitendawili vichwani mwa Wajerumani wengi.

Siasa na Mikakati ya Kijiografia.
Kabla ya Ujerumani kuungana Wababe wa Ulaya walifahamiana, Uingereza, Ufaransa, Urusi na Austria-Hungary. Lakini mara tu nchi ya Ujerumani kuibuka kwenye ramani ‘balance of power’ Ulaya ilitikisika, maana lilitokea dubwana kubwa, lenye nguvu halafu katikati ya Ulaya likiligawanya bara upande wa mashariki na magharibi.

Uwepo wa Ujerumani ulitazamwa kwa jicho tofauti na mataifa yaliyokuwepo;

Urusi 🇷🇺
Iliiona Ujerumani kama ‘Buffer zone’ itakayoilinda Urusi dhidi ya Ufaransa, kama vita baina yake na Ufaransa ingezuka.

Uingereza 🇬🇧
Mpaka kati yake ya Ujerumani ni nchi ndogo za Uholanzi, Ubelgiji kisha Bahari ya Kaskazini ikimaanisha shambulio lolote la Ujerumani kwenda Uingereza lililazimika kuhusisha jeshi la majini na angani, na Uingereza ilikuwa na jeshi bora zaidi na majini wakati huo, hivyo kwao Ujerumani halikuwa tatizo kubwa.

Ufaransa 🇫🇷
Kabla ya Ujerumani kuungana Ufaransa alikuwa ni kama mtawala mwenza wa ardhi za wajerumani akishirikiana na Austria-Hungary, waliingia na kutoka kadri walivyotaka.

Ujerumani kuungana kulimaanisha zama za Ufaransa kutawala ardhi za Wajerumani zimekwisha! Na wao kushindwa vita na Ujerumani mwaka 1870-1871 ilimaanisha dhahiri kuwa Ufaransa hawana uwezo wa kujilinda dhidi ya Ujerumani.

Austria-Hungary, 🇦🇹
Austria wenyewe ni wajerumani wakatoliki ambao walikuwa wakijichukulia kuwa viongozi wa Wajerumani, kwakuwa walikuwa na Dola kubwa iliyotawala ardhi za wajerumani na wasio wajerumani na ni wao walipendekeza Muungano wa wajerumani wote kuunda ‘Ujerumani kubwa’ (Großdeutsche Lösung).

Hivyo Ujerumani hii kwao ilikuwa ni mbadala wa Austria-Hungary kumaanisha zama za tawala za Austria zimefika tamati.

Ujerumani 🇩🇪
Kwa Wajerumani wenyewe nchi hii mpya ilimaanisha faraja na tumaini baada ya miaka mingi ya kugawanyika na udhalili.

Ujerumani hii ilijihisi kuzungukwa maana iliwekwa ambakati na maadui zake, Magharibi yupo Ufaransa, Kaskazini yupo Uingereza, Mashariki yupo Urusi na Austria.

Ujerumani iliiona Ufaransa kama tishio maana inapakana nae ardhi, Uingereza haikuipa tabu sana maana wana mpaka wa bahari lakini jeshi la maji la Uingereza liliendelea kuwa tishio kwao, Urusi upande wa Mashariki pia haikutoka vichwani mwa majenerali wa kijerumani, Austria ilikuwa ni dola inayoanguka hivyo haikuipa tabu sana kuifikiria.

Kutokana na hali hiyo kijiografia iliilazimu Ujerumani kuja na mkakati tiba ili kujilinda.

Chokochoko za Balkan na WWI
Kabla Ujerumani haijakaa vizuri ndugu zao Austria-Hungary walikuwa na madai yao huko Balkan, lakini kutokana na kutokuwa na jeshi imara hawakuweza chukua hatua.

Lakini mwanamfalme wa Austria Franz Ferdinand na mkewe Sofia alipokuwa kwenye ziara ya kijeshi huko Sarajevo, Bosnia na Herzegovina, wanaharakati wa Serbia waliiona hii ni fursa kuwaonesha Austria-Hungary kuwa hawataki kuingiliwa mambo yao, zikapangwa njama na ilipojiri saa 5 na dakika 15 asubuhi ya Juni 28, 1914 mwanamfamle huyo na mkewe wakauwawa.

Kwa Austria-Hungary suala hili halikukubalika na walitumia kama sababu ya kutimiza yale yote waliyokuwa wakiyataka huko Balkan, kitu cha kwanza walitafuta uungwaji mkono wa Ujerumani, mfalme wa Ujerumani akawahakikishia ‘sapoti’, kisha wakatuma ‘Ultimatum’ yenye masharti magumu kwa Serbia ambayo kwa uoga waliyakubali isipokuwa mawili tu.

  1. Kuwafuta kazi baadhi ya maafisa wa jeshi lake
  2. Maafisa wa kijeshi wa Austria-Hungary waingie Serbia katika safishasafisha ya watu wote wanaoenda kinyume na maslahi ya Austia-Hungary

Julai 28, 1914 mizinga ya Austria-Hungary ikaanza kurindima kuwatwanga waSerbia.

Urusi kuona Serbia, mwanawe wa kumzaa, anashambuliwa wakaanza kukusanya jeshi mpakani na Austria-Hungary, na Austria-Hungary wakaanza kusanya jeshi mpakani na Urusi huku yuko vitani na Serbia.

Ujerumani ambayo inamuona Austria-Hungary kama nduguye na ilimpa hakikisho la ulinzi endapo vita ikatokea ikaamua kutuma ‘Ultimatum’ Julai 31, 1914 kuitaka Urusi kuacha mara moja kukusanya jeshi dhidi ya Austria ndani ya masaa 24.

Pia ikatuma ‘Ultimatum’ kuwataka Ufaransa ndani ya masaa 18 kuahidi kuwa hawataingilia vita ya Ujerumani na Urusi.

‘Ultimatum’ hizo zote zilitupiliwa mbali na ile ndoto mbaya ya Ujerumani kuwekwa ambakati na maadui ikatimia, kesho yake Agosti 1, 1914 Ujerumani ikatangaza vita dhidi ya Urusi, na siku mbili baadaye ikatangaza vita dhidi ya Ufaransa.

Wakati Wajerumani wanakwenda kuitwanga Ufaransa njiani wakazichukua ardhi za Luxembourg na Ubelgiji, Uingereza alikuwa na makubaliano ya kuilinda Ubelgiji dhidi ya uvamizi wowote ule, hivyo ikawalazimu kutangaza vita dhidi ya Ujerumani kwa sababu ya Ubelgiji siku hiyo hiyo.

Mambo yakazidi kuwa mabaya kwa Ujerumani akawa anapigana vita pande tatu.

Vita ikachukua taswira mpya, Austria-Hungary ilitangaza vita dhidi ya Urusi mnamo Agosti 5; Serbia dhidi ya Ujerumani mnamo Agosti 6; Montenegro dhidi ya Austria-Hungary mnamo Agosti 7 na dhidi ya Ujerumani mnamo Agosti 12; Ufaransa na Uingereza dhidi ya Austria-Hungary mnamo Agosti 10 na Agosti 12, mtawalia; Japan dhidi ya Ujerumani mnamo Agosti 23; Austria-Hungary dhidi ya Japan mnamo Agosti 25 na dhidi ya Ubelgiji mnamo Agosti 28.

Kwa Ujerumani hili halikuwa ‘suprise’ maana kabla ya vita walishaona kuwa ipo siku watalazimika kupigana pande mbili, dhidi ya Ufaransa na Urusi. Hivyo mipango kadhaa ilikwishasukwa, katika mipango hiyo mpango uliowafaa zaidi ni ule wa ‘Schlieffen Plan’

Mpango huu ulieleza hatua kwa hatua nini kifanyike hali hiyo ikitokea.
Ilipendekezwa kuwa Ujerumani ianze kuitwanga Ufaransa huku ikiizuga Urusi kwa jeshi dogo kwakuwa walikadiria kuwa Urusi kutokana na kukosa miundombinu ya kisasa, kuwa na nchi kubwa, na Urasimu wa kizamani wa jeshi lake wangechukua muda mrefu zaidi kukusanya jeshi, hivyo ingeipa Ujerumani muda wa kutosha kuizima Ufaransa kwa nguvu zake zote na baadae kuhamia kuitwanga Urusi.

Kwa sehemu mipango iliwaendea sawa kabisa Wajerumani mpaka pale Marekani walipoingilia vita.

Kilichoiingiza Marekani ni vitendo vya Ujerumani kushambulia meli za kiraia za Marekani zilizokuwa zikisafirisha bidhaa kwenda kwa ‘Allied powers’.

Kama hilo halikutosha mwaka 1917 Marekani ilikamata ujumbe uliotoka Ujerumani kwenda Mexico uliolenga kuishawishi Mexico kutangaza vita na Marekani huku ikiahidiwa kupewa majimbo ya sasa ya Marekani ya California, Nevada, Utah, sehemu kubwa ya Arizona, nusu ya magharibi ya New Mexico, robo ya magharibi mwa Colorado, na kona ya kusini-magharibi ya Wyoming.
Majimbo haya yalikuwa ya Mexico zamani, yaliporwa na Marekani wakati wa vita vya 1846-48 kati ya Mexico na Marekani.

Kwa upande wa mashariki Ujerumani alipokuwa akipigana dhidi ya Urusi na Romania mambo yalikuwa mazuri sana kiasi kufikia Mei 7, 1918 Urusi na Romania zilishaanguka na Ujerumani na washirika wake walishinda vita.

Aprili 17, 1917 Marekani ilitangaza vita dhidi ya Ujerumani, kuingia kwa Marekani Vitani ilikuwa ni ‘Game changer’, iliyaongezea nguvu majeshi ya ‘Allied powers’ upande wa Magharibi na kuwawezesha kuwafurusha Wajerumani toka Ufaransa.

Novemba 11, 1918 Ujerumani ilishindwa vita rasmi na kulazimima kusaini mkataba wa kusitisha mapigano, na Disemba 1, 1918 majeshi ya Uingereza na Marekani yaliingia ndani ya ardhi ya Ujerumani kutamatisha vita.

Mkataba wa Versailles ulisainiwa, Ujerumani ikaunda mfumo mpya wa shirikisho kuendesha serikali yake na kuachana na mfalme wao Wilhelm II, na ikawa inatambulika kama ‘Weimar Republic’ ikaadhibiwa vikali hali yake ikawa dhoofu, kutengwa kimataifa, mfumuko bei na kugombea madaraka ikawa ni ada ya kila siku kwa Wajerumani.

HITLER NA ‘UKOMBOZI WA UJERUMANI’
Miaka mingi ya mateso ikamleta Hitler, aliyeonekana mtetezi, muokozi na mlinzi wa Wajerumani.

Jamaa akasimama imara, akajenga reli, viwanda, akaajiri watu na akafufua jeshi la Ujerumani! Kimsingi alifanya vyote hivyo na ndio sababu Al Habib Kanju anavutiwa sana na huyu jamaa.

Akapiga marufuku vyama vya wafanyakazi, vyama vya upinzani, akabinafsisha mashirika ya umma, akaunga mkono wafanyabiashara na akaongeza bajeti ya jeshi mara dufu zaidi ya iliyokatazwa na ‘Versailles peace treaty’
Ujerumani ikapata matumaini tena, japo hofu haikuisha.

Kufufuka kwa ndoto ya kuitawala Ulaya
Fikra za Ujerumani kuitawala Ulaya hazikufa, na safari hii Hitler aliwaambia Waingereza na Wafaransa kuwa Wajerumani wanataka ‘sehemu ya kuishi’ (lebensraum), akimaanisha kuwa baada ya kupokonywa makoloni 1919 ardhi ya Ujerumani haiwatoshi!
Mwaka 1938 Wajerumani wakaingia Austria, baadae wakayatwaa baadhi ya maeneo ya Czechoslovakia.

Uingereza na Ufaransa wakakubali kutambua maeneo mapya ya Ujerumani wakiamini kuwa wataishia hapo. Lakini ikawa tofauti.

Mwaka 1939 Ujerumani ikataka kuivamia Poland, lakini wakahofu USSR ingeingilia hivyo kulituliza hilo Ujerumani ikaingia mkataba wa kutoshambuliana na USSR, pia walikubaliana kwa siri kugawana Poland!

Poland wao walisaini makubaliano na Uingereza ‘mutual assistance agreement’

Hitler hakujali, Septemba 1, 1939 Ujerumani ikaivamia Poland, Septemba 3 Uingereza na Ufaransa wakatangaza vita dhidi ya Ujerumani.

Wajerumani walizamisha meli nyingi za Uingereza na kuituliza kwa muda, huku ikizikalia Uholanzi, Ubelgiji, Luxembourg na kuikaba koo Ufaransa.

Wakati huo Wakaitwaa Poland na kuigeuka USSR, hapo ndipo walipokosea hesabu. Katika vita yao na USSR walisababisha mauaji ya mamilioni ya askari wa USSR na kuitia hasara kubwa sana.

Wakati wanaelekea kushinda vita mwaka 1944 Upepo ukabadilka…
Uingereza, Marekani na Canada wakavamia fukwe za Ufaransa walikokuwa wamepateka na kuwasha moto upya.

USSR nayo ilistahimili mapigo na kuanza kurudisha, Ujerumani ikajikuta mtu kati kwa mara nyingine, mwaka 1945 ilisalimu amri na vita kutamatika.

Kwa mara nyingine Ujerumani ikashindwa timiza azma yake ya kutawala Ulaya.

Ujerumani yagawanywa tena
USSR, Ufaransa, Uingereza na Marekani ikaigawa Ujerumani vipande vinne na kuikalia.

Uingereza, Marekani na Ufaransa waliamua kuunganisha maeneo waliyoyakalia na kuunda nchi ya Ujerumani Magharibi, USSR nayo ikatangaza kuunda nchi ya Ujerumani mashariki.

Ujerumani Magharibi ikajazwa misaada toka Marekani, uchumi wake ukanyanyuka na kuboreka zaidi, Ujerumani mashariki kutokana na sera za kikomunisti ikadhoofika na kuwa masikini. Kwa mara nyingine tena Wajerumani wakagawanyika!

UJERUMANI YABADILI MBINU YA KUITAWALA ULAYA ?
Kuna msemo unasema “If you can’t beat them join them”, na hapa ndio maana yake hudhihirika.

Baada ya vita Wafaransa wakaona njia pekee ya kuidhibiti Ujerumani ili isitokee tena Vita baina yao ni kuungana nao maana mara zote katika vita za dunia Ujerumani lazima aishambulie Ufaransa.

Ufaransa ikapendekeza kuiweka karibu Ujerumani kisiasa na Kiuchumi wakiamini kwa kufanya hivyo hakutakuwa na mgogoro tena baina yao.

Jitihada zilifanywa na mwaka 1957 ikaundwa European Economic Community (EEC) ambamo Ujerumani Magharibi na Ufaransa wakawa wanachama muhimu pamoja na nchi nyingine. EEC ikakua na baadaye kubadili jina na kuitwa European Union (EU) na bado Ujerumani na Ufaransa wameendelea kuwa wanachama muhimu.

UJERUMANI IMEIKAMATA ULAYA KWA SASA?

Wataalamu husema “Vita ni Uchumi”, Kwa sasa Ulaya kote Ujerumani ndiye nchi inayoongoza kuwa na uchumi imara, na ndiyo nchi inayoongoza kwa ushawishi mkubwa EU.

Ni ngumu kuzungumzia EU bila kuigusa Ujerumani, Ujerumani ni EU na EU ni Ujerumani!

GDP- Mwaka 2021, Benki ta Dunia ilikadiria Ujerumani kuwa na GDP dola za kimarekani Trilioni 4.22.

European debt crisis’ 2009- katika janga hili Ujerumani ilisimama kidete kutatua na misingi iliyotumika ni yenye kulinda maslahi ya kitaifa ya Ujerumani.

Janga la wakimbizi 2015/16- Ujerumani iliamua, bila kuwashirikisha wengine kuwapokea wakimbizi waliokataliwa na nchi za Ulaya mashariki na kupelekea athari kwa wanqchama wote.

Japo haina jeshi kubwa kama Ufaransa na Uingereza lakini Ujerumani ina uchumi mkubwa na ina uwezo wa kushawishi sera na nchi nyingine Ulaya kwa kupitia kivuli cha EU,
Katika nafasi za juu za EU si ngumu kukutana na Wajerumani wengi kwenye idara nyeti.
Ushawishi huu wa Ujerumani ndani ya Ulaya unaongezeka kila kukicha, na tangu mwaka 2014 Ujerumani ilitumia 1.1% ya GDP yake kwenye masuala ya kijeshi,
2017- 1.2% ya GDP
2019- 1.3% ya GDP
2020- 1.4% ya GDP

Wakati huu Urusi inapigana Ukraine, Ujerumani inaitwaa Ulaya, Uchina inajiandaa kwa Taiwan je, Vita ya tatu ya Dunia inakaribia?

Swali limebaki je EU ni mpango wa Ufaransa 🇫🇷 na Marekani 🇺🇸kuidhibiti Ujerumani 🇩🇪 au ni mpango wa Ujerumani 🇩🇪 kuitawala Ulaya 🇪🇺?

Copyright © 2022 - 2030 JumaKilumbi
Some rights reserved. Ruksa kunakili na kusambaza andiko hili kwa sharti la kutobadili chochote!
 

Attachments

  • 89715CBA-DE91-45A1-A894-578847554E5D.jpeg
    89715CBA-DE91-45A1-A894-578847554E5D.jpeg
    32.9 KB · Views: 20
  • 47B193B6-1FE2-47CD-B663-958940855ED4.jpeg
    47B193B6-1FE2-47CD-B663-958940855ED4.jpeg
    47 KB · Views: 21
  • 50EB5202-A99A-418A-9BA5-49DBA7C77F29.jpeg
    50EB5202-A99A-418A-9BA5-49DBA7C77F29.jpeg
    26.9 KB · Views: 20
  • 8656AF2A-423E-49D0-9843-17A188DC9D33.jpeg
    8656AF2A-423E-49D0-9843-17A188DC9D33.jpeg
    30.2 KB · Views: 21
  • F6CC459C-92E7-4B56-808E-70B6116C93DF.jpeg
    F6CC459C-92E7-4B56-808E-70B6116C93DF.jpeg
    25.7 KB · Views: 19
  • 2BC5DDB7-2DC4-4121-9227-8ACC5974883E.png
    2BC5DDB7-2DC4-4121-9227-8ACC5974883E.png
    89.1 KB · Views: 22
Juma...mimi sikujui ila nimeona unajulikana...nina miaka 18 tokea niliposoma gazeti la philadelphia trumpet..la mwaka 1996 ...
Una akili
Unajitambua
Na uko mbele ya muda wako(ahead of your time)

Germany ndio ataanzisha vita ya tatu ya dunia
Alianzisha ya kwanza
Akaanzisha ya pili
Na ataanzisha ya tatu....

Yeye na russia au either Iran....

Mfalme wa kaskazini na wa kusini....

MUNGU NDIO ANAJUA...
 
Juma...mimi sikujui ila nimeona unajulikana...nina miaka 18 tokea niliposoma gazeti la philadelphia trumpet..la mwaka 1996 ...
Una akili
Unajitambua
Na uko mbele ya muda wako(ahead of your time)

Germany ndio ataanzisha vita ya tatu ya dunia
Alianzisha ya kwanza
Akaanzisha ya pili
Na ataanzisha ya tatu....

Yeye na russia au either Iran....

Mfalme wa kaskazini na wa kusini....

MUNGU NDIO ANAJUA...
Shukran Mkuu I appreciate that, really.
 
Back
Top Bottom