Tangu kuanzishwa uzi huu, wamejitokeza wakuu kuupinga kwa nguvu zote huku wakipaza sauti zao kujaribu kuwahadaa wengine kwamba punyeto ni jambo jema. Namshukuru Mungu kwa sababu ya wale walioguswa na huu ujumbe na moja kwa moja wakaamua kuchukua hatua. Kwa Mungu hakuna kuwahi wala kuchelewa, hapo hapo ulipoanzia atakufanya upya nawe utakuwa na amani katika siku zako zilizosalia hapa duniani. Napenda kuwatia moyo kwa ujumbe huu mfupi:
Luka 18
35 Ikawa alipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya njia, akiomba sadaka;
>> Sisi sote tumekuwa vipofu kwa sababu hatujaona siri za ufalme wa Mungu. Licha ya Kristo kujidhihirisha kwetu, bado hatukuikubali kweli na kujidhani tunaona. Lakini Yeye asemaye: (Yohana 9
39 Yesu akasema, Mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa hukumu, ili wao wasioona waone, nao wanaoona wawe vipofu.
40 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwapo pamoja naye wakasikia hayo, wakamwambia, Je! Sisi nasi tu vipofu?
41 Yesu akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa).
Kwa hiyo tatizo sio kuwa tu vipofu, bali ni kukubali kwamba sisi ni vipofu!!
36 na alipowasikia makutano wakipita, aliuliza, Kuna nini?
37 Wakamwambia, Yesu wa Nazareti anapita.
38 Akapiga kelele, akisema, Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu.
>> Sasa mimi ni chombo tu, nimetumika kufikisha ujumbe wa ufalme wa Mungu. Wale waliosikia, wengine wameuliza kuna nini? Hawa ni wale waliojigundua kuwa ni vipofu na hawakuwahi kuiona nuru ya Kristo. Pale walipojibiwa kuna neno la Kristo linapita hapa jukwaani, wakaamua kupaaza sauti wakiomba rehema ya Mungu. Wakatambua mara kuwa wanahitaji msaada wapate kuona, wanahitaji rehema ya Mungu, sio macho!! Kwamba wametambua wamemwasi Mungu na kutumbukia gizani, hivyo dawa si macho, bali ni huruma ya Mungu ili awatoe gizani kwani wamekuwa vipofu hawawezi tena kuona njia.
39 Basi wale waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza sauti, Ee Mwana wa Daudi, unirehemu.
>> Hapa liko tendo linaloendelea hata sasa. Mtu akiisikia sauti ya Kristo na kuamua kupaza sauti akimwita, WALIOTANGULIA, wale wanaodhani wanaona wala si vipofu, hujaribu sana kumkemea mtu huyu. Hujaribu kumnyamazisha, hawataki Kristo ampe attention, wamemmiliki Kristo. Ni namna ya mabaunsa wa leo makanisani. Ni aina ya wale waliowahi kusikia habari za Kristo na kudhani wamemjua vema. Ni vipofu wakubwa wa kiroho, wakimlinganisha Kristo na kile wanachokiamini wao.
40 Yesu akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza,
41 Wataka nikufanyie nini? Akasema, Bwana, nipate kuona.
42 Yesu akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya.
43 Mara hiyo akapata kuona, akamfuata, huku akimtukuza Mungu. Na watu wote walipoona hayo walimsifu Mungu.
>> Lakini Kristo Yesu anashughulika na mtu mmoja mmoja. Ukimwita kwa kukusudia hayuko mbali. Atakuja kwako na swali lake kwako ni moja tu, UNATAKA NIKUFANYIE NINI? Hapa ndipo penye imani ya watakatifu, usibebwe na imani ya wengi. Jenga uhusiano wako na Mungu huku ukikusanyika kumsifu na kumtukuza.
Acha kusikiliza sauti za pembeni pale unapoamua kumtafuta Kristo, kwani wengi hujitokeza na kukuvunja moyo. Ndivyo ilivyo hata sasa, ukiamua kiachana na mfumo wa dunia hii, ndipo sasa sauti za upinzani zitaamka dhidi yako. Ni kipindi kigumu mno chenye kila aina ya majaribu. Unajua ni kwa nini huwa hivi?
SIRI: Pale unapokuwa kwenye ufalme wa giza, shetani hana shughuli na wewe kwa sababu tayari keshakupata, ndio maana utaona kama unaishi vizuri tu. Huwezi kumhangaikia mkeo kumtongoza akupe unyumba, lakini asiye mkeo huyo atakufanya ulipe gharama kubwa kumpata. Ndio maana mwanamke ataendelea kuwa mgumu kumpata mpaka pale atakaposajiliwa kwenye ufalme wa giza, ambako huvikwa bango usoni pake. Hapo ndipo kila mwenye kumhitaji husoma bango alilovikwa mwanamke huyu na kujua gharama zake. Akiwa tayari kuzilipa atampata kirahisi tu.
Ndivyo ilivyo kwa mwanamume mzinzi, huyu tayari kavikwa bango kwenye paji la uso. Hutokwa kwa gharama ndogo tu. Mwanamke akiacha mapaja nje, tayari macho hutiwa upofu, mwanamke akimlegezea macho akili huhama. Ni aina ya msukule ingawa anajidhani yuko hai. Kiukweli anaishi katika giza na hawezi kamwe kutoka humo mpaka apate mtu wa kummulikia mwanga aweze kuona njia.
Kwa hiyo ukiamua kumfuata Kristo tarajia vita kali sana, kutoka ndugu na jamaa wanaokuzunguka. Kumbuka Kristo alikuja kuleta upanga!! Shetani hawezi kukuacha kirahisi, utashangaa hata mambo ya dhambi uliyokuwa ukiyasotea siku za nyuma, ghafla yamekuwa mepesi mno kuyapata. Afu utaona kule unakojaribu kuhamia kumegeuka ukame na hakuna maisha. Ukiona hivyo tambua kwamba uko kwenye njia sahihi na kwamba hayo majaribu ni ya muda tu ili kuimarisha imani yako. Kwamba umeshatambua dunia na anasa zake si chochote, umepata kitu cha thamani kubwa zaidi ya hivyo. Ukisimamia ukiri huo, Kristo atakushika mkono na kukutoa katika bonde la uvuli wa mauti na kukuingiza kwenye malisho ya majani mabichi.
Kikubwa hapa, usijenge imani kwa mwanadamu kamwe, sisi tunapeana habari njema azinazookoa tu, lakini kazi ya kuokoa hufanywa na Roho Mtakatifu mwenyewe. Kwa maana hiyo sisi tumekuwa mabalozi wa ufalme wa Mungu. Balozi hawezi kuwakilisha matakwa yake ila ya yeye aliyempeleka. Hivyo usiseme, napenda sera za balozi wa Uingereza, bali useme, napenda sera za serikali ya Uingereza.
Amani ya Kristo ipitayo fahamu zetu ikae nanyi daima.
Amina.