BARD AI
JF-Expert Member
- Jul 24, 2018
- 3,591
- 8,826
Katika kosa la bughudha ya kijinsia (Sexual harassment)
Sheria inaeleza kwamba, mtu yeyote ambaye kwa dhamira atamshambulia, au atatumia nguvu kinyume cha sheria akambughudhi mtu mwingine kijinsia au kwa kutumia maneno au vitendo na kusababisha maudhi au bughudha kijinsia kwa mtu mwingine, basi mtu huyo aliyembughudhi mwingine atahesabika kisheria kama ametenda kosa la bughudha ya kijinsia.
Adhabu ya Kosa la Bughudha ya Kijinsia
Adhabu ya mtu atakayetenda kosa la bughudha ya kijinsia pindi akipatikana na hatia ni kifungo kisichozidi miaka mitano au faini isiyozidi shilingi laki mbili au atahukumiwa adhabu zote mbili yaani kifungo pamoja na faini kama ilivyoelezwa hapa juu na pia anaweza kuamuriwa kulipa fidia kwa kiasi kitakachotathiminiwa na mahakama kulingana na athari alizozipata muathirika.
Aidha sheria inasisitiza zaidi katika kuainisha kosa la bughudha ya kijinsia kuwa mtu yeyote atakeyedhamiria kudhalilisha utu wa mwanamke au msichana kwa kutumia maneno, kutoa sauti au kuonesha ishara au kwa kuonyesha kitu chochote ikiwa ni pamoja na kuonyesha kiungo chochote kiwe cha kiume au cha kike kwa kudhamiria kwa maneno au sauti hizo zisikike au ishara au kitu hicho kiweze kumwingilia sehemu za siri mwanamke au msichana, basi mtu huyo atakuwa ametenda kosa la bughudha ya kijinsia.
Kwa kutafsiri shambulio katika kipengele hiki itajumuisha matendo yote ambayo si kubaka kwa mujibu wa sheria hii. Ili kuondoa wasiwasi wowote wa kimaana, bughudha za kijinsia zitahusisha matendo yote ya kumtaka bila ridhaa mwanamke kimapenzi kwa kutumia maneno au vitendo kwa mtu aliyeko madarakani katika sehemu za kazi.
Ukomo wa Kupeleka Shauri la Bughudha ya Kijinsia
Shauri lolote la bughudha za kijinsia linapaswa kufikishwa katika vyombo vya sheria na mtu aliyeathirika na bughudha hizo muda wowote lakini isizidi siku 60 toka tukio la bughudha lilipotokea.