Ukweli wazee wengi hao unaowaita ni wamjini, elimu walikuwa hawana. Walikuwa wanaungaunga tu. Ujanja wa mdomoni tu
ABBAS SYKES (1929 - 2021) SEHEMU YA TATU: KING'S COLLEGE BUDO SHULE MOJA NA KABAKA EDWARD MUTESA WA UGANDA 1940s
Siku moja katika mazungumzo na Balozi Sykes akaniambia kuwa yeye baba yake alimtoa Kitchwelle Boys Government School na kumpeleka Kampala Uganda kwa ajili ya kupata elimu.
Balozi anasema yeye hakuwa anajua ni shule gani baba yake alikuwa anataka kumpeleka lakini walipokuwa Nairobi wakiwa pale hotelini wakisubiri safari ya kwenda Kampala baba yake akakutana na jamaa wa Kinubi na katika maongezi baba yake akawaeleza kuwa alikuwa katika safari anaelekea Uganda kumpeleka kijana wake shule.
Basi mmoja wao katika wale jamaa wa Kinubi akamwambia Kleist kuwa shule nzuri sana ni King's College Budo kama ana uwezo na itakuwa vyema kama anatampeleka mtoto wake shule hiyo.
Hapo King's |College Budo ndipo Abbas Sykes ailipokuja kusoma na Freddie Mutesa ambae baadae akajakuwa Kabaka wa Buganda na Rais wa Uganda mwaka 1962 Uganda ilipopata uhuru.
Balozi Sykes anakumbuka kumuona mama yake Freddie Mutesa akiwa kavaa yale magauni ya Kiganda akija shule kumtembelea mwanae na jinsi shule nzima ilivyokuwa ikitetemeka kwa ujio wa bi. mkubwa yule kwani Freddie ndiye aliyekuwa akitegemewa kuwa Kabaka wa Uganda.
Wote Abbas Sykes na Freddie Mutesa katika utawala wa kikoloni wakahusika kikamilifu katika kupigania uhuru wa nchi zao.
Inasikitisha kuwa kutoka miaka ile ya 1940 wazalendo hawa hawakupata tena kuonana wakati nchi zao washazikomboa kutoka kwa Muingereza na labda kwa kuwa Kabaka Mutesa alipunduliwa mwaka wa 1966 na kwenda kuishi uhamishoni Uingereza ambako alifariki mwaka wa 1969.
Miaka hiyo Abbas Sykes tayari alikuwa kwenye ubalozi wa Tanzania Ufaransa na Canada.
Hii shule King's College Budo ina sifa ya pekee katika shule za Afrika ya Mashariki kwani viongozi wengi na watu mashuhuri wamesoma hapo kutoka Uganda kwenyewe, Kenya hadi Nyasaland na wenyewe wanajiita Budoians.
Hii ni ''club,'' pekee ya wasomi kama Yusuf Lule, Godfrey Binaisa na Charles Njonjo kwa kutaja majina maarufu katika siasa za Afrika ya Mashariki.
Balozi Sykes anamkumbuka baba yake kwa mapenzi makubwa sana.
Balozi mara nyingi akinambia kuwa, ''Sisi baba yetu alitujengea msingi mzuri sana wa maisha na alipofariki aliacha jina kubwa la ukoo wetu.
Hakuna mahali ambako baba yetu hakuacha alama yake kuanzia kwenye siasa, biashara na katika dini ya Kiislam hasa katika kuwasomesha watoto wa Kiislam wake kwa waume.
Yeye na wenzake akina Ali Jumbe Kiro walijenga ile shule ya Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika.
Mungu akajaalia kuwa Bwana Abdul baada ya kifo cha baba yetu mwaka wa 1949 yeye akavaa viatu vya baba na vikamuenea vizuri sana ndani ya TAA hadi kuasisi TANU mwaka wa 1954.
Hapa ikawa tumekuwapo katika African Association mwaka wa 1929 na tukawepo katika kuunda TANU mwaka wa 1954.
Balozi akipenda sana kunitania kwa kuniita, ''Yaa Mohamed, unaiona Sykes dynasty?''
Nakumbuka siku nilipomtembelea baada ya Kleist Abdul Sykes kuchaguliwa kuwa Mayor wa Dar es Salaam.
''Unajua Mohamed somo yake alikuwa Mwafrika wa pili kuchaguliwa katika board ya Dar es Salaam Municipal Council kwa hiyo Kleist kafuata nyayo za babu yake,'' Balozi aliniambia kwa furaha.
Mwafrika wa kwanza kuchaguliwa katika board hiyo alikuwa Juma Mwindadi.
Mwandishi na Abbas Sykes katika mahojiano ya kipindi cha televisheni 2012