Naheshimu mawazo yako, na mengine uliyoyatamka, nakubaliana nawe. LAKINI kuniambia kuwa labda mimi ni mmoja wa walamba asali, hukunitendea haki. Ni kunitusi.
Sijawahi kulamba asali wala hata sijui inalambwa vipi. Katika maisha yangu yote sijawahi kuwa mwajiriwa wa Serikali wala taasisi yoyote ya Serikali. Hiyo asali nitailamba wapi na kwa namna gani? Kama kuna asali, ambayo ningeweza kuisubiria kwa hamu, ni sera nzuri za uchumi. Nimefanya kazi nje kwa muda mrefu, na sasa naona ni wakati wa kuwekeza, hata kwa kiasi kidogo, nchini mwangu. Tujadiliane kwa hoja bila kutwezana.
Jambo moja ninalokubaliana nawe ni kuwa maisha ya wafanyabiashara wengi wa Tanzania ni ya kuviziana. Hakuna ethics za biashara. Ndiyo maana unaweza kumwona machinga amebeba shati, unamwuliza bei gani, anakutazama kwanza wewe unayemwuliza upoje. Wewe utaambiwa sh 30,000. Utanunua kwa sh 30,000, mwingine shati hilo hilo atanunua kwa shilingi 10,000!
Kauli ya Rais kuwa vitu vimepanda Duniani kote kwa sababu ya vita, na hapa kwetu vimepanda bei, ma vitaendelea kupanda, kwa kuzingatia jamii ya wafanyabiashara wa hapa kwetu, haikuwa kauli nzuri maana ilikuwa ni kama kuwaambia kuwa wapandishe bei.
Nadhani ni wakati sahihi sasa kuweka sheria ya Business ethics. Kwa mfano, sheria itamke kuwa mfanyabiashara yeyote anayetumia mazingira ya uhaba wa bidhaa yoyote kujipatia faida halisi (net profit) zaidi ya 50%, atakuwa amekiuka sheria ya maadili ya biashara. Na anayekiuka sheria ya maadili ya biashara aadhibiwe, na kisha kupewa muda wa matazamio.
Lakini pale ambapo ongezeko la bei ya bidhaa yoyote ile ni halisia, hatuna namna nyingine zaidi ya kukabiliana na hali hiyo, au kama bidhaa hiyo ni kiwezeshi cha uzalishaji au kiwezeshi cha uchumi, Serikali iweke ruzuku. Lakini kama hakuna ruzuku, na gharama za uzalishaji zipo juu, mzalishaji ili kulipia gharama za uzalishaji atalazimika kuuza kwa bei kubwa, hakuna namna.