Robert Heriel Mtibeli
JF-Expert Member
- Mar 24, 2018
- 28,297
- 68,017
LISSU UMENISIKITISHA SANA, NILIKUWA SAHIHI KUSEMA UENGULIWE NA NEC. ONA SASA!
Na, Robert Heriel
Kipindi cha mchakato wa NEC kuteua wagombea watakaopeperusha bendera za Urais kupitisha vyama vya siasa hapa nchini, nilipendekeza kuwa Tundu Lissu aenguliwe kwa maslahi ya Muungano. Nilisema, Tundu Lissu sio tishio huku bara, hawezi kushinda huku bara, lakini hofu yangu ipo Zanzibar. Macho yangu yaliona kitakachotokea. Sijajua kwa nini NEC ilimpa nafasi, je mlimpuuza, au mlijua ananguvu ndogo bara hivyo mkasahau ya Zanzibar?
Tundu Lissu ni Rafiki yangu, ndugu na jamaa wangu wa karibu wanajua jinsi ninavyomfagilia. Lakini haiondoi ukweli kuwa Kupita kwake NEC kutaleta athari zaidi huko Zanzibar.
Tundu Lissu umeniudhi sana, hatuwezi kumchagua mtu anayetaka kuvunja umoja wetu. Hatuwezi kuiondoa hiyo CCM kwa kuligawa taifa hili. Hatuwezi kupata madaraka kwa kuleta uzanzibar na Utanganyika. Lisu leo umeniudhi mno.
Hotuba yako huko Zanzibar haijanivutia kwa sehemu kubwa. Imenifanya nikuone hauna nia njema na taifa hili.
Nilitegemea ungeongea kwa namna nyingine kabisa. Hasa kuhamasisha umoja, ikiwezekana useme kuwa; ingefaa taifa hili lisiwe na marais wawili. Rais awe mmoja ili kuondoa ile dhana ya upande mmoja kuonewa. Hii ni kusema kuwa, kuwe na serikali moja badala ya serikali mbili. Rais awe mmoja tu badala ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kisha Rais wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar.
Kung'ang'ania Zanzibar ni nchi hakuna la maana zaidi ya uchu wa madaraka kwa baadhi ya viongozi wetu. Zanzibar ni ndugu zetu, ni sehemu ya nchi yetu. Hata kama historia inaweza kutugawa lakini haizuii sisi kuwa nchi moja. Nafikiri Tundu Lisu hukupaswa kutoa maneno yanayoleta utengano baina ya nchi yetu kwa kuwafanya Watu waishio Zanzibar kujiona wanaonewa, ilhali hawaonewi.
Kugusa Muungano na kuuvunja, ni kuifisha nguvu Zanzibar. Ni kuwaonea ndugu zetu wa Zanzibar.
Ifike mahala tuijadili Zanzibar kama sehemu ya nchi yetu na wala sio nchi huru. Zanzibar ichukuliwe kama sehemu ya Mkoa wa Tanzania na kufuta serikali mbili ili iwe serikali moja. Najua itakuwa ngumu lakini itasaidia kupunguza migogoro ndani ya nchi.
Nafasi pekee niliyoiona ya Zanzibar kubaki salama ni kipindi kile cha mchakato wa kuchukua Fomu ya kuwania Urais NEC ambapo nilishauri Tundu Lisu aenguliwe, kwa makusudi ya kutokumpa nguvu Maalimu Seif. Nilisema pia kuwa, najua haitakuwa halali na sio haki lakini yote ni kulinda umoja wa nchi hii.
Tundu Lissu Leo umezingua mno. Huku najua hautashinda lakini macho yangu yanauona mchango wako katika ushindi wa Maalimu Seif kuichukua Zanzibar.
Zingatia; Taikon atazingatia zaidi maslahi ya nchi siku zote, kwa maana ndipo anapopata chakula, mke, watoto, na kila kitu. Taikon hata nyamaza pale anapoona maslahi ya nchi yanaathiriwa kwani kwa kunyamaza kwake ni kuruhusu Athari hizo zimfikie.
Acha Nipumzike sasa. Leo sitaki maswali, kama hujaelewa pumzika kama mimi.
Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300