SEHEMU YA NNE
Kwenye Bus kama kawaida ya Watanzania tulianza kufahamiana na kupiga story za hapa na pale. Wengi wetu ilikuwa ni mara etu ya kwanza kwenda South isipokuwa jamaa mmoja alituambia anaitwa Ahamad yeye ndo ilikuwa kama mara yake ya Tatu kwenda huko na Kuna Dada aliitwa Matlida, ni mtu wa Mbeya ila yeye ilikuwa anaishi South Miaka Mingi. Hata kwenye hii Safari yeye bus alikuja kupandia Mbeya.
Tulifika Boda ya kwanza Tunduma Majira ya saa Sita Usiku. Kulikuwa na Baridi sana. Ukweli Wakuu nitaahadithia kila kitu kama kilivyotokea. Tulivyoshuka pale Tunduma tulipokelewa na Vishoka wengi sana waliokuwa wanakimbilia Abiria ili kuwapa Msaada kwenye zile Ofisi za Uhamiaji. Vishoka walikuwa wengi sana tena walikuwa wanajiamini sana na kuingia mpaka ndani ya Ofisi za Uhamiaji.
Ukweli nilishangaa sababu nilishawai kufika Boda ya HoroHoro kwa Upande wa Tanga, Nilishawai kufika Boda ya Sirari kule Tarime, Boda ya Namanga Arusha pia naifahamu lakini sikuwai kuona Vishoka wanaingia mpaka ndani ya Ofisi za Uhamiaji kama vile unaweza kudhani wao ni Maafisa Uhamiaji.
Niligonga Mhuri wa EXIT kwenye Passport yangu upande wa Tanzania kisha nilikwenda kugonga upande wa Nakonde Zambia. Nakumbuka nilivyofika kwenye ile Kaunta ya yule Dada wa Uhamiaji Upande wa Zambia alinikatalia kugonga muhuri kwa madai kwamba nimuoneshe kama Nina Balance ya Pesa ya kutosha ya kuweza kuishi South Africa. Alisema hayo ndo Matakwa ya Sheria. Kwa wakati ule sikujua kama alichosema ni kweli ama La. Nilimwambia yule Dada kuwa Pesa ninazo kwenye Account ila alikataa, alihoji nina uhakika gani kama kweli kwenye Account una Pesa? Niliwaza labda nilipaswa kutembea na Bank Statement lakini ndo ivo nimeshachelewa.
Yule Dada alivyokataa kunigongea nikasogea pembeni ya ule mstari kupisha wengine waendelee. Nikaona Vishoka kama watatu hivi wananifuata kuniuliza nini Tatizo, Nikawaeleza kuwa yule Dada amekataa kunigongea mhuri. Mmoja ya wale Vishoka nakumbuka akaniambia kazi ndogo sana hiyo, akaingiza mkono wake mfukoni akanipa Kwacha 50 pesa ya Zambia. Akaniambia chukua hii pesa mdogo wangu weka katikati ya Passport yako kama Rushwa halafu rudi tena kwa yule Dada. Nikafanya kama alivyoniambia.