NILIVYOMKOMESHA TAPELI WA VIWANJA KIVULE
Sehemu ya 2
KASHESHE LILIPOANZA
Baada ya kama miezi 6 nikaanza na utaratibu wa kumtafuta fundi wa kuweza kufanya zoezi la ujenzi na kupitia yule jamaa yangu ambaye ni mwenyeji wangu kule tukashauriana tumpate mjenzi kutoka eneo la karibu na ujenzi na tukampata mzee mmoja ajulikanaye kama mzee Ndevu (alikuwa mwema sana kwangu)na akanipa gharama na mahitaji ya ujenzi na kazi ikaanza
Ilipofika siku ya tano toka ujenzi kuanza nikiwa katikati ya mji nikiwa katika mihangaiko yangu ya mtu mweusi nikapigiwa simu na namba ngeni nikaipokea na yule jamaa baada ya salamu akajitambulisha kwangu majina yake, umiliki wake wa eneo nami sikupaniki kwa yale maelezo yake na wala sikutaka kumbishia kuhusiana na umiliki wake ila kikubwa nikamuomba tukutane kwa kujuana, kujuzana zaidi na mengineyo (kiukweli upokeaji wangu wa simu na kuongea nae kiungwana kulinisaidia sana sana)
Basi yule jamaa akanielekeza anapokaa ambapo ni Kinondoni Mkwajuni na wakati huo mimi nilikuwa nimeshatoka Sharifu Shamba na kuhamia Magomeni kanisani hivyo usiku wa siku hiyo hiyo muda wa saa 2 nikaenda Mkwajuni kukutana na yule jamaa, nikakutana na yule jamaa (jina lake nimelisahau nilitamani sana nimtaje kwa jina kwani nae alinipigania sana)pale maeneo ya Katumba bar na tukazungumza kindugu sana na jamaa kwanza alikuwa ni mwanajeshi na yupo makao makuu yao kule Upanga na akanieleza mengi kuhusiana na yule Kasangu kuwa ni msumbufu sana na amekuwa na tabia ya kuuza maeneo ya watu sana tena amekuwa akilindwa na mapolisi wa kituo cha Staki shari katika uovu wake ila aliniahidi kuwa tutakuwa pamoja na kweli tulikuwa pamoja wakati wote wa sakata hili na akanishauri kwa hatua ya awali niende kufungua jalada pale Staki shari.
Siku iliyofuata nikaelekea huko na kufungua shauri na nikapewa mpelelezi mmoja aitwae Juma, huyu jamaa dah yaani wakati mimi nina moto wa kesi yeye akawa nikifika ananitoa tunaenda pale nje ya kituo ananambia mi sijanywa chai njoo tuongelee pale mgahawani yaani ikawa mimi tena ndio naumizwa zaidi na baada kama ya wiki tatu za kalenda yule jamaa akaenda likizo uko kwao Tabora na simu zikawa hazikauki mara vocha, mara huku kijijini nipush na mengine mengi na hadi wakati huo sakata langu halijapata mwanga wowote na wakati ameenda likizo faili langu likahamishiwa kwa mpelelezi mwingine mtu mzima hivi na nadhani alikuwa katika nyakati zake za mwisho ofisini (huyu alikuwa tatizo kuliko yule Juma😂).
Huyu mpelelezi mpya nae nadhani alikuwa anaitwa mzee Juma kama sijakosea dah yaani suala langu ndio likawa limelala kabisaaa yaani kama mwanzo lilikuwa linatambaa hapa likawa limesimama na hakukuwa na mwelekeo na halikuwa linaeleweka linaelekea wapi
MUNGU SI ATHUMANI
Nikiwa nimekata tamaa sijui mwelekeo wa shauri langu siku hiyo nimekaa maskani nikaona simu inaita na mpigaji alikuwa yule Marwa dah nikajisemea anataka nini huyu mtu.
Nirudi nyuma kidogo kutoka kufungua shauri hadi hii siku Marwa ananipigia ilishapita zaidi ya miezi 6 na huyu Marwa alinambia ana matatizo ya kiafya nadhani alikuwa na tatizo la moyo au presha na kliniki yake alikuwa anaenda pale Mnazi mmoja hivyo kama mara mbili tatu alikuwa ananipigia anapita Ilala tunaongea nampa nauli na kiukweli hii ilinisaidia sana katika kupata mwanga wa shauri langu
Turudi kwenye simu aliyopiga Marwa, nikaipokea na kusalimiana nae na akaniuliza niko wapi nikamjibu nipo Kariakoo, akaniambia njoo haraka sana Staki shari kwani Kasangu amekamatwa na ndugu zake wanaangaikia kumtoa hivyo nimuwahi kabla hajatolewa, kiukweli nilichukua pikipiki hadi pale njia panda ya Segerea na nikawa natembea mbiombio kuelekea Staki shari na Mungu jaalia nafika kituoni ndio yule bwana alikuwa ameshadhaminiwa na yupo nje tu ya jengo, nikamdaka mkono na kumwambia turudi kule kituoni na kama anabisha ntamjazia watu na hatoamini macho yake!
Kiupole nikiwa nimemshika mkono wale jamaa zake wakawa wanashangaa imekuwaje tena mimi sikutaka kuwaeleza lolote wao wakawa wanajiuliza tu imekuwaje ndugu yao bila kupinga anakubali kurudi kituoni?
Nilipofika nae kaunta pale askari tuliyemkuta akawa anamuuliza yule Kasangu "Juma imekuwaje tena?" Mimi sikumpa nafasi ya kuzungumza nikamueleza kuwa yule ni mtuhumiwa wangu na nimemleta pale kutokana na suala hilo ,akaniuliza je unayo file number? Nikatoa simu yangu ndogo nikamsomea RB# na akatizama katika daftari lake kujiridhisha na akaona kweli, shauri lilifunguliwa kwa "UTAPELI WA KUUZA ENEO AMBALO SIO LAKE" na akaandika maelezo pale na kunitaka niende na kufika siku inayofuata na nikafanya hivyo.
Siku iliyofuata nikafika na kuonana na mpelelezi wangu yule mzee Juma ili kujua nini kinaendelea na nikamkuta tukazungumza kidogo na nilipotaka kujua kuhusu mtuhumiwa wangu akanambia yule bwana amedhaminiwa na niende nyumbani atanijuza siku mbili tatu, kiukweli shauri hili lilinipa ujasiri sana hadi katika maisha yangu ya sasa kwani nikamjibu pale pale hivi niende nyumbani unaona inatosha sio?
Yaani nimepoteza pesa wewe unamuachia mtuhumiwa ambaye nimefungua shauri miezi na leo nimemleta wewe unanijibu simple kabisa eti kadhaminiwa, nikamwambia dhamana ni haki yake lakini tambua haki ina wajibu mimi naenda na sitakaa eti kusubiri simu yako,nadai changu na nitakuja kadri nijisikiavyo kujua kinachoendelea kuhusu hili suala
Nikatoka nikiwa nimeghadhibika sana na kesho kutwa yake nikatimba tena pale kituoni kujua huyo aliyedhaminiwa yuko wapi akanipiga kalenda ila nikampa vipande vyake tena na nikaenda tena kama mara 4 hivi hadi yule mzee Juma akawa ananikaripia na kuniona mimi msumbufu dah kiukweli sikumkawiza nikamwambia wewe umempa dhamana mtuhumiwa wangu kwa maana umejiridhisha na documents zake sasa hao wadhamini wake wako wapi?
Je, umekwenda Serikali ya mtaa huko anapokaa kuwafatilia wale wadhamini wake? Nikamwambia mtuhumiwa nimemleta mwenyewe na ninamtaka hapa na sitakaa kimya hadi nijue hatima ya haki yangu na uliweke kichwani hilo
Sasa wakati nakwenda kwenda pale kituoni sura yangu ikawa imezoeleka kwa maaskari pale kituoni maana naweza nikafika kituoni saa 1 asubuhi hadi saa 6 mchana na nikawa sasa yule mzee simpigii simu nafika tu nakaa upande wa pili wa kituo kwenye mgahawa na nikimuona ndio namfuata kumuuliza maana alikuwa mara hapokei au ananiambia ametoka nisije yuko mbali
Nikiwa nimekaa pale mgahawani siku moja kuna afande fulani akaniuliza "we jamaa hivi hadi leo jambo lako ni danadana? Komaa ndugu ujue yule Juma Kasangu anakula na baadhi ya maaskari kwani yupo mtaani na hawataweza kumkamata kama hautakomaa, kaza uzi ndugu yangu" dah kiukweli yale maneno yalinipa ujasiri sana kwani awali mawazo yangu yalikuwa yanaamini askari wote wa pale walikuwa wanalipuuzia shauri langu lakini baada ya yule afande kunambia yale maneno tena akiwa na wenzake wawili yalinipa hope sana na nikajiambia sasa ngoja nikajipange kwa mpango kazi!
Nikatoka pale bila kuonana na yule mzee Juma nikarudi zangu nyumbani na kiukweli niliumiza kichwa sana na kujiuliza sasa nafanyaje? Nakumbuka ile siku ilikuwa ni Jumamosi
Itaendelea....