Nilivyonusurika Kifo baada ya Mzee kunitimua nyumbani - 12.
Niliendelea kumtazama dogo kwa makini asije kuwa anakuja na watu ili ikiwezekana nichukue hatua katika mbio!.Baada ya kujiridhisha ya kwamba alikuwa akija yeye mwenyewe nilikaa kwa kutulia nikiendelea kumsubiria!.
Dogo "Bro jamaa kasema akupatie ngapi!"
Mimi "Sijakuelewa!"
Dogo "Jamaa ameniambia waweza taka pesa ngapi kwa ile exchange!?"
Mimi "Kwani jamaa huwa anabadili kiasi gani kwa kila Tsh 10,000!"
Dogo "Sikia bro kwanini nisikupeleke kwa huyo mjamaa ukaelewane nae!"
Mimi "Jamaa anafanyia kazi zake wapi?"
Dogo "Yuko tu hapo ng'ambo na hata siyo mbali!"
Mimi "Hakuna wanoko?"
Dogo "Ati unasema aje!?"
Mimi "Hakuna tatizo nikienda kwake?"
Dogo "Wala hakuna problem yeyote,jamaa yuko fiti tu!"
Sasa baada ya mazungumzo na yule dogo kumbe alimuachia huyo jamaa ile hela na jamaa akawa amemwambia aje aniulize ili kujua kwenye ile laki mimi angenipatia kiasi gani, basi kiukweli niliogopa sana na nikaona uenda ulikuwa ni mchongo wa mimi kudakishwa!
Lakini nilipompeleleza yule dogo sana akaniambia jamaa anauza vifaa vya magari, hivyo pia huwa anabadilishaga na hela!.Basi ili kuonekana sikuwa na wasiwasi nikamwambia dogo tuelekee kwa yule jamaa!.Tulitembea kwa takribani dakika 4 tukawa tumefika kwa yule jamaa ambaye alikuwa na duka la spare za magari!.
Kiukweli niliamua kujiamini na niliamua kuiweka hofu kando,sasa yule jamaa alikuwa ni mkenya ambaye alionekana kiswahili kukifahamu vizuri japo kuna muda pia alikuwa akichapia!.
Jamaa "Mambo vipi bro"
Mimi "Poa kabisa"
Jamaa "Ni wewe ndiye umemwagiza Mkamilifu?"
Mimi "Yes ni mimi!"
Jamaa "Oooh hapo iko poa,maana hata sikumuelewa"
Aliendelea "Ulitaka sasa bro nikupee pesa ngapi?"
Mimi "Wewe huwa unabadili kiasi gani kwa kila Tsh 10,000?"
Jamaa "Mimi bro nitakupea Ksh 3500!"
Mimi "Ok sawa haina tatizo"
Basi kimoyo moyo nilikuwa namshukuru Mungu sana kukutana na yule jamaa maana kiukweli kama angekuwa mjuaji pale nisingechomoka!.Jamaa aliingia dukani akawa amenipa Ksh 3500 ambapo na mimi nilimpatia yule dogo Ksh 500.Sasa jamaa akaniambia kama nilikuwa ninapesa nyingine nimpelekee maana baada ya siku mbili alikuwa anatoka! sasa yeye alichoamini ni kwamba kupitia hela ile angejipatia faida mara dufu,kuna muda nilikuwa naona kabisa natenda dhambi lakini sikuwa na namna kwasababu mimi nilichotaka ni pesa tu!.
Jamaa "Bro kama uko na pesa ingine waweza tu niletea nikubadilishie!"
Kimoyo moyo nikasema "wewe humjui umughaka vizuri,ngoja nikuonyeshe mimi ni nani".Basi nilimwambia ningerudi jioni kuleta hela kiasi fulani anichenjie.Basi tuliondoka na dogo huku tukiendelea kupiga stori za hapa na pale,nilimwambia dogo anionyeshe maduka ya nguo ili ninunue sweta nivae maana kwa kipindi kile kulikuwa na baridi ya kiaina hapo Migori!.Baada ya kununua sweta mimi nilirudi lodge na dogo akaelekea kuendelea na mishe zake!.
Sasa ilipofika mida ya saa 12 jioni sikumuoma dogo nikajua uenda atakuwa ametingwa na majukumu,basi nikachomoa tena mle kwenye begi shilingi laki moja nikaelekea kwa yule jamaa.Nilipofika jamaa alinipatia Ksh 3500 kama kawaida na kiukweli alikuwa akinishangaa sana na alitaka kufahamu kwa Tanzania nilikuwa natokea maeneo gani,mimi nilimdanganya ni mwenyeji wa Mwanza!.
Kama nilivyosema hapo awali ya kwamba, baada ya kujishughulisha na hiyo shughuli haramu hata muonekano wangu ulibadilika sana na ulikuwa ukiniangalia huwezi amini kama mimi ni mpiga debe pale Sirari!
Sasa baada ya jamaa kunipatia ile hela nililipa pale lodge pesa ya siku mbili nikawa nimebaki na pesa kadhaa!.Nilitaka nikae pale Migori ndani ya siku 3 halafu nigeuke zangu Sirari ili nikaone kama mambo yalikuwa yamepoa!. Niliamini ya kwamba kama jamaa angetoka akaenda kubadili zile hela halafu wakamshitukia basi najua angemtafuta dogo Joe akawaleta pale Lodge nikapata kashikashi, hivyo nilipanga nichomoke mapema kabisa!.
Sasa kabla ya kuondoka nilinunua begi dogo la mgongoni kisha nikanunua na suruali ya jeans moja nikawa nimebadilisha,zile hela niliziweka kwenye lile begi la mgongoni pamoja na ile shati niliyokuwa nimevaa siku naingia hapo Migori,ile sweta na jeans nikavaa nikawa sasa na muonekano mpya!
Sasa siku naondoka nilienda kuonana na yule dogo Joe pale stendi nikamkabidhi lile begi nikampatia na hela kiasi cha elfu 50 ya Tanzania,sasa ilikuwa ni juu yake kuzibadili ili aionjoi maisha,kama walidamka basi ni yeye na mungu wake!.
Nilipanda zangu shuttle za Isebania nikageuka zangu.Nilipofika pale Isebania nilishuka nikaingia zangu kitaani kupita njia isiyokuwa rasmi kuingia Sirari,ile njia walikuwa wakiipita watembea kwa miguu hivyo hakukuwa na bugudha toka kwa mamlaka zote mbili!.Ilijulikana ya kwamba watu wa Kenya wanapita kuingia Tanzania na watanzania walikuwa wanaingia Kenya kununua bidhaa na mahitaji.Sasa nilipofika hapo Sirari,sikutaka kabisa kwenda moja kwa moja nyumbani,nilianzia kwanza kijiweni!
Nilipofika pale niliwakuta wadau wangu wakiwa wanaendelea na kazi huku wengine wakishangaa na kuniuliza ndani ya siku mbili tatu hizo nilikuwa wapi!.Mshikaji wangu Nyamori sikumuona hapo kijiweni hivyo nikaelekea dukani kwa yule mama kununua vocha ili nimpigie simu.
Nilimpigia simu yake ikawa inaita tu bila kupokelewa,basi nilipoona haipokelewi nikaamua kuachana nae,sasa ikabidi nimpigie Gabriel,nilipoipiga namba yake ikawa haipatikani!,nikarudia tena lakini haikupatikana!.Sasa sikutaka kumtafuta kabisa yule mwanamke wake kwasababu nilikuwa nakifahamu kichwa chake kilivyokuwa kibovu!
Nia ya mimi kumtafuta Gabriel nilitaka kujiridhisha kama yuko hewani ili anieleze kilitokea nini siku ile,sasa nilipomkosa niliamua kupiga kimya!. Sasa wakati nikiwa naendelea kutafakari, kuna mshikaji alikuwa mdau hapo kijiweni nae alikuwa mpiga debe, huyu alikuwa akiitwa Magesa! Sasa jamaa akawa ananiambia kuna jamaa toka juzi alikuwa akinitafuta hapo kijiweni na hata asubuhi ametoka hapo kuniulizia!.
Mimi "Jamaa yukoje?"
Magesa "Ni jamaa mmoja hivi tolu halafu blaki!"
Mimi "Alikuwa anasemaje?"
Magesa "Aisee hata sijui maana juzi ameshinda hapa na hata leo pia amekuja lakini hakukaa!"
Mimi "Alikuwa na gari?'
Magesa " Sijajua kama ana gari maana hapa hakuja na gari"
Baada ya Magesa kuniambia vile kiukweli moyo wangu ulilipuka tena kwa hofu,kwa namna alivyozitaja sifa chache za huyo mtu nilijiridhisha kabisa ya kwamba hakuwa Gabriel.Sasa baada ya muda kidogo nikiwa pale kijiweni simu yangu ikawa inaita,kuangalia nikakuta ni Nyamori alikuwa akinipigia.
Nyamori "Mwanangu ulikuwa wapi?,mbona simu yako ilikuwa haipatikani!"
Mimi "Mwanangu nilienda hapo Migori mara moja"
Mimi " Nipo hapa kijiweni lakini sikuoni!"
Nyamori "Mi nilitoka niko Nyamongo tangu jana,kuna mzee tumemletea ng'ombe hivyo nitarudi jioni au kesho asubuhi"
Aliendelea "Sasa sikia,kuna jamaa mmoja ni askari namjua,toka juzi anakusarandia hapo kijiweni Mwanangu"
Basi baada ya jamaa kuniambia vile sikutaka kabisa kupoteza muda pale kijiweni nikawa nimeondoka,sasa ndipo nikaunganisha na yale maelezo ya magesa nikaona kumbe bado kulikuwa na msako unaoendelea kimya kimya!..
Nyamori " Mwanangu kwani kuna ishu gani?
Mimi "Mwanangu bado ni ile ishu ya deni!".
Nyamori "Kwanini usimwambie mshikaji uwe unamlipa kidogo kidogo mpaka umalize ili aache kukusumbua!"
Mimi "Nitajua cha kufanya Mwanangu!"
Yeye hakufahamu kwamba ni lile dili haramu ndilo lilikuwa likiniangaisha,alichofahamu na nilichomwambia ni kwamba nilikuwa ninadaiwa!.
Basi nikaondoka zangu nikawa natembea haraka uelekeo wa Tarime ili nikapande gari nielekee Tarime mjini,sasa sikutaka kunyooka na lami,nilipita pembezoni mwa barabara ili nikifika mbele nidandie gari mpaka Tarime!.Wazo la kurudi tena pale geto kwangu sikuwa nalo kabisa na niliamua kama ni vitu ngoja viozee ndani lakini si kwenda kujikamatisha!.
Sasa namshukuru Mungu nilifika Tarime na niliamua kupita njia nilizokuwa nazifahamu kuelekea nyumbani kwetu ambako Mzee miezi michache iliyopita alikuwa amenitimua!
Nilipofika hapo nyumbani nilimkuta binti ambaye nilikuwa simfahamu na nilipomuuliza wenyeji wameenda wapi akawa ameniambia Mzee hajui alipo kwenda ila mama yangu alikuwa ameenda sokoni na dogo Amos yeye alikuwa shule! sasa niliondoka mdogo mdogo kuelekea sokoni ambako mama yangu alikuwa akifanyia biashara zake!
Muendelezo >
Sehemu ya 13