Niliweka shada za maua kwenye makaburi matano ya watu wangu wa karibu - 05
Niliita Zai! Zai! Lakini hakunisikia wala hakunijali, aliendelea kubamiza mlango akiropoka na kunguruma. Niliogopa hata kumsogelea maana nilihisi angenivamia na kunijeruhi hivyo nikawa namtazama kwa mbali, namtazama huku nikipaza sauti kama itasaidia.
Kidogo nikapatwa na ufahamu, ufahamu wa kupiga simu kuomba msaada wa nini cha kufanya katika janga lile. Nliperuzi katika simu yangu nikaibuka na namba ya mama mmoja hivi ambaye alikuwa ni jirani yangu kule nilipokuwa ninaishi kabla ya kuhamia kwangu, mama huyo tulizoea kumwita Mama Miraji, alikuwa mama mwenye kushika dini sana, masaa ishirini na manne amejisitiri, hakosi ibada, swala tano kama chakula.
Nikamweleza mama huyo shida yangu naye akaniambia yuko mbali lakini ningoje aone kipi cha kufanya. Basi baada ya muda mdogo, mama huyo akanipa maelekezo, alinitaka niweke 'loudspeaker' simu yangu kisha niwe karibu na mhanga wangu, nikafanya hivyo, mara mama yule akaanza kuongea kwa lugha ya kiarabu, lugha nisiyoielewa, aliyasema na kuyasema mambo ambayo kwangu yalikuwa mageni, aliyatamka kana kwamba anayasoma mahali, kidogo kama utani, nikaanza kumwona Zai analegea na kulegea.
Hapo nikapata nguvu ya kumsogelea. Nilimsogelea nikiwa namwelekezea simu yangu kana kwamba simu ile ni silaha, si punde Zai akaanguka chini na kuwa kimya, kimya kama amekufa, nikaogopa tena!
Haraka nilimsogelea nikamtikisa, simu nimeiweka kando, bado inaendelea kusema maneno nisoyaelewa, nikamwita Zai, Zai, kimya. Ila alikuwa anahema, hilo angalau likanipa nguvu.
Baadae, kama baada ya robo saa hivi, Amiri alirejea nyumbani. Nilisikia mtu akisemezana na ng'ombe huko nje, kutoka nikamwona kijana huyo akiwa anawaswaga ng'ombe kwenda zizini, upesi nikamwita, naye upesi akaja.
Nilimuuliza alikuwa wapi namtafuta kiasi hiko? Kabla hajajibu nikamtaka aingie ndani haraka kunisaidia, akafanya hivyo mpaka kwenye mwili wa Zai, alimnyanyua mwanamke huyo kama ubua akamweka kwenye kochi. Kweli nilistaajabu. Sikutegemea kijana yule kama angeweza kumnyanyua Zai namna ile. Kama ungewahi kumwona Amiri nadhani ungenielewa kwanini nilistaajabu kiasi hicho. Mwili wake ulionekana goigoi kinyume kabisa na matendo yake.
Baada ya kumweka Zai kwenye kochi, aliniaga akafungie ng'ombe, basi akaondoka akiniacha mimi namtazama Zai. Si muda, Zai akaamka akiwa analalamika kichwa kinamuuma.
Aliponyanyua mkono wake kujishika kichwa akahisi pia maumivu. Alitazama mikono yake akaiona mekundu kwa kuvilia damu, inamwaka moto, akabubujisha machozi kama mito, tayari alishajua nini kilitokea.
Alinambia, "nimechoka hii hali! Nitaishi hivi mpaka lini?" Kweli nikamwonea huruma sana. Alinambia namna gani hali ile inavyomtesa, haikuwa habari mpya kwangu maana nilikuwa nafahamu, lakini siku ile nilihisi kila alichonieleza ni kipya, pengine sababu nilimshuhudia kwa macho yangu na si kuhadithiwa kama hapo awali.
Alilalamika, "kila mwanaume ninayepata, akishajua nina mambo haya basi ananikimbia. Nitakuja kuishi na nani mimi?"
Nilimpa pole nikamshauri tuonane na yule mama Miraji kwani kwa yale aliyoyafanya siku ile kwa simu pekee niliamini angeweza kutusaidia kukabili lile janga, hata kama hatoweza basi anaweza kutushauri pa kwenda au kipi cha kufanya.
Haikupita muda, Zai aliaga akaenda zake. Niliona hiyo ni kheri maana hakuonekana na raha tena pale. Nilijaribu kumwongelesha na kumfurahisha lakini sikufua dafu. Alipopotea, hata nami nikapata afueni. Nilijumuika na Amiri kutazama mifugo, huko tukaongea mambo machache.
Kwasababu Amiri hakuwa mtu wa kuongea sana, ni mimi ndo' nilikuwa namchokonoa kwa maswali ya hapa na pale. Kitu peke ambacho Amiri alikianzisha katika maongezi lilikuwa ni swali moja tu, aliniuliza;
"Yule ni rafiki yako?" Akimaanisha Zai, nikamjibu ndio, naye hakuongeza tena neno. Alikaa kimya mpaka mimi nilipoondoka, nilimwona akinitazama nikienda zangu mpaka kuudaka mlango na kuzama ndani.
Baada ya tukio hilo la Zai, zilipita kama siku mbili hivi bila kumwona mume wangu, kama kawaida akisema ni majukumu mapya ya kazi. Siku ya tatu, alirejea nyumbani na mimi siku hiyo nikaazimia kuendelea na zoezi langu la kukagua simu yake.
Lakini simu hiyo nilipoishika, katu sikufanikiwa, nilikuta amebadili nywila za kufungulia simu yake akiweka mpya ambazo mimi sizifahamu. Nilijaribu kila nilichowaza lakini wapi! Mwishowe nikaachana nayo nikiwaza kwanini bwana yule ameamua kufanya mabadiliko yale.
Ina maana amenishtukia au?
Au alipata kuongea na yule mwanamke kuhusu simu niliyopiga siku ile? Simu ile ambayo sikusema kitu hivyo mwishowe akagutuka? Sikupata majibu sahihi lakini niliamini mawazo yangu, bwana yule atakuwa ameshtuka.
Kesho yake majira ya mchana nikiwa kazini, nilimpigia simu mama mkwe wangu, lengo kujua atapokea nani na kama ninaweza pata chochote kwake kuhusu yanayoendelea, simu ikaita pasipo kupokelewa, kimya.
Nilijaribu kupiga tena lakini napo sikuambulia kitu, simu ilikuwa inaita mpaka kukata kwake, basi nikaachana nayo niendelee na mambo mengine, baadae majira ya jioni, nikajaribu tena, simu ikaita na mara hii ikapokelewa na sauti ya mwanamke, si sauti ya mama mkwe wangu lakini pia sio ngeni masikioni mwangu, sikuwaza sana nikaikumbuka sauti hiyo barabara, nilikuwa sahihi, ilikuwa ni sauti ya mwanamke wa siku ile, mwanamke aliyemwita bwana Mgaya mume wangu!
Mwanamke huyo alinisalimu kisha akasema mwenye simu hayupo, nikamuuliza kaenda wapi, akakaa kimya kidogo, nikarudia swali kaenda wapi? Akanijibu anaumwa yu hospitali, hawezi kutumia simu majira hayo.
Nikamuuliza, "wewe ni nani yake mama?" Hakujibu, kama kawaida nikarudia tena swali, nikalirudia kwa mkazo, akanijibu yeye ni mwangalizi wa mama wakati huu akiwa anaumwa.
Mwangalizi? Nikagunia kifuani.
Mwangalizi kama nani yani? ... Kabla sijatema kauli, akawa amekata simu. Tangu hapo nilipiga kadiri ya nilivyoweza, hakupokea tena, zaidi nilipoongeza usumbufu akani-block kabisa. Niligundua hilo maana nilipojaribu kupiga simu hazikuwa zinatoka tena, wala ujumbe haukuwa unafika.
Sasa nikaona nitulie. Nitulie nione huu mchezo unapoelekea.
Keshokutwa yake, bwana mkubwa alirejea nyumbani na kitu cha kwanza kunambia punde tu baada ya kupeana salamu ilikuwa ni hali ya mama yake. Aliniambia mama yake anaumwa, hali yake si nzuri, na vile tuongeapo, yuko hospitalini anauguzwa.
Moja kwa moja nikajua maongezi yale ni sababu ya mazungumzo nilofanya siku ile na yule mwanamke kwani mama mkwe hakuanza kuumwa siku hiyo, kwa namna nilivyoongea na mwanamke yule siku ile tayari yule mama alishatumia siku kadhaa hospitali, sasa mbona Mgaya hakuniambia?
Nilijikuta natabasamu nikimskiza Mgaya. Muda mwingine kuna raha yake mtu kukuona zuzu huku wewe unamsanifu, lakini Mgaya alihisi kabisa kuna jambo lipo kombo, kila alichosema mimi nilimkubalia na wala sikuuliza swali, mwishowe akaniuliza; "uko sawa kweli?"
Mimi nikamjibu niko sawa, hamna shaka, basi maisha yakaendelea, kichwani mwangu nikipanga vyangu na namna ya kufanya. Ilipofika mwisho wa juma, pasipo kumwambia mtu yeyote, nlijiandaa nikafunga safari kwenda Iringa, nyumbani kwa wakina Mgaya, huko ndo' nikaenda kujua mbivu na mbichi ...
Kumbe Mgaya alikuwa ameoa kimila, na mwanamke yupo huko kwao, kwenye 'kamji' kake ndani ya kaya yao, ndugu zake wote wanafahamu kinachoendelea na wanamtambua mwanamke huyo kama mke wa Mgaya!
Walishtuka kuniona nimefika hapo, na si muda mrefu Mgaya akawa amearifiwa kuhusu ujio wangu wa kushtukiza. Alipiga simu mno lakini hamna hata moja nilopokea, mwishowe nikazima simu kukwepa usumbufu.
Nilichokuja kubaini kule Iringa ni kwamba, mama yake na Mgaya, yaani mama mkwe wangu, ndiye alimshinikiza Mgaya kuwa na mwanamke mwingine wa kibena ambaye atakuwa anamtazama na kumuagua pale nyumbani.
Sawa, nalifahamu mwanamke yule hakuwa ananipenda, hata mimi sikuwa nampenda vilevile, lakini kile alichonifanyia kilivuka mipaka. Niliona amenikosea mno mno, na ajabu ni kwamba hakuonekana kujutia nalo, zaidi nilipomwona kule hospitali aliniuliza akinikenulia meno yake, umemwona mke mwenzio?
Nilitamani nimkabie hapo kitandani mpaka afe!
Baadae nilikuja kupata taarifa kuwa mume wangu yuko njiani anakuja akitokea Dar, maneno hayo niliyasikia toka kwa shemeji zangu walokuwa wakiishi hapo, nami sikutaka kuonana naye, nikafanya upesi kupanda zangu basi kurejea huko yeye alipotoka, hivyo tukapishana njiani.
Simu yake sikupokea, wala ujumbe wake sikuujibu.
Sasa nieleze, mtu huyu hakustahili kifo? Sijui kwako, lakini kwangu alistahili mno mno. Si yeye tu, pia na mama yake. Kama waliyajua haya, kwanini walikubali nikaolewa katika familia yao na desturi ile ya kipuuzi? Kwanini wasingemtafutia mtoto wao mwanamke wa huko kwao yote yakaisha?
Niliongea mwenyewe njia nzima. Nang'ata meno na kufuta machozi yanayonilenga. Naumwa na uchungu lakini nikimtazama mwanangu napambana kutabasamu, nilikuwa nafanya hivyo mpaka kufika Dar. Safari ndefu ya kuchosha. Safari ambayo mume wangu alikuwa akiifanya alipokuwa akipotea juma zima kule nyumbani.
Kuja kumwona mkewe mwingine.
Basi nilifika nyumbani nikashinda siku mbili, siku ya tatu yake majira ya usiku namwona mume wangu akiingia ndani pamoja na mama yake mzazi. Mama huyo anatembea kwa kuchechemea. Amevalia gauni na kujitanda khanga.
Bwana Mgaya akaniambia, "mke wangu, najua kuna mambo mengi yalitokea hapa katikati. Usijali, nitakueleza kila kitu pasipo kuficha. Nimeona ni stara nikamleta mama hapa nyumbani tukamuuguza, kwanza naomba tumpokee alafu yetu binafsi tutayaongea na kuyamaliza."
Mgaya ....
Maskini Mgaya,
Hakujua alikuwa amemleta mama yake kwenye kifo. Hakufahamu kuwa pale mama hakuja kuuguzwa bali alikuja kuuawa.
Mama yule hakuliona jua mara tatu katika nyumba ile, tukatangaza msiba. Yeye akiwa ndo' mtu aliyefungua dimba la umauti pale nyumbani....
***