Niliweka shada za maua kwenye makaburi matano ya watu wangu wa karibu


Kuna vitu nimesoma huku Nacheka sana hii episode!!

Anyways Ngoja nisubirie episode inayofuata!!
 
Sehemu ya Tatu:



Baada ya miezi kadhaa kupita, mama mkwe alirejea nyumbani kwake akatuacha mimi na mume wangu tukiwa huru kama hapo awali.

Siku ya kuondoka kwake ilikuwa ni furaha kweli kwangu, nilitamani hata nifanye sherehe nialike watu wakala na kunywa kwani nilihisi nimetoka kifungoni. Kifungo huru. Nikawaza sasa, hata mwili wangu utarejea maana nilikuwa nimekongoroka kweli.

Kuyabeba mambo kifuani huku ukiwa unaigiza uko sawa mbele za watu yataka moyo wa jiwe kwelikweli.

Nakumbuka mume wangu alikuwa ananiuliza kunani, mbona unapukutika? Hauli? Unaumwa? Akawa ananisihi sana niende hospitali, hata siku moja akataka kunilazimisha nipande kwenye gari niende naye hospitali lakini nikakataa kata, hakujua naumwa ugonjwa wa 'mama yake'. Hakujua sikuwa na raha kabisa na nyumbani kwangu.

Kweli mwezi tu kupita toka mama yule alipoondoka, nuru ikanijia usoni na mwilini. Nilimlelea mwanangu vema mpaka pale likizo yangu ya uzazi ilipokwisha, nilipewa likizo ya mwaka mmoja tu kutoka kazini, hivyo nikaripoti kwa meneja. Nilimpigia tu simu kumpasha habari ya kwamba natambua muda wangu wa kurejea kazini umewadia na nitafanya hivyo punde. Nilifanya hivyo kwasababu sikutaka kabisa kupoteza kile kibarua changu, maslahi yake hayakuwa haba ukilinganisha na kule nilipotoka mwanzoni.

Nakumbuka meneja yule, bwana Salum, aliniuliza: "Magreth, kila kitu kipo sawa?" Kisha akaniambia, "take your time, you don't need to rush. Utakapoona you are totally ready, fika kazini."

Bwana huyo alikuwa na kawaida ya kuongea sana kiingereza, asingeweza kumaliza sentesi moja kamilifu pasipo kutia maneno kadhaa ya ughaibuni, ujana wake wote alipata kuishi huko nje ya nchi, Uingereza, hivyo aliathirika sana na mazingira yale.

Lakini zaidi ya hilo, hata tabia za bwana Salum hazikuwa za mtu wa kiswahili, usingemkuta akipiga majungu, kukimbia majukumu yake, kulaumu waliochini yake kwa kila jambo wala kusikiza mambomambo ya kuambiwa na wafanyakazi wake, haswa mambo ya umbea umbea.

Alikuwa mtu 'panctual' sana na mtu wa kutuhamasisha kazi kazi, ila udhaifu wake mkubwa ulikuwa ni mmoja ... usijali, utaona kwa macho yako mwenyewe hapo mbeleni.

Basi kwa kauli ile ya meneja na hivi sikuwa na sikutaka kuwa na msichana wa kazi katika malezi ya mwanangu, nikaendelea kukaa nyumbani kufanya malezi huku mshahara wangu ukiingia kama kawaida.

Mara kadha wa kadha, rafiki yangu, Zai, naye alipokuwa akipata muda alikuwa anakuja nyumbani kwangu na kuutumia muda wake kunisaidia shughuli za hapa na pale. Kuja kwake kukawa kunanipa 'kampani' kubwa sana na kuniondolea upweke wa pale nyumbani.

Angeniambia mambo haya na yale, angenisimulia ya kule shuleni nilipotoka maana nilikuwa nimemwacha bado akifundisha huko, angenieleza mizaha yake tukacheka, angeniambia pia mambo 'serious' tukajadili, lakini zaidi angenieleza habari za Anwari.

Wapi alipomwona bwana huyo, kipi alichokuwa akifanya na nani alikuwa naye. Angeniambia kila kitu anachokijua, na mwishowe angeniuliza; haumkumbuki bwana yule? Na mimi ningekataa abadani.

Ningebisha kadiri ninavyoweza, ningeapa kila kiapo kuwa bwana yule hakuwa akilini mwangu, lakini Zai angeutambua ukweli kwenye mboni za macho yangu. Angetambua ya kwamba naongopa.

Hakuwa anasema kitu bali kuguna tu, na mwisho wa habari hizo, angeniaga akaenda zake. Akiondoka ananiacha mpweke, mimi pamoja na mwanangu mdogo mpaka majira ya usiku au kesho yake kabisa ndo' nipate kuonana na mume wangu, bwana Mgaya.

Basi kama ujuavyo, muda huwa haugandi, siku zilikimbia kusonga mbele na mume wangu akaanza taratibu kutimiza mpango wake wa kufuga kwa kujenga mabanda madogo madogo, mabanda yatakayohifadhi kuku na bata.

Mabanda hayo yalipokamilika, waliletwa kuku kadhaa wa kienyeji na bata wachache. Kwasababu mimi nilikuwepo pale nyumbani na mifugo ile haikuwa ya kisasa, nikaimudu kuitazama vizuri tu, kitu ambacho mume wangu alikifurahia sana.

Alikuwa akinambia mara kwa mara, katika uzee wetu, mimi na yeye tutakuwa tunakaa nyumbani shughuli yetu kubwa kutazama mifugo inayotuzunguka. Hatutakosa mayai, nyama wala maziwa.

Nasikitika ndoto zake hizo hazikupata kutimia kamwe. Aliongozana nazo kaburini, mwili wake na mawazo yake, vyote kwa pamoja, vikafukiwa na kifusi kizito. Kifusi ambacho juu yake mimi nilipata kusimama nikiweka shada la maua.

Shada lililoandikwa kwa herufi kubwa ... 'MKE'.

Nisamehe sana Mgaya. Kile kilio nilichokuwa nakitoa pale msibani hakikuwa na kweli yoyote bali unafiki tu. Nililia usoni mwangu huku moyoni nikikung'ong'a na kukusonta.

Niliona unastahili kifo kile. Niliamini ilikuwa ni adhabu tosha kwa yale yote uliyoyatenda na kunitendea, lakini kuyaeleza mambo hayo kwa sasa si vema. Ni kheri kushuhudia kuliko kusikia. Basi niyaachie hapa na wewe utakapoyaona hayo, utanihukumu utakavyo.

Lakini nihukumu kama wewe ni msafi kuliko mimi unayeninyooshea kidole.

Basi likizo ile ya uzazi toka shuleni ilidumu kwa miaka miwili. Muda wote huo nilipata wasaa wa kukaa na kumlea mwanangu lakini kutazama mifugo ambayo mume wangu aliianzisha, yaani kuku na bata.

Mpaka kufikia muda huo, yaani mimi kurejea kazini, mifugo ilikuwa imeongezeka sana, na kama haitoshi mume wangu aliongeza banda jingine ambalo alisema ni mahususi kwaajili ya ufugaji wa ng'ombe wa kisasa kwaajili ya maziwa.

Na kwasabababu ratiba zangu za kazini hazikuwa zinanibana sana, nilikuwa naenda shule na kurejea mapema nyumbani maana nilikuwa nafundisha madarasa ya chini, niliendelea kutunza mifugo vizuri, nikihakikisha nawaachia chakula cha kutosha asubuhi kisha naja kuwamalizia ninaporudi.

Mtoto wangu nilimwanzisha 'baby class' palepale nilipokuwa nafundisha, achilia mbali alikuwa anasoma bure maana ni mtoto wa 'staff' wa pale shuleni lakini pia nilifanikiwa kujipunguzia majukumu lukuki kwani niliweza kufanya kazi na kulea kwa wakati mmoja.

Nakumbuka niliporejea kule kazini, meneja, bwana Salum, alinipongeza sana hata kunipa zawadi. Alinisihi nifanye kazi lakini pia nisisahau kuzingatia afya yangu, kwa kuonyeshea msisitizo kwenye hilo, alimuagiza mkuu wa shule anipunguzie majukumu na jambo hilo likafanyika japo liliibua maneno maneno kwa baadhi ya walimu wengine, haswa wa kike, wakisema ule ulikuwa upendeleo ulovuka mipaka, mbona wao hawakuwahi kufanyiwa hivyo hata walipoagua ndugu zao ama kukaa majumbani kwa likizo za kujifungua?

Mimi wala sikujali, alimradi yangu yalikuwa yanaenda basi nami nikaenda nayo, mengine niliwaachia wenyewe. Hao wenye huo muda.bBasi maisha yakasogea. Naishi vilevile kwa mujibu wa ratiba yangu.

Nakumbuka sasa, muda mfupi baada ya kurejea hapo kazini, ndo' nikaanza kukumbana na tafarani na bwana Mgaya, yaani mume wangu. Bwana yule alianza kushinda siku mbili hata tatu kazini pasipo kurejea nyumbani, kitu ambacho kwangu kilikuwa kipya kabisa.

Nilimuuliza vipi na mabadiliko hayo, akanijibu sasa kazi imembana, wameongezewa majira yao ya utendaji lakini vilevile na kiasi kidogo cha pesa katika ujira wao.

Kwa maneno yake, alikuwa akilala ndani ya gari tena kwa muda mchache tu, muda mwingi yuko macho kwenye mizunguko, na yote hayo ni sababu ya kupambania malengo ya familia yetu.

Nami sikuwa na budi kukubali, kwa maana sikutaka nionekane kikwazo kwenye mafanikio ya familia.

Lakini siku moja, bwana yule alikuja nyumbani akashinda sana ndani ya gari akiongea na simu. Alitumia kama robo saa hivi tangu alipozima gari yake kiasi kwamba nikatoka nje kuangalia usalama.

Mbona nimesikia gari linaingia lakini simwoni mtu akiingia ndani?

Niliposogelea gari nipate kujua kinachoendelea, sikuambulia kitu, bwana yule aliaga akakata simu yake, lakini baadae kwenye maongezi yetu ndo' nikabaini simu ile alikuwa anaongea na mama yake, na kweli nilithibitisha baada ya kuangalia 'call logs' wakati alipoenda kuoga akiacha simu yake mezani.

Bwana Mgaya alinambia hali ya mama yake si nzuri, sukari inamsumbua, hivyo maongezi yale yote walikuwa wanajuliana hali lakini wanapanga namna ya kufanya.

Katika namna hizo mimi nikawa naomba, tena kwa dhati, isiwe kuja kukaa pale nyumbani na mimi ati kuamgua. Hilo sikutaka hata kulisikia.

Lakini mbali na hayo,

Kuna kitu kilinambia kuna jambo bwana Mgaya ananificha. Sijui kwanini niliamini vile lakini nilihisi kabisa kutoka ndani yangu, na hisia hizi nilikuja kuzithibitisha mimi mwenyewe hapo mbeleni.

Kweli Mgaya, kaburi lile lilikuwa ni haki yako! Tena haki yako ya msingi.

Ni ndani ya mwezi huo na kuendelea, kwa ufuatiliaji wangu wa karibu, ndo' nikaona maongezi baina ya Mgaya na mama yake yamepamba moto. Kila siku aliporejea nyumbani baada ya kushinda siku mbili ama tatu, kama ilivyokuwa kawaida yake mpya, nikawa nakuta 'call logs' akiwa ameongea na mama yake kwa dakika za kutosha.

Dakika si chini ya tano kwenye kila maongezi.

Nami sikusema tena kitu kwake, nakumbuka mtu pekee niliyemgusia jambo hilo alikuwa rafiki yangu Zai. Siku hiyo alikuja nyumbani kunisalimu kama kawaida, tukaongea mambo mengi ya hapa na pale, lakini kubwa lililomleta lilikuwa ni tatizo lake sugu la kupandwa na mashetani.

Alinambia usiku wa jana yake alisumbuka sana na kusumbua majirani mpaka kuja kutulia. Anahangaika sana apate tiba lakini hamna anachoambulia, zaidi ya tatizo kutulia tu kwa muda kisha linaibuka upya.

Nilipomshirikisha lile jambo langu, Zai akanipa wazo jema. Aliniuliza kama zile namba za mama yake na Mgaya nishawahi kuzijaribu kwa kuzipiga? Nikamwambia hapana. Akaniuliza kama nishawahi kuzilinganisha na namba za mama huyo katika simu yangu kuhakikisha ndizo zenyewe? Napo nikamjibu hapana.

Akaniambia;

"Shoga 'angu acha uzembe. Mbona unakuwa mzito hivyo? Mjini hapa!"

Kweli nikajihisi uzito wa kiboko. Nikakaa kwa hamu sana kungoja siku bwana atakapokuja basi nianze oparasheni yangu yangu kabambe.

Nikangoja siku ya kwanza, hakurudi nyumbani. Kesho yake pia hakurudi nyumbani. Hata siku ilofuata, hakurejea nyumbani. Hamaki juma zima likapita sijamtia machoni! Hiyo ilikuwa ni rekodi mpya kwangu. Hakuwahi kuvukisha muda mrefu kiasi hicho.

Nilijaribu kumpigia simu baada ya siku zile tatu kupita, hakuwa anapatikana. Hata nilipoendelea kujaribu, sikufanikiwa. Nilikuja kumpata baada ya juma moja kukata, tena hapo akaniambia yuko njiani anakuja, akifika tutaongea.

Alipokuja nilistaajabu anaingia na fuso nyumbani, nyuma amepakia ng'ombe wawili. Akanieleza alikuwa amesafiri kwenda kuonana na mama yake lakini hukohuko akachukua fursa ya kuja na ng'ombe hao kwaajili ya ufugaji alonambia hapo awali.

Lakini kwanini hakuniaga? Kwanini hakunambia kama alienda huko kuonana na mama yake? Hakunieleza kitu nikaelewa.

Nilitamani nimrukie kwa maswali na jazba lakini nikaona haina faida. Nitaharibu mipango yangu. Waswahili wanasema kumchinja kobe yataka subra. Nikaona niwe mpole mpaka pale nitakapojiridhisha kinyume chake.

Lakini pamoja na hayo, hiyo siku SITAKAA NISAHAU maana ndo' siku ambayo nilikutana uso kwa uso na kijana Amiri. Kijana huyo alikuwa amekuja akiongozana na bwana Mgaya katika fuso ile.

Kijana mwembamba mweusi, chini amevalia kandambili rangi ya samawati. Nyayo zake zimepasukapasuka, shati lake limejikunjakunja na suruali yake ya kitambaa imeishia kwenye vifundo vya enka.

Mgongoni mwake amebebelea begi jeusi, haya manegi ya bei rahisi, begi hilo limeandikwa Sport.

Kwa makadirio, bwana Amiri alikuwa na miaka isiyozidi ishirini na tatu hivi, lakini alionekana mkubwa kupita miaka hiyo kwasababu ya ufukara wake, ufukara usohitaji maelezo, unaonekana bayana machoni.

Mume wangu alinitambulisha kwa kijana huyo kuwa ni 'shamba boy', ametoka naye kijijini, na amemleta hapa kwaajili ya kusimamia mifugo tu, haswa haswa ng'ombe. Kutafuta malisho yao, kukamua maziwa na hata kuyasambaza kwa wateja panapobidi.

Nikampatia kijana huyo mkono, mkono wa karibu, naye akaupokea akisema: "naitwa Amiri."

Hapo baadae nilipata shaka, kweli kijana yule alikuwa anaitwa Amiri ama shetani? Sikuuona utofauti.

Laiti nisingekutana na Amiri siku ile, huenda leo hii ninavyokisimulia haya, ningekuwa mwanamke mwenye mume na watoto, pia kama binadamu wengine ningekuwa na watu wa karibu wa kunitazama na kunipa bega pale ninapolia.

Lakini leo hii naishi kama mtawa, tena mtawa ninayenuka damu mikononi mwangu.

Hapa sasa ndipo mfululizo wa vifo ulipopata kuanzia...



**
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…