Niliweka shada za maua kwenye makaburi matano ya watu wangu wa karibu

Niliweka shada za maua kwenye makaburi matano ya watu wangu wa karibu

Sehemu ya Tisa:


Anwari aliniambia anafahamu ya kwamba nina mtoto, mtoto wa kiume, na mtoto huyo umri wake unawiana sawa na muda tulokutana mimi na yeye.

Hapo nikamgomea, si kwamba hatukukutana, lah, bali nilimwambia muda huo nilishiriki tendo pia na mume wangu, hivyo yeye ana uhakika gani kama kweli mtoto yule ni wake?

Nilimuuliza nikiwa nayajenga yangu kichwani, bwana yule hajui ninapoishi wala wapi ninapofanya kazi, alitambuaje kama nina mtoto? Alitambuaje kama nilipata mimba?

Akili yangu ikanambia ni Zai. Hamna mtu mwingine isipokuwa yeye. Zai alimwambia Anwari kuwa mimi nina mimba na akamwambia nimepata mtoto.

Zai alimwambia kila kitu isipokuwa mahali ninapoishi na mahali ninapofanya kazi. Bila shaka angefanya hivyo, tayari Anwari angelifika getini kunigongea.

Lakini kwanini Zai aliyasema yale? ... Sikukaa nikajua.

Tuliendelea kuzozana na Anwari tusipate muafaka, na kwasababu muda ulinitupa mkono, nikamwambia nataka kwenda zangu nyumbani, siku nyingine tukionana panapo majaliwa basi tutaongea.

Bwana huyo akakataa.

Alinambia haniamini maana sikawii kum-block akahangaika tena kama hapo awali, kuhangaika mpaka kumhusisha Zai.

Na mimi kwasababu sikutaka aendelee kuwasiliana na Zai kuhusiana na lile jambo letu, nikaona ni vema nimpatie Anwari uhakika wa kunipata muda wowote atakaonitafuta.

Yale alokuwa anayajua Zai yanatosha, sikutaka azidishe tena hata punje.

Basi nikamwambia namba yangu nilompigia ndo' hiyohiyo itakayokuwa hewani milele. Akinihitaji anitafute aidha kwa kupiga ama kutume ujumbe, lakini nilimpa onyo asinitafute majira ya usiku, mimi ni mke wa mtu na sikuwa radhi kuivunja familia yangu kwa muda huo.

Baada ya hapo nikaondoka kurejea shuleni, nikamchukua mwanangu na kwenda naye moja kwa moja nyumbani.

Sikufahamu, kumbe Anwari alikuwa ananifuatilia nyendo zangu mpaka mwisho.

Kwasababu ya kujificha nisimwone na kumtambua, Anwari aliacha gari lake mahali fulani akanifuata kwa kutumia usafiri wa kukodi.

Hiyo ndo' sababu pekee sikufanikiwa kumwona siku ile, laiti angelitumia gari lake ambalo nalifahamu vema kama kiganja cha mkono wangu, isingenichukua macho mawili kumbaini.

Hata kama gari hilo lingekuwa limebadili rangi yake ya muda mrefu.

Nakumbuka gari lile lililombeba Anwari kunifuatilia, nilipata kulishuhudia kwa macho yangu kabisa lakini sikufikiria kwa muda huo kama gari lile lipo kwenye misheni maalum, nilidhani ni gari tu lenye shughuli zake, limembeba mtu ama watu wanaokaa katika mandhari yale, kuja kubaini nilikuwa nimeshachelewa.

Siku Anwari ananambia baada ya kumuuliza amepajuaje kwangu , maelezo anayonipa ndo' yananirejeshea kwenye fikra ya gari lile.

Gari dogo rangi ya fedha nililoliona kwa umbali wa mita kadhaa, muda mfupi tangu niliposhuka toka kwenye gari lile la shule linalonichukua na kunirejesha.

Basi siku ile niliyoonana na Anwari, nilifika nyumbani, kama ada, nikafanya kazi zangu na kuweka kila kitu sawa.

Nakumbuka siku hiyo nilimkuta mume wangu kesharudi nyumbani, yu pamoja na Amiri wakishughulikia mifugo.

Bwana huyo alinambia siku hiyo alirejea mapema nyumbani, majira ya mchana, maana alikuwa amechoka sana kwasababu ya ule ulevi wa jana yake usiku, alilalamika kichwa kilimsumbua kweli kazini achilia mbali uchovu hivyo akaona ni vema kurejea mapema.

Lakini mbali na hayo, alinambia habari mbaya alokuta pale nyumbani, matetea mawili ya kuku yalokuwa yanatamia mayai yamekutwa yamekauka huko bandani majira ya asubuhi.

Na chanzo cha matetea hayo kufa, hamna alokuwa anajua.

Habari hiyo ikanikumbusha upesi usiku ule wa jana, usiku ule niliposikia kuku wanalia na kuparura kule bandani.

Kumbe yale nilokuwa nawaza yalikuwa ni sahihi - ya kwamba kuna mdudu ama mnyama aliingia mule bandani?

Mume wangu alinambia wamekagua banda zima pamoja na Amiri lakini hawajaona sehemu yenye uwazi wa kuingiza hata nyoka, hawajui imekuaje kuku wale wakafa kwahiyo basi walihitimisha huenda ni ugonjwa hivyo kuku wapatiwe chanjo upesi.

Niliwatazama kuku wale walokufa, kweli walikuwa wamekauka kana kwamba mti mkavu, viungo vyao vimekakamaa mno, si mbawa wala miguu yao ilokuwa inajikunja, nikahamaki ule ni ugonjwa gani ulowapata?

Kwasababu sikuwa na ufahamu wowote na mambo ya mifugo, nilinyamaza kimya maisha yakaendelea.

Kesho yake, mapema asubuhi, niliwasiliana na rafiki yangu Zai kumjulia hali.

Alinambia ameshatoka hospitali, sasa yuko kwa ndugu yake kwasababu ya uangalizi mpaka pale atakapojihisi yuko sawa.

Nilimuuliza Zai kama alimwambia chochote Anwari kuhusu mimi, Zai akakataa katakata. Nilimweleza Anwari alikuwa anajua kuhusu ujauzito wangu na sasa anajua kama nina mtoto, habari hizo kazitoa kwa nani? Zai akasema hajui kitu.

Hajawahi kuongea jambo lolote na Anwari.

Basi nikampatia ujumbe kuwa kuanzia muda huo sitaki amwambie Anwari kitu chochote kile kunihusu mimi. Sitaki kabisa wanizungumzie huko watakapokutana ama kuongea.

Niliongea kwa kufoka na swala hilo likamkwaza Zai. Alinyamaza kunisikiliza nikiropoka mpaka mwisho wake pasipo kutia neno alafu akamalizia kwa ufupi, "sawa." Kisha akaniuliza, "umemaliza?"

Nikamwambia nimemaliza, hayo yamekwisha.

Akaniuliza, "naweza kukata simu?"

Kabla hajakata, nikamgusia kuhusu lile swala lake la kuonana na yule mama kwaajili ya tatizo lake la kupandwa na kusumbuka na maruwani.

Nilimwambia nimewasiliana na mama Miraji na tayari ameshanipatia muda na siku ya kuonana naye basi tufanye hima tukatimize wajibu wa kutafuta tiba, ajabu mwanamke huyo akanigomea katu, alinambia hana shida, na kama akiwa nayo basi atajua mwenyewe namna ya kuhangaika nayo.

Baada ya kusema hayo, alinikatia simu nikabaki na butwaa.

Zai alikuwa ameghafirika.

Sikuhangaika naye siku hiyo, nikamwacha na mimi nikandelea na mambo yangu. Baada ya kama siku mbili hivi, nilipigiwa simu na Anwari.

Sikutaka kupokea simu hiyo lakini sikuwa na budi kwasababu ya maagano niliyoyaweka. Nilipokea moja kwa moja nikamuuliza bwana huyo anataka nini, hapo akaniuliza mara yangu ya mwisho ni lini kuwasiliana na Zai, nikamweleza ni juzi, basi akanambia Zai amezidiwa sana, na hapo anapoongea na mimi yupo na Zai hospitalini!

Kutazama saa, ni jioni ya saa kumi na moja, tayari nisharudi nyumbani nipo kwenye maandalizi ya chakula cha jioni.

Sasa nafanyaje?

Niliharikisha mambo yangu kisha nikamwita Amiri na kumwambia aketi na mtoto pale nyumbani, mimi natoka kidogo ila nitarudi muda si mrefu.

Niliondoka na mwendo wa dharura, sikupata hata kugusa kile nilichokipika, niliona ni vema nikawahi kwanzan hospitali alafu nitarejea kuendelea na mambo yangu.

Nilikodisha bajaji mpaka huko ambako nilielekezwa, kufika nikamkuta Anwari pamoja na dada ambaye nilimtambua kama ndugu yake na Zai, yule ndugu ambaye kwake ndipo Zai alikuwa akiishi baada ya kutoka hospitali.

Dada yule aliniambia hali ya Zai ilibadilika majira ya jioni, akisema na kubwata maneno yasoeleweka, akipasua na kubamiza vitu alafu ghafla akaanguka chini na kupoteza fahamu!

Hapo ndo' akafanya jitihada za kumleta mwanamke huyo hospitali, moja kwa moja akaingizwa kwenye chumba cha dharura na hata sasa akiwa chini ya uangalizi wa madaktari.

Walipopata wasaa wa kusema na daktari waliambiwa mwanamke huyo anasumbuliwa na presha kali ya kupanda, moyo wake umetanuka, hivyo kwa muda kidogo watabaki naye mpaka pale watakapoona ni muda sahihi kumruhusu.

Gharama za siku hiyo, zote kuanzia usafiri mpaka vipimo vya Zai, bwana Anwari alivifunika kwa kuvilipia 'cash', pesa kutoka mfukoni mwake.

Bwana huyo alitoa pesa pasipo kugugumia wala kunung'una. Nilimtazama usoni akiwa anatoa pesa kweli nikaguswa na tukio lile.

Moyo wa kipekee kabisa.

Lakini jambo lile lilinipa mwanga ni kiasi gani Zai na Anwari walivyokuwa wameshibana. Nikajiaminisha moyoni mwangu kuwa kweli Zai alimpa maneno yale bwana Anwari. Maneno kunihusu mimi.

Baada ya kukaa hapo hospitali kwa takribani masaa mawili, niliona niage niende nyumbani maana muda ulishanitupa mkono.

Bahati haikuwa na mimi, muda wote n'lokaa hapo sikufanikiwa kumwona rafiki yangu Zainabu zaidi ya kuambiwa tu hali yake na vinywa vya watu wengine.

Niliahidi nitarejea tena kesho asubuhi, kwa muda huo waniache tu niende maana nimeacha mtoto mpweke na mume atakuwa yu njiani kurudi nyumbani.

Baada ya kueleza hayo, Anwari alisema;

"Naomba nikupeleke kama hutojali."

Sikukubali.

Nilimsihi abakie hapo pamoja na yule dada, ndugu yake na Zai, mimi nitaenda mwenyewe.

Lakini bwana yule hakukoma, aliendelea kusisitiza ya kwamba muda umepita na hivyo ni vema tukaenda wote ili anisogeze.

Kweli kutazama muda nikaona nimechelewa mno, nikamwambia bwana yule anisogeze mpaka mahali fulani, si mbali sana na nyumbani kwangu, hapo nitajua cha kufanya kufika ninapoishi.

Akaridhia.

Alinibeba na gari yake, na pasipo hata kumwelekeza makazi yangu yalipo, akanyoosha na njia kwenda mwelekeo sahihi.

Tulienda kilomita kadhaa, sikujua nini kilitokea, lakini nilianza kuhisi kichwa changu kizito, sioni vizuri na siwezi kuongea.

Nilijipapatua nikauliza; "Anwari, nini kina ..." Sikumalizia kauli yangu nikabebwa na usingizi mzito mno mno, nilikuja kupata ufahamu kesho yake nipo juu ya kitanda cha Anwari, sina nguo yoyote mwilini mwangu!

Shuka limenifunika upande mmoja tu, huko kwingine ni Mungu nisadie.

Kutazama saa ya simu yangu ni saa tatu ya asubuhi! 'Missed calls' kumi na tatu za bwana Mgaya, ujumbe ndo' usiseme, kweli nikajikuta napagawa na roho yangu.

Mungu wangu! Mungu wangu! Nini hiki?

Nilikurupuka pale kitandani nikaangaza huku na kule, sikuona nguo zangu, nilimtafuta Anwari naye sikumuona, niliita jina lake mara tatu lakini hakuna aliyenijibu, kimya nyumba nzima.

Sijakaa vema, simu ya Mgaya ikaita tena, sikuelewa nipokee ama niache.

Nikipokea nasema nini?

Nikiacha nitaenda kusema nini?

Sikuelewa nataka nini, sikuelewa nafanya nini?

Nikiwa nimeshikilia shuka langu kunisitiri, mara nikaona mlango wa chumba nilichomo unafunguliwa, kutazama ni Anwari.

Bwana huyo aliingia akiniuliza, "umeamkaje, mpenzi?"

Nikajikuta najisema mwenyewe rohoni...

Maneno ya ghadhabu,

K*mmmmmmk zako Anwari!


***
 
🤣🤣🤣🤣🤣🤣🤣🤣

Anwari utalipa hili. Siyo siku nyingi bali hivi karibuni. Umembaka Mage? Hahaha basi naye atakutoa roho yako hivi karibuni.

Nasikitika kutangaza kifo cha Anwari mapema kuliko nilivyotegemea.
 
Nawaza kwa sauti.

Je, tukio hili halikuwezi kuwa limepangwa kiustadi kati ya Anwari na Zai?

Mage kaongea na Zai kumkataza kutoa taarifa zake kwa Anwari. Zai akachukia, akagomea mpaka na miadi ya kumuona Mama Miraji.

Jioni Anwari anapiga Zai kuwa mahututi. Mage analazimika kwenda kumuona shoga yake. Anwari anagharamikia matibabu ya Zai kwa malipo ya awali. Unganisha dots hapo. Anashawishiwa na Anwari amsogeze kwa kuwa tayari muda umeenda.

Anaingia kwenye gari la Anwari. Anapuliziwa madawa ya usingizi. Anwari alifanyaje? Mbona yeye hakuathirika endapo gari zima lilikuwa limepuliziwa dawa? Maana yake alishajipanga mapema. Siyo ishu ya kujiandaa ndani ya dakika chache. Na bila shaka dawa ilikuwa katika kiwango kikubwa. Masaa zaidi ya 12 baada ya mhusika kuivuta.

Je, nini kitaharakisha kifo cha Anwari?
1. Hasira ya kubakwa
2. Kumuacha mtoto usiku mzima
3. Kutoeleweka kwa Bw. Mgaya
4. Kumpanda kichwani kuhusu mtoto

Rest in Peace in Advance Anwari.

Zai to follow.
 
Back
Top Bottom