Niliweka shada za maua kwenye makaburi matano ya watu wangu wa karibu

Niliweka shada za maua kwenye makaburi matano ya watu wangu wa karibu

Sehemu ya Kumi:


Nilikurupuka sana, kichwa kinaniwaka moto, nikavaa nguo zangu kama nakimbizwa lakini tena nikazivua.

Mwili ulikuwa umechunda kwa jasho. Harufu haieleweki. Vipi nikikutana na Mgaya nyumbani? Akihisi harufu hii haitakuwa tabu?

Nikakimbilia bafuni kuoga, nilijimwagia maji upesiupesi, hata sabuni haikutoka vizuri mwilini nikawa nishatoka na taulo kujifuta.

Nilijipakaa mafuta toka kwenye mkoba wangu, nikavaa upesi na kutengenezea nywele zangu vema, vilevile kama nilivyotoka nyumbani, nilipomaliza nikajipulizia marashi, yale aloniletea mume wangu kama zawadi, baada ya hapo nikawa tayari kuondoka.

Hapo nilitumia robo saa tu mpaka kuwa mkamilifu. Siku ile ndo' nilijua kumbe kujiandaa harakaharaka naweza, maana mimi desturi yangu ni kutumia si pungufu ya lisaa na kitu kwenye kujiandaa tu.

Muda wote huo nikiwa najiandaa, Anwari alikua amejilaza kitandani akinitazama, japo nilikuwa nafoka na kutusi juu, bwana yule hakuonekana kujali, ni kama vile alikuwa anafurahia yale yanayoendelea pale, namna mimi ninavyoteseka na kuhanyahanya.

Aliniuliza nikupeleke? Nikamjibu sitaki hata kuona sura yako, Anwari, achilia mbali kunipeleka.

Kwa hofu nilokuwa nayo, nilichuruza jasho japo nilitoka kuoga muda si mrefu na mule chumbani kulikuwa na kiyoyozi kinachoyoyoa hewa kwa mbali.

Anwari aliniambia; "sasa kama hutaki nikupeleke, utapata wapi usafiri haya maeneo yetu?"

Japo sikutaka kuzungumza naye wala kuongozana naye, ila alichokisema Anwari kilikuwa ni kweli, kule alipokuwa anaishi kulikuwa ni mbali na kituo cha magari na sikuwa na namba yoyote ya dereva aidha pikipikipiki au bajaji.

Kwahiyo hapa nikajikuta namrejea tena Anwari kama waswahil na baniani mbaya ...

Bwana huyo aliongozana na mimi, ndani ya gari yake, simu yangu nimeishikilia mkononi nawaza niandike nini ama nimpigie nani na ninwambie nini.

Niimtazama Anwari, nikayawaza mengi kichwani mwangu, Anwari ni nini umenifanyia? Nilimuuliza. Anwari, kwanini umenifanyia hivi?

Unajua kabisa nina familia nyumbani, mtoto na mume pia, hayo kwako hayakutosha?

Naye akanijibu kwa kuniuliza, kama ningekuambia ungenikubalia? Kisha akaongezea, si ungeanza kusema ngonjera zako za mimi ni mke wa mtu, nina mume wangu?

Bwana huyo akahitimisha akisema alikuwa ananihitaji na ndo' maana akafanya vile.

Akafanya ....?

Hapo ndo' fikra zangu zikakumbuka mchezo ulipoanzia.

Nikiwa pale kwenye benchi la kungojea, mimi pamoja na yule ndugu yake Zai, bwana Anwari alituomba radhi akatoka idogo kwenda mahali nisipopafahamu.

Baada ya dakika kadhaa, bwana huyo alirejea akiwa na chupa mbili za soda na 'foil' lillokuwa na nyama ya kukaanga ndani yake, akaniambia shika hii nimekuletea, najua una njaa.

Na ni kweli nilikuwa na njaa, nyumbani nilipika lakini ile dharura yangu ilin'tia pupa nikaondoka tumbo likiwa tupu, sikuwa nimekula tangu majira ya mchana, tena mchana wenyewe niligusagusa tu chakula cha shuleni maana nacho huwa cha hovyo.

Kwahiyo kwa ile njaa nilokuwa nasikia, 'foil' na kinywaji kile niliviona kama mkombozi.

Nilipovishika niliacha vinipe ahueni ya hali yangu, na kweli vikaninusuru, lakini kumbe vilitumwa kwa mkakati maalum.

Mkakati wa kunidhoofisha taratibu kadiri na muda.

Anwari alijua kunipata kweli, na alijua kunitumia. Makosa yale niliapa kutoyarudia kamwe katika mikono yake.

Huwezi kuamini alinambia, kama mimi nilivyokuwa namhitaji kipindi kile mpaka nikamrubuni akalala na mimi, basi naye ndivyo hivyo hivyo alivyofanya, hamna mwenye dhambi kumshinda mwenziwe.

Aliponifikisha maeneo fulani ambayo naweza nikapata usafiri kwa urahisi, nilimtaka anishushe niende zangu mwenyewe.

Niliposhuka nilinyookea moja kwa moja nyumbani nikitumia usafiri wa pikipiki, kufika Amiri ananipokea mkoba na pia ananipokea kwa maneno ya yale yalotukia pale nyumbani.

Alinambia bwana Mgaya hayupo, ametoka na mtoto kwenda asipopajua lakini alienenda akisema lengo lake ni kunitafuta mahali nilipo kwani simu zake hazipokelewi na hana habari yoyote ile.

Amiri alinambia bwana Mgaya alikuwa kama mtu alochanganyikiwa, anaongea mwenyewe na kufokea hewa, hata alipoingia kwenye gari lake alisahau funguo, alipoenda kuuchukua ufunguo akamsahau mtoto, alipomrejea mtoto akasahau simu!

Alienda akarudi akipiga honi nyingi, niletee simu yangu, niletee simu yangu!

Katikati ya masimulizi hayo ya Amiri, mara simu yangu ikaita, kutazama ni yuleyule tulokuwa tunamwongelea, yaani bwana Mgaya, nikapokea simu hiyo kwa mara ya kwanza na kumwambia niko nyumbani, nimeingia hapo muda si mrefu.

Alipotaka kuniparamia kwa pupa ya maswali, nikamwambia aje kwanza nyumbani, tutaongea kila kitu, haina haja ya kumaliza muda na salio la simu.

Basi nikiwa naongea na simu hiyo ya bwana Mgaya, bado hatujamalizana, mara simu nyingine ikawa inaingia na kuita 'diiii-diiii diii-diiii' kutazama naona jina la Anwari kwenye kioo!

Hii ndo' sababu sikuwa nataka kumpatia bwana huyu namba yangu, najua hana mipaka, hajui muda gani wa kutulia na muda gani wa kutenda, kweli anapiga muda huu na yale yote yalotokea?

Vipi kama ningemkuta bwana Mgaya pale nyumbani?

Mgaya alipokata simu, nilipokea ile simu ya Anwari nikafoka kumuuliza anataka nini? Anahangaika nini na mimi muda huo baada ya kunitenda yote yale? Ajabu bwana yule akawa anaongea mambo nisiyoyaelewa, alikuwa anabwata kama mtu alozidiwa na ulevi na mimi baada ya kuona huo ni upuuzi, nikakata simu yake.

Nilikata simu hiyo lakini nikaendelea kuongea mwenyewe kama mwehu. Nasonya kila mtindo.

Amiri aliyekuwa amesimama kando ananitazama kana kwamba bango, aliniuliza, "kuna tatizo?"

Sikumjibu, nikaingia zangu ndani moja kwa moja mpaka chumbani.

Muda si mrefu, bwana Mgaya akiwa ameongozana na mtoto wailifika nyumbani kikazuka kikao cha dharura.

Bwana Mgaya alikuwa amefura kwelikweli na mimi sikuwa na kingine cha kumweleza isipokuwa kumtumia mgonjwa Zai kama ngao yangu.

Nilimwambia rafiki yangu Zai yu hospitali amelazwa na mimi nilikimbilia huko kumwona baada ya kupewa taarifa hiyo mbaya.

Aliniuliza mbona sikuwa napokea simu yangu wala kurejesha jumbe zake lukuki? Nikasema simu yangu niliisahau nyumbani kwa zile haraka zangu, nilikuja kubaini sina simu nilipofika hospitali na sikuwa na namna tena.

Nilimwambia: "kumbe niliisahau simu jikoni ndani ya shelvu, nilivyorudi Amiri akanisaidia kupekua huku na kule maana simu yenyewe haikuwa na sauti, hata kuipiga isingesaidia."

Hapo nilimtazama Amiri, Amiri naye akajua kila jambo ndani yangu, sikuhitaji kumweleza kitu zaidi ya yale macho mangu, naye akashika hatamu kama vile tulikaa kitako kuyapanga yale mambo.

Akamweleza Mgaya namna tulivyotafuta simu mule ndani na namna mimi nilivyohamaki baada ya kuipata simu hiyo na kuona jinsi Mgaya alivyonitafuta.

Aliyaeleza mambo katika namna ambayo alinishangaza. Aliyasema kwa kujiamini pasipo kupepesa macho hata kunishinda mimi mtunzi wa wongo ule.

Alipomaliza hayo maelezo, Mgaya akabakiwa na hoja dhaifu, hakuwa na kingine cha kusema zaidi ya kukazia kwenye swali lake la kwanini usingechukua simu ya mtu mwingine ukanipa taarifa?

Alisema alikuwa na hofu sana juu ya usalama wangu kiasi cha kuanza kufikiria kupita vituo vya polisi ama kupita hospitalini kuniulizia.

Alisema laiti asingeniona siku hiyo nzima, basi angeanza zoezi hilo mara moja.

Baada ya hiko kikao, niliongozana na Mgaya kwenda naye chumbani, sasa nina amani maana kikwazo kile nimekikwatua.

Baadae nilipiga simu kule hospitali kwa ndugu yake Zai kumuuliza hali ya mgonjwa, nilipopata taarifa njema nikaendelea na ratiba yangu ya kawaida, nikipanga kesho ama keshokutwa nikitoka shule basi nipitie tena hospitali kumjulia hali rafiki.

Kweli baada ya siku mbili, kama nilivyopanga, nilifika hospitali na huko nikamkuta Zai anangoja kupewa bili yake ili apate kurejeshwa nyumbani, hali yake ilikuwa njema, si haba.

Bili ikatoka anadaiwa kama laki sita hivi kwa ujumla, achilia mbali bili ya siku ile ambayo Anwari alikuwa amemsaidia.

Sasa shida ikaja Zai hakuwa na pesa hiyo mfukoni, kwa maelezo yake alibakiwa na laki mbili tu kama akiba, akitoa hiyo hajui atadumu vipi na maisha mpaka kuja kuupata mwisho wa mwezi.

Hata yule ndugu yake anayekaa kwake hana kazi ya maana hivyo mbali na kumhudumia, kwenye swala la mambo ya pesa ni mtu dhoofu l'hali, pangu pakavu tia mchuzi.

Zai alisema; "Anwari aliniahidi atanisaidia kwenye hili janga langu mpaka mwisho wake lakini hata sasa simwoni."

Alisema amejaribu sana kumpigia Anwari pasipo mafanikio, mwanzoni simu yake ilikuwa inaita lakini sasa hivi imekuwa kimya. Ukipiga hapatikani.

Anawaza ni nini kimemkuta bwana huyo kwani si kawaida yake kupitisha siku asije kumwona, achilia mbali zimeshapita siku tatu sasa!

Alilalamika gharama za pale ni kubwa sana, kama ingekuwa ni kwa utashi wake mwenyewe asingekuja hospitali hiyo, angeenda zake hospitali za serikali, lakini Anwari alimsisitizia hapo maana anaamini pana huduma nzuri.

Sasa Anwari hapatikani, anafanyaje?

Nilitazama uwezo wangu binafsi wa kumsaidia rafiki Zai katika adha ile lakini bado sikufua dafu.

Kujikamua kote mifuko yangu niliambulia laki moja na alfu hamsini tu ya akiba ingali pesa inayohitajika pale hospitalini ni pomoni.

Nikajaribu kumpigia Anwari, simu haipatikani. Nikajaribu tena, bado haipatikani.

Nilijaribu kama mara tano lakini hamna nilichoambulia zaidi ya mhudumu kunihasa namba ya mteja ninayempigia hapatikani kwa muda huo.

Hapo akili yangu ikanikumbusha maongezi yangu ya mwisho na mwanaume yule.

Yale maongezi baada ya kuongea na Mgaya.

Yale maongezi niliyomfokea na kumtukana.

Nilichokumbuka katika maongezi hayo ni namna bwana huyo alivyokuwa anazungumza kana kwamba mwendawazimu mpaka mimi nikaikata simu yake.

Sasa leo hii hapatikani, na si tu leo ni tangu siku ile nilipoteta naye hewani.

Anwari, nini kimekukumba?

Sasa nikajiuliza na kichwa safi kisichokuwa na mawingu ya hasira.

Kwanini siku ile ulinipigia?

Ulikuwa unataka kuniambia nini ambacho sikuelewa? Na hicho ulichotaka kuniambia kina mahusiano na wewe kutokuonekana hospitali ama kutopatikana hewani?

Nikamwambia Zai acha niende nyumbani kwa Anwari nikatazame.


***
 
Ewe dada ambaye leo ulikuwa katika ofisi ya basi la Nacharo, hapo Tanga, ukikata tiketi ya kuja Dar, nashukuru sana kwa support yako, niliona unapitia story hii kwa umakini sana wakati ukingoja basi ling'oe nanga.

Msalimie na huyo dada aliyekuwa amevaa hijabu pembeni yako. Huyo ambaye ulikuwa ukimsomea kisa hiki kwa sauti.
 
Ewe dada ambaye leo ulikuwa katika ofisi ya basi la Nacharo, hapo Tanga, ukikata tiketi ya kuja Dar, nashukuru sana kwa support yako, niliona unapitia story hii kwa umakini sana wakati ukingoja basi ling'oe nanga.

Msalimie na huyo dada aliyekuwa amevaa hijabu pembeni yako. Huyo ambaye ulikuwa ukimsomea kisa hiki kwa sauti
kimenuka
 
Back
Top Bottom