Mkono Slaa ni muongo
Shadrack Sagati
HabariLeo; Saturday,September 22, 2007 @00:05
MBUNGE wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM), amejibu tuhuma za ufisadi zilizoelekezwa kwake na kueleza kuwa tuhuma hizo amezushiwa kutokana na wivu wa baadhi ya wanasheria wenzake baada ya yeye kusaidia Benki Kuu (BoT) isilipe mabilioni ya fedha za walipa kodi kwa watu binafsi.
Mkono ambaye ni wakili maarufu na wa kimataifa, alisema madai yote yaliyotolewa na Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa (Chadema) ni ya uongo yenye lengo la kuchafua jina lake.
Amemtaka Mbunge huyo aliyemwelezea kuwa ni ‘Padri wa Kanisa Katoliki' kutubu mbele ya Mungu kutokana na kumzushia madai ya ufisadi. Dk. Slaa aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Akizungumzia tuhuma moja moja kati ya tatu zilizoelekezwa kwake, Mkono alikiri kulipwa fedha ambazo alidai ni malipo yake halali katika kesi ya Benki Kuu Tanzania (BoT) ya kudaiwa Sh bilioni 60 na Valambhia. Lakini alisema tangu aanze kutetea BoT mwaka 2003, amefanikiwa kuepusha gavana asifungwe na kuokoa mabilioni ya fedha kulipwa kwa waliofungua kesi hiyo.
Wapinzani wanamtuhumu Mkono kuwa amelipwa Sh bilioni 8.1 sawa na asilimia ya 15 fedha ambazo BoT inadaiwa.
Mkono katika kujibu hoja hiyo hakutaja kiasi cha fedha ambacho amelipwa hadi sasa, lakini alitoa mchanganuo wa Sh bilioni 2.1 ambazo mawakili wake wa nje ya nchi wamelipwa kutokana na kushiriki kwenye kesi hiyo kuanzia mwaka 2004 hadi Juni mwaka jana.
Alisema katika kesi hiyo kampuni yake inawakilishwa na mawakili wanane. Mawakili wanne wa hapa nyumbani na wawili wa Ireland na wengine wawili kutoka iliyokuwa Czechoslovakia. Alisema wakili wa hapa nyumbani akisimama mahakamani analipwa dola 500 za Marekani kwa saa moja wakati dola za Marekani 1,000 kwa saa moja zinalipwa kwa mawakili wa nje ambao wanasaidia kwenye kesi hiyo.
Mbunge huyo wa Musoma Vijijini alisema kesi hiyo iko katika nchi tatu, Czech, Ireland na hapa nchini. Alisema ndiyo maana kampuni yake inatumia mawakili wa kigeni kuitetea Tanzania katika kesi zinazotajwa katika nchi hizo za nje.
Hata hivyo, alisema mkataba wa malipo kati yake na BoT uko wazi na haujavunja kanuni ya malipo ya uwakili kama ilivyodaiwa na wapinzani.
"BoT ni lazima watulipe fedha kila mwezi kutokana na mkataba tulioingia. Walikuja kuniomba niwasaidie baada ya mahakama kutoa hukumu ya kufungwa gavana. Sasa tumefanikiwa gavana hafungwi tena na tayari tumegundua kuwa kulikuwa na njama za kughushi," alisema Mkono.
Aliongeza kuwa katika kesi hiyo BoT ilitakiwa kumlipa Valambhia malipo ya aina tatu ambayo ni asilimia 45 ya fedha zinazodaiwa, dola za Marekani milioni 160, riba na gharama za mahakama.
Mkono alisema yeye kwa kutumia juhudi zake alizuia gavana asifungwe kama ilivyosema hukumu ya awali kabla ya yeye kuanza kushiriki kwenye kesi hiyo.
"Sasa baada ya kuzuia fedha za umma nyingi zisitolewe, mimi naambiwa fisadi. Lakini ninachotaka kusema ni kwamba walioungana na wapinzani kunichafua ni mawakili wa Valambhia kwa sababu tayari mteja wao amefariki dunia na wao wanataka malipo kutoka BoT.
"Angalia wakati kesi inaanza hawa mawakili walidai walipwe dola za Marekani milioni 9.9 (Sh bilioni 10 na sasa hivi mawakili hao akiwamo Marando (Mabere) wanaomba walipwe dola za Marekani milioni 19.8 ( Sh bilioni 23.7).
"Je, kati yangu na hawa ni wapi mafisadi?" alihoji huku akitoa vielelezo vinavyoonyeshwa kuandikwa na kampuni ya uwakili ya Marando & Mnyele ya Dar es Salaam, za kutaka malipo hayo.
Alidai baada ya yeye kuisaidia hadi BoT ikazuia malipo hayo, ndiyo maana Marando yuko mbele kushabikia madai hayo ya ufisadi yaliyoelekezwa kwake yeye Mkono.
"Hawa ni wivu tu ndiyo unaowasumbua, wanaona mimi ni wakili maarufu na nina uwezo wa kuwa na ofisi nzuri kama hii, jambo ambalo wao hawaliwezi," alidai Mkono akiwa ofisini kwake, Jengo la PPF Towers.
Marando alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo, alikiri kuwa wanamwonea wivu Mkono kwa vile wamemshinda katika kesi zote ambazo yeye amekuwa anaitetea BoT, lakini ajabu ni kwamba Mkono analipwa fedha na wao wanaoshinda kesi zote, hawajalipwa hata senti moja.
Alihoji kuwa katika kesi hiyo walimshinda Mkono hadi mahakama ikaamuru gavana Daud Ballali afungwe au alipwe faini kwa kudharau mahakama. Alilipa faini ya Sh 400,000 akaponyeka kwenda jela.
Marando aliongeza kuwa kampuni yake na ya Moses Maira zina haki ya kulipwa fedha hizo kwa vile wao ndiyo wameshinda katika kesi hiyo.
"Sio siri tunamwonea wivu huyu Mkono… iweje yeye anashindwa katika kesi analipwa fedha na sisi tulioshinda hatulipwi. Angalia katika mashauri yote mahakama iliamuru tulipwe baada ya kushinda na mwenye kutulipa ni BoT, lakini mkono hataki tulipwe fedha hizo," alisema Marando.
Hata hivyo, Marando alikanusha kuwatumia wapinzani, bali alisema Dk. Slaa aliona nyaraka hizo za Kampuni ya Mkono kulipwa Sh bilioni nane kutoka kwa ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Mkono pia alikanusha tuhuma kuwa ni mkurugenzi wa kampuni mbalimbali zilizotajwa na Dk. Slaa. Aliwataja wakurugenzi wa kampuni anazotuhumiwa kama kampuni ya Azania Agricultural ambayo alisema kwa mujibu wa Wakala wa Msajili wa Makampuni (Brela) wakurugenzi wake ni Jayantikumar Chandubhai Patel, Sarbjitsingh Bharya na Alex Khalid.
Kuhusu kampuni ya Viatu ya Liberty Leather wakurugenzi wake ni Patel, Bhara na Robert Feruzi ambao pia ni wa wakurugenzi wa kampuni ya Azania Eximco.
Akizungumzia kutajwa kuhusiana na kashfa kubwa ya ufujaji au ubadhirifu wa fedha za umma kwa kushirikiana na kampuni mbalimbali za V. Chavda, Mkono alikanusha madai hayo na akaeleza kuwa yeye alikuwa wakili wa Chavda baada ya kutakiwa kuondoka nchini.
Mkono alisema yeye kama wakili ana leseni ya kutetea wahalifu hata awe muuaji, lakini kamwe hawezi kuwa mhusika kwenye tuhuma za mteja wake. Alikiri kuwa yeye alimtetea Chavda asifukuzwe nchini, hali iliyosababisha achukiwe na kulaaniwa, lakini alikuwa anatekeleza wajibu wake.
"Huyu Dk. Slaa kafunguliwa kesi kule kwenye jimbo lake, hivi wakili wake naye alihusika kwenye tuhuma anazotuhumiwa? Sasa anawaambia watu milioni 35 waamini uongo wake, anasema uongo wakati yeye ni Padri! Kwa kweli sijawahi kusikia wakili akitetea kesi naye anakuwa mtuhumiwa," alisema.
Kuhusu tuhuma kuwa yeye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Oxford Service Ltd na Marcus Ltd ambazo zilifaidika kupata Sh bilioni 4.5 chini ya utaratibu wa uuzaji wa madeni (Debt Conversion Programme), Mkono alisema hizo ni kampuni za kigeni ambazo zilikuwa wateja wake katika mpango huo wa DCP.
Alisema mpango wa kuuza madeni kwa dola ulisaidia taifa kupata fedha za kigeni "Sijui nisingekuwa mimi hii nchi ingekuwa wapi leo hii, maana mimi nilisaidia kuwa wakili wa kampuni hizi na mpango huo ukafanikiwa. Je, kuwa wakili ni ufisadi, ufisadi wangu uko wapi hapa?" alihoji.
Alisema anashangaa kwamba ‘Padri' Dk. Slaa anaomba Mungu majina yabadilishwe kwenye kampuni hizo na jina la Mkono liwamo. Alisema Mbunge huyo alipaswa kwenda kumuuliza yeye Mkono kuhusiana na kuhusika kwake na kampuni hizo na siyo kukurupuka kumtangaza kuwa yeye ni fisadi wakati yeye anafanya kazi ya uwakili.
Pia alimshangaa Dk. Slaa kumdhalilisha Rais Jakaya Kikwete kuwa ni fisadi. Alisema demokrasia ya vyama vingi inatumiwa vibaya na akahoji kutokuwapo kwa sheria ambayo inapiga watu marufuku ya kumtukana rais.
"Angalia rais yuko Marekani anasaka fedha kidogo zije zitusaidie, lakini kuna watu huku nyuma wanamtukana, hiyo ndiyo demokrasia kweli?" alihoji Mbunge huyo.
Mkono ni miongoni mwa viongozi 10 waliotajwa na Dk. Slaa wakituhumiwa kuwa ni mafisadi ambao wanaitafuna nchi. Mbunge huyo aliwataja kwa kushirikiana na Tundu Lissu ambaye ni mwanasheria kama njia ya kuwashtaki viongozi hao kwa wananchi.