James...
Mimi si mtu wa ubishi kwani ubishi haujengi mjadala bali unabomoa.
Hivi kwa nini wewe ushughulishwe na jambo la kupokelewa?
Kwani lina kipi kikubwa sana?
Kubwa kwa Nyerere wakati ule ni yeye kupelekwa na kujulishwa kwa Mufti Sheikh Hassan bin Ameir na Abdul Sykes.
Hili ndilo kubwa katika historia ya Nyerere.
Mwezi October 1999 nilikuwa Dubai na nikikaa Carlton Hotel.
Siku moja jioni simu yangu ikalia.
Walikuwa BBC London Idhaa ya Kiswahili wanataka kunihoji kuhusu Mwalimu Julius Nyerere ambae wakati ule alikuwa amelazwa St. Thomas Hospital, London.
Ulikuwa mwaka wa pili toka kitabu changu, ‘’The Life and Times of Abdulwaid Sykes (1924- 1968) The Untold Story of the Muslim Struggle Against British Colonialism in Tanganyika,’’ kichapwe na kitabu hiki kikawa kimenifanya nifahamike na sababu kubwa ni kuwa kilikuja na historia mpya ya yeye Mwalimu Nyerere mwenyewe, historia ya TANU na historia nzima ya kudai uhuru wa Tanganyika.
Kitabu kilimweeleza Mwalimu Nyerere kwa namna ambayo hakuna mwandishi alipatapo kufanya hivyo.
Hii nadhani ndiyo ikawa sababu ya BBC kutaka kunisikia nikimzungumza Mwalimu Nyerere.
BBC wakawa wanataka tuzungumze kidogo kuhusu Mwalimu na jinsi Watanzania walivyoathirika na ile hali ya Mwalimu kuwa kwenye matibabu Uingereza.
Katika kipindi kile cha maradhi ya Mwalimu akiwa hospitali kila siku habari ya hali yake ilikuwa inatolewa na kwa kweli sote tukifuatilia kwa karibu sana hadi pale alipofariki tarehe 14 Oktoba 1999.
Kishindo chake kilikuwa kikubwa hakijapatapo kutokea na mazishi ya Mwalimu hayapata kutokea halikadhalika simanzi iliyoonyeshwa na Watanzania haijapatapo kutokea.
Umma mkubwa usio na kifani ulijitokeza kupokea jeneza lake Uwanja wa Ndege na maelfu ya watu walijipanga pembeni ya barabara kutoa heshima zao wakati jeneza lake lilipokuwa linapita kuelekea nyumbani kwake Msasani.
Mimi nilikuwa Tanga nikifuatilia kwenye TV na binafsi fikra nyingi zilipita katika kichwa changu.
Mimi sikupata kujuana na Mwalimu lakini katika utafiti wangu wa maisha ya Abdul Sykes na harakati za uhuru nimemjua kwa karibu Mwalimu Nyerere kushinda wale waliokuja kuwa karibu na yeye baada ya uhuru.
Katika utafiti nimekutana na Mwalimu Nyerere ndani ya Nyaraka za Sykes na ndani ya nyaraka hizi nimesoma barua zake akiwa Rais wa TAA na kisha TANU katika miaka ya mwanzoni ya 1950, nimezungumza na Ally Sykes na Dossa Aziz na Mama Daisy (mke wa Abdul Sykes) watu waliokuwanae toka siku ya kwanza wanaanza mapambano ya kudai uhuru.
Katika mikoa ya Tanzania nilikokwenda kwa utafiti nimekutana na kuzungumza na watu waliokuwanae bega kwa bega katika siku hizo za mwanzo wakati Mwalimu Nyerere ndiyo anaanza harakati za kudai uhuru wa Tanganyika akiwa kijana wa miaka 30.
Wakati naangalia TV usiku mmoja wakionyesha ndege ya Air Tanzania Corporation (ATC) iliyokwenda kuchukua mwili wa Mwalimu Nyerere London camera ikapita kwa Abbas Sykes kwa haraka lakini nilimtambua bila wasiwasi wowote kuwa ndiye yeye.
Wakati ule yeye alikuwa ndiye Mwenyekiti wa ATC nafasi aliyoteuliwa na Rais Benjamin Mkapa.
Nilikuwa na kawaida kila nikija Dar es Salaam kutoka Tanga lazima nipite ofisini kwa Bwana Ally Sykes kumjulia hali kisha niende nyumbani kwa Balozi Abbas Sykes.
Safari hii nilikwenda kwa Balozi Sykes kwa nia khasa ya kutaka kujua safari yake ya London kwenda kuchukua mwili wa Mwalimu Nyerere.
Bwana Abbas tukiwa mimi nimekaa kwenye kiti changu ninachokipenda ndani ya ukumbi wake, kiti ambacho kinanipa mandhari ya mchanga mweupe wa bahari na bahari yenyewe na yeye kama kawaida amekaa kwenye kiti cha baba mwenye nyumba kwani huwa siku zote ndicho kiti chake nilianza mazungumzo kwa kumpa pole kwa msiba wa Mwalimu Nyerere.
Balozi Sykes akaitikia ile pole yangu kisha akasema, ‘’Unajua mimi kama Mwenyekiti wa ATC nilitiwa katika msafara wa kwenda kuuchukua mwili wa Nyerere.
Ingekuwa si hii nafasi yangu ya uenyekiti nisingepata fursa na heshima ile kwani hawa viongozi walioko madarakani hawajui kuwa Nyerere sisi ni ndugu yetu.’’
Nilijua bila ya kuuliza kuwa ile, ‘’sisi,’’ Balozi alikusudia wao Sykes Brothers.
Nilikuwa sijapatapo kumsikia Bwana Abbas akijinasibisha udugu na Nyerere.
Mara zote alipokuwa akieleza harakati za kudai uhuru alikuwa akimweleza Nyerere katika nafasi ya urafiki wake na kaka yake Abdul na kama kiongozi wa TANU, hili la udugu ndiyo siku ile nalisikia kwa mara ya kwanza.
‘’Mimi nimejaaliwa kumuona Nyerere siku ya kwanza kaja kwetu pale Mtaa wa Stanley na Sikukuu kaja kumuona Bwana Abdul akiwa kaongozana na Joseph Kasella Bantu na kuanzia hapo tukawa kama ndugu mama yake Bi. Mugaya akafahamiana na mama yetu na akawa anamtembelea mama nyumbani kwake pamoja na Sophia dada yake Nyerere.
Nikajuana na Joseph mdogo wake na Mama Maria Nyerere ambae alikuja kuwa shoga mkubwa wa Mama Daisy.’’
Bwana Abbas alipomaliza utangulizi huu na hapa alinistua kwani ingawa vifo siku zote vinatokea lakini huwa hatupendi kusikia vile vitu vya karibu vinavyomgusa maiti kama jeneza sanda na kadhalika.
Bwana Abbas akanieleza hali ilivyokuwa ndani ya ndege, ‘’Mohamed Nyerere nimejuananae kuanzia mwaka wa 1952 mimi kijana wa miaka 23 mdogo sana hata Bwana Abdul alikuwa mdogo kwa Nyerere.
Ndani ya ndege tuliweka sanduku lililokuwa na mwili wake mbele kabisa tumelifunika na bendera ya Tanzania.
Ilikuwa tabu sana kwangu kukwepa kulitazama sanduku lile lenye mwili wa Nyerere.
Kila mara fikra zinakwenda mbele na kurudi nyuma zinakwenda mbele zinarudi nyuma namkumbuka Nyerere kijana na Bwana Abdul kijana wote vijana wako pale nyumbani kipindi kile ameacha kazi na siku za mwanzo za TANU.
Endapo mtu angelinambia kwa wakati ule kuwa Nyerere atakuja kuwa kiongozi mkubwa barani Afrika ingekuwa tabu kwangu kuamini kuwa mambo yale waliyokuwa wanayanzungumza wakipanga na kupangua yatakuja kuwa makubwa kwa kiasi kile kilichofikia.
Nimekuwa na Nyerere kwingi Ulaya katika mikutano na nimeshuhudia kwa macho yangu viongozi wenzake na watu maarufu duniani wanavyokuwa wakiwa mbele yake.
Kwangu mimi ile ilikuwa historia inafunguka mbele ya macho yangu ya mtu niliyemuona akitembea kwa miguu mitaa ya Gerezani akiwa na mimi au na Bwana Abdul wakienda kumuona huyu au yule.