Nguruvi,
Mjadala ulianza hapa na kurahisisha mambo naweka mwanzo wake kisha In Shaa Allah nitaendelea kujibu hayo uliyoandika:
KWA NINI BENJAMIN MKAPA ALISHINDWA KUCHAPA TAAZIA YA ABDUL SYKES KATIKA THE NATIONALIST BRENDON GRIMSHAW AKACHAPA "OBITUARY" YA ABDUL SYKES KATIKA SUNDAY NEWS (TANGANYIKA STANDARD)?
''Mgogoro wa EAMWS nimeueleza kwa kirefu katika kitabu cha Abdul Sykes.
Vyombo vilivyohusika katika mgogoro ule kuanzia gazeti la Uhuru na The Nationalist Mkapa akiwa Mhariri, Radio Tanzania Dar es Dalaam Martin Kiama akiwa Mkurugenzi, Polisi Geofrey Sawaya akihusika na Usalama wa Taifa alikuwapo Rashid Kayugwa.
Wote hawa walikuwa wakiamrishwa kutoka juu wengine wameyasema haya kwa kujuta kabla ya kufa kwao.
Hakika ni mkasa wa kusisimua.
Nataka nikupe mfano mmoja.
Kifo cha Abdul Sykes katikati ya mgogoro wa EAMWS maziko yake yalikuwa hayajapata kuonekana Dar es Salaam.
Mazishi yale yalikuwa habari kubwa kutokana na mchango wa Abdul Sykes katika TANU na uhuru wa Tanganyika achilia mbali kuwa yeye ndiye aliyempokea Nyerere Dar es Salaam na kuishinae nyumbani kwake Mtaa wa Stanley na Sikukuu.
Haya hakuna aliyekuwa hayajui haya na hii ndiyo ilikuwa sifa yake kubwa akitambulika kama mwezeshaji wa mambo yote ya TANU na kudai uhuru wa Tanganyika.
Sasa jiulize vipi magazeti ya TANU chama alichounda Abdul yasimwandike inavyostahiki?
Mkapa kama mwandishi bila shaka alijua uzito wa stori iliyokuwa mbele yake na pengine kwa kufahamu uhusiano wa Abdul na Nyerere alimtaka Nyerere mwenyewe amwandikie rafiki yake taazia kwa mkono wake au amhoji (exclusive interview).
Yawezekana kuwa Mkapa aliyataka yote haya kwa Mwalimu na yeye akakataa?
Hapa ndipo panapoumiza kichwa.
Kuamini kuwa Mkapa kwa kutaka kwake tu aliamua kupuuza kifo cha Abdul Sykes huu ni muhali mkubwa sana.
Mwandishi mpumbavu peke yake.ndiye anaeweza kuchagua uamuzi wa kijinga kama huu.
Benjamin Mkapa hakuwa mtu zuzu.
Kama ulivyohitimisha kuwa Allah ni mjuzi wa siri na dhahiri nami nasema hivyo hivyo.
Yapo mengi Mkapa aliyafanya hata alivyokuwa rais lakini kwa hali ya siasa zetu Tanzania, alijikuta mikono yake imefungwa na si kufungwa tu bali imefungwa nyuma ya mgongo wake.
Hapo chini ni taazia ya Abdul Sykes katika Sunday News la 20 October, 1968.
Lakini taazia hii ilileta mgogoro mkubwa ofisi ya TANU New Street.
Kuna baadhi ya viongozi ndani ya TANU walikerwa na taazia hii.
Hapo chini kuna Kumbukumbu ya Abdul Sykes kama zilivyochapwa na magazeti ya Chama na Serikali Uhuru na Daily News ya tarehe 12 Oktoba 1988.
Kumbukumbu hizi nazo zikafikwa na mkasa pia.
Wahariri walitishika na waliyoyasoma wakasema hawatachapa hadi wamepata kibali kutoka Dodoma.
Walipopewa ruhusa ya kuchapa Kumbukumbu ya Abdul Sykes yale yote muhimu katika kumuelewa Abdul Sykes yaliondolewa.''
Naanza na hili la Wamanyema.
Soma hapo chini:
WAMANYEMA WA DAR ES SALAAM KATIKA TANU NA SIASA ZA KUDAI UHURU
Iddi Faiz Mafongo TANU Card No. 24 Iddi Tosiri TANU Card No. 25 Ndugu Wawili Katika Kupigania Uhuru wa Tanganyika, 1954
Wamanyema wanajulikana kama watu wenye harara na ya ushujaa.
Mmanyema anaweza kuulipia fedha ugomvi ili na yeye awemo, na kadri mpinzani anavyokuwa na nguvu na hodari, ndivyo Mmanyema anavyofaidi ugomvi wake.
Katika siku hizo Wamanyema walikuwa wameshikwa katika magomvi.
Katika mwaka wa1941 ilibidi serikali, maimamu na masheikh wa msikiti mingine mjini Dar es Salaam kuingilia kati ili kuamua ugomvi uliowakumba Wamanyema kuhusu msikiti wa Manyema.
Msikiti huu Wamanyema waliujenga mwaka wa 1912.
Wamanyema hawakumstahi mtu yeyote, waligombana hata wenyewe kwa wenyewe.
Hamaki hizi zilipoelekezwa kwa serikali ya kikoloni zilikuja kuwa na manufaa sana.
Kwa kuwa walikuwa ni kabila la Waislam watupu, Wamanyema hawakuweza kufaidika na elimu iliyokuwa ipo mokononi mwa wamishionari.
Hata hivyo Wamanyema walipiga hatua kubwa katika elimu ya dini yao na hii ndiyo sababu kuwa hadi leo utamaduni wa Kiislamu umeenea katika kila familia ya Mmanyema iwe nyumbani Kigoma au huko pwani.
Mmanyema hayupo mbali sana na utamaduni wa Kiislam.
Wamanyema, Warufiji na Wadigo ni katika makabila ambayo ni tabu sana kumpata Mkristo.
Iddi Faiz alikuwa Mmanyema.
Hadhi yake iliongezeka zaidi kwa kuwa alikuwa mweka hazina wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika na TANU.
Vilevile aliifanyia kampeni TANU, akifuatana na Nyerere katika safari za awali za kukitangaza chama, akihutubia mikutano jukwaa moja na Nyerere.
Ilikuwa ni Iddi Faiz na kaka yake Iddi Tosiri ndiyo waliompeleka na kumtambulisha Nyerere kwa binamu yao Sheikh Mohamed Ramia wa Bagamoyo.
Ilikuwa ni baada ya utambulisho huu kwa Sheikh Ramia ndipo urafiki ukajengeka kati ya Sheikh Ramia na Nyerere na ndiyo Nyerere akakubalika Bagamoyo.
Sheikh Ramia akiwa khalifa wa tariqa ya Qadiriya alikuwa na murid wengi waliomfuata katika TANU kama kiongozi wao.
Juu ya hayo alikuwa miongoni mwa wanachuoni walioheshimiwa sana.
Hakuna kilichoweza kusimama na kuota mizizi Bagamoyo bila kupata ridhaa ya Sheikh Mohamed Ramia na hii ilikuwa toka wakati wa TAA.
Akiwa khalifa wa tariqa ya Qadiriya ambayo ilianzishwa na kustawishwa Bagamoya na baba yake, Sheikh Yahya Ramia, mwanzoni mwa karne ya ishirini, nguvu za Sheikh Ramia zilikuwa hazisemeki.
Alichosema sheikh ndicho hicho kilichofuatwa.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba IddI Faiz Mafongo alihudhuria mkutano wa uzinduzi wa TANU katika Ukumbi wa Arnautoglu mwezi Agosti 1954.
Haifahamiki kwa hakika hasa ni lini Iddi Faiz alijiunga na TANU kwa sababu kadi yake ya kwanza ya uanachama ilipotea na akapewa kadi nyingine iliyokuwa na namba 915 iliyotolewa tarehe 28 Agosti, 1954.
Lakini kwa kukisia tu kutokana na kadi ambayo Iddi Faiz mwenyewe aliitoa kwa kaka yake Iddi Tosiri ambayo ilikuwa kadi namba 25 na yenye saini yake kama afisa aliyetoa kadi hiyo, inaweza kuchukuliwa kwa uhakika kuwa Iddi Faiz alikuwa miongoni mwa wale watu wa mwanzo kabisa kuingia TANU na huenda akawa miongoni mwa wanachama ishirini wa mwanzo.
Ukichukua katika fikra ukweli kwamba Ali Mwinyi Tambwe aliyekuwa katibu wa Al Jamiatul Islamiyya aliingizwa TANU na Mtemvu katikati ya mwezi Agosti, 1955, huenda Ali Mwinyi kama katibu wa Al Jamiatul Islamiyya na Idd Faiz akiwa mweka hazina, wote wawili waliingia TANU wakati mmoja.
Iddi Faiz na nduguye Idd Tosiri, muasisi wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika, walikuwa Wakusu, moja ya makabila ya Kimanyema, kwa upande wa baba yao; na Wabwali kwa upande wa mama yao.
Wote wawili walikuwa katika Batetera Union (Congo Association), chama kilichokuwa kikiwaunganisha Wamanyema wa Tanganyika.
Mzee bin Sudi alikuwa rais muasisi wa chama hicho na baada ya kifo chake Sheikh Hussein Juma alichaguliwa kushika nafasi hiyo.
Batetera Union (Congo Association) kilikuwa chama kilichoshikamana na chenye nguvu sana miongoni mwa vyama vya kikabila vilivyokuwapo wakati wa ukoloni.
Wamanyema ni kabila la Waislam watupu na kwa sababu hii hakukuwa na pingamizi katika kuunga mkono TANU.
Batetera Union kilikuwa na nguvu sana kiuchumi kwa kuwa kilikuwa katika wafuasi wake, watu waliomiliki majumba na walihodhi takriban nusu ya nyumba zilizojengwa mjini Dar es Salaam kati ya vita kuu mbili za dunia.
Uwezo huu wa kiuchumu uliwafanya Wamanyema kuwa wapinzani wagumu wa serikali ya kikoloni na uliwanyanyua hadi kufikia kuwa mbele katika siasa mjini Dar es Salaam na katika miji mingine ya Tanganyika.
Umoja wa Wamanyema ndiyo uliojenga msikiti maarufu wa Wamanyema mwaka wa uliokuwa karibu na makao makuu ya African Association.
Mzee bin Sudi alikuwa rais muasisi wa chama hicho na baada ya kifo chake Sheikh Hussein Juma alichaguliwa kushika nafasi hiyo.
Mzee bin Sudi alikuwa pia ni muasisi wa African Association mwaka wa 1929 pamoja na Kleist Sykes.
Batetera Union kilikuwa chama kilichoshikamana na chenye nguvu sana miongoni mwa vyama vya kikabila.
Wamanyema ni kabila la Waislam watupu na kwa sababu hii hakukuwa na pingamizi katika kuunga mkono TANU.
Batetera Union kilikuwa na nguvu sana kiuchumi kwa kuwa kilikuwa katika wafuasi wake, watu waliomiliki majumba na walihodhi takriban nusu ya nyumba zilizojengwa mjini Dar es Salaam kati ya vita kuu mbili za dunia.
Uwezo huu wa kiuchumu uliwafanya Wamanyema kuwa wapinzani wagumu wa serikali ya kikoloni na uliwanyanyua hadi kufikia kuwa mbele katika siasa mjini Dar es Salaam na katika miji mingine ya Tanganyika.
Umoja wa Wamanyema ndiyo uliojenga msikiti maarufu wa Wamanyema mwaka wa 1912 uliokuwa karibu na makao makuu ya African Association.
Kubwa ambalo Iddi Faizi alifanya ni kule kuwa mratibu wa safari ya kwanza ya Julius Nyerere UNO mwaka wa 1955.
Iddi Faizi ndiye aliyekuwa musanyaji wa fedha za safari hii na kama Mweka Hazina wa Al Jamiatul Islamiyya alitoa fedha za jumuiya hiyo na kuzitia katika mfuko wa safari ya Nyerere UNO.
Picha: Iddi Faizi Mafongo Aliyevaa Kanzu Koti na Tarabush Uwanja wa Ndege Dar es Salaam Akimsindikiza Nyerere Kwenda New York, UNO 1955 wengine kuanzia kushoto ni Rashid Sisso, Robert Makange, Iddi Faizi Mfongo Julius Nyerere, John Rupia na Bi. Titi Mohamed
Habari zaidi za Iddi Faiz Mafungo ingia hapa:
http://www.mohammedsaid.com/2014/02/idd-faiz-mafongo-mweka-hazina-wa-safari.html
Sasa tuje katika Maulid ya Mfungo Sita ya mwaka wa 1963.
Kleist Sykes alikuwa katika Maulid Committee kuanzia mwaka wa 1926 hadi 1940.
Kleist Sykes na baadhi ya Wazulu, Wamanyema na Wanubi walijitoa katika kamati hii kwa hoja kuwa watashughulika na shule ya Al Jamiatul Islamiyya.
Hiki ni kisa kirefu hatuwezi kuyaongea yote hapa.
Mwaka wa 1963 Mwenyekiti wa Maulid Committee alikuwa Sheikh Abdallah Iddi Chaurembo aliyepata kuwa mwanafunzi wa Sheikh Hassan bin Ameir.
Hayo hapo chini ndiyo yaliyokuwapo wakati ule:
''Wakazi wa Dar es Salaam kila mwaka walikuwa wakifanya maulidi katika viwanja vya Mnazi Mmoja kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW).
Huu ndiyo toka asili ulikuwa uwanja ambao TANU ilifanya mikutano yake yote wakati wa kupigani uhuru.
Mwezi Juni 1968 maulidi mbili katika usiku mmoja zilisomwa kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume (SAW). Maulidi moja ilisomwa Mnazi Mmoja na nyingine Ilala.
Chanzo cha haya yote ni kuwepo kwa kutoelewana kati ya viongozi wa Waislam waliokuwa wanajiona kuwa ni wazalendo wafuasi wa TANU na wale viongozi wa EAMWS ambao kambi nyingine ilikuwa ikiwaona kama wapinzani wa TANU.
Yale maulidi yaliyosomwa Ilala yalihudhuriwa na viongozi wa EAMWS na yalipata watu wengi na yakafana sana ukilinganisha na yale maulidi ya Mnazi Mmoja, ya wafuasi wa TANU.
Uongozi wa TANU ulitishika na hali hii iliyokuwa ikijitokeza kwa maana ilikuwa inaonyesha kuwa chama kilikuwa kinapoteza wafuasi ambao walikuwa wakijiunga na kambi ya Tewa na Titi iliyokuwa ikisemekana ipo dhidi ya Nyerere. ''
Baada ya maulid haya haikupita miezi mitatu mgogoro wa EAMWS ukazuka na baada ya miezi mitatu serikali ikaivunja EAMWS kuunda BAKWATA.
Ninachojaribu kueleza ni kuwa historia hii si ya kufanyia utani na maskhara kama unavyofanya hapa ni kitu muhimu sana na nyeti kwa kuelewa mengi katika historia ya Waislam, TANU na uhuru wa Tanganyika.
Ndiyo maana unaona kitabu cha Abdul Sykes kimekamata fikra ya kila aliyekisoma na mwandishi bila kutegemea amejikuta yupo katika dunia ambayo hakutegemea kama angeingia na kuishi humo.