Sio mara zote mahakama inatoa amri ya kukamatwa kwa shahidi aliyepelekewa wito wa mahakama na asifike
Utasikia katika kesi kadhaa zenye mazingira kama hayo upande unaohusiana na shahidi aliyeitwa unasema ama shahidi hapatikani au shahidi hajafika na hatuna taarifa naye na mahakama inaendelea na usikilizaji kesi
Hii hutokea sana kwa upande wa mashahidi wa upande wa mashtaka hasa kwa wale mashahidi ambao ushahidi wao hauna uzito mkubwa na hauwezi kuathiri kesi ya upande wao
Kwenye kesi nzito kama za mauaji, dawa za kulevya, utakatishaji pesa na hii ya uhaini mashahidi muhimu wa upande wa mashitaka hutafutwa na hulindwa hasa kesi inaporibia kuzungumzwa
Changamoto katika sheria zetu ni kwamba kwenye kesi za jinai hasa zile ambazo hazina dhamana pande mbili zinazopambana haziingii mahakamani zikiwa na faida(advantage) sawa
Upande wa mashitaka unakua na faida lukuki
Kwa mfano kwa mshitakiwa ambaye hana dhamana na yupo mahabusu bado anabebeshwa mzigo wa kuwatafuta mashahidi wake ajue mwenyewe watakutana vipi kuongea mipango ya kesi yao pamoja na ugumu wa kuonana na watu akiwa gerezani japokua summons inaandikwa na mahakama
Lakini pia kutokana na mazingira na masharti ya jeshi la magereza inakua vigumu kwa mshitakiwa hasa kama anajitetea mwenyewe kupata muda wa kuonana na shahidi wake na kumtayarisha kama wafanyavyo upande wa mashitaka
Hata pale asubuhi mshitakiwa anapopelekwa mahakamani na kabda Jaji/Majaji/Hakimu hajaingia na kesi kuanza bado mshitakiwa hapatiwi fursa ya kumtayarisha shahidi wake kwa viwango vinavyotakiwa
Wakati mwingine wala sio sheria ila ni kama utaratibu tu waliojiwekea jeshi la magereza kutoruhusu mtu kuongea kwa nafasi ya kutosha na mshitakiwa wakati akiwa mahakamani
Kwa ujumla sheria, kanuni, taratibu na miongozo mingi kuhusiana na haki jinai zinabidi kufumuliwa na kutengenezwa upya kama ilivyoshauriwa katika mapendekezo ya tume kadhaa ikiwemo ya hivi karibuni ya Jaji Chande