Mimi ni kati ya watu ambao siyo mshabiki sana wa Nyerere. Nilianza shule wakti Tanzania ndiyo mwanzo imepata uhuru. Maisha ya Tanganyika/Tanzania kwa kweli yalikuwa duni sana. Wakati Tanganyika tunapata uhuru hali yetu ya kiuchumi haikuwa tofauti sana na ile nchi za South East Asia – Malaysia, Singapaore, Thailand, etc. Leo tumeachwa mbali sana.
Nyerere alikuwa na tatizo kubwa na kudhani kuwa wengine hawajui kitu. Kila kitu anajua yeye na ukimbishia basi wewe ni adui yake wa maisha. Hawezi kukusamehe kabisa. Hakuwa mtu anayependa kuonea watu lakini alipenda sana kulipiza kisasi. Mifano ipo mingi. Akina Tuntemeke Sanga ambaye aliambiwa asitembee nje ya wilaya ya Njombe, Oscar Kambona alimpa baba yake (an Anglican Pastor) gari la Landrover. Oscar alipokimbilia UK yule mzee aliambiwa lile gari lisitembee hata nchi moja. Liliozea lilopoegeshwa.
Katika Africa yeye alijipatia sifa nyingi katika kuongoza vita za kulikomboa bara hili. Wazungu wengi hawakupenda siasa yake ya ujamaa wakidhani kuwa itaenea bara zima. Lakini katika Afrika Nyerere vilevile aliwahi kufanya vitendo ambavyo alikuja kuvijutia baadaye kama kuunga mkono kwa kujitenga jimbo la Biafra kule Nigeria. Tulipeleka pesa nyingi na inawezekana hata ushauri wa kivita.
Mafanikio ya Nyerere kwenye uchumi wa Tanzania ni sifuri, au tuseme "negative". Watanzania tulipata shida sana asana. Kwa wale ambao hawakuwepo wakati huo wasiombee maisha kama yale yawafike. Ilifika wakati ilibidi sukari, sabuni ya mbuni, mchele, unga wa mhogo(makopa), betri, viberiti,n.k vyote vilipatikana kwa mjumbe wa nyumba kumi. Kuwa nyumba kumi wakati huo ulikuwa umeukata. Wakati Nyerere anaachia ngazi pale Benki kuu walikuwa na dola laki tano tu. Walishindwa kununua mafuta na nchi nzima magari yalisimama. Wakati huo magari hayakuwa mengi kwani watu hawakuwa wanruhusiwa kuwa na magari na wale waliokuwa nayo walikuwa hawaruhusiwi kuendesha Jumapili kuanzia saa nane mchana.
Kuhusu "villagilisation" Nyerere hawezi kukwepa lawama. Tamaa ya Nyerere ilikuwa ni kuweka watu pamoja na kudhani watabadilika kuwa wajamaa. Kwa vile alizungukwa na wapamabe tu kama akina Kawawa, Songambele, etc. basi walifanya chochote kumfurahisha. Nakumbuka kijijini kwangu kuna mzee wa zaidi wa miaka 60 alihamishiwa umbali wa chini ya kilomita moja kutoka kwenye nyumba yake wakati nyumba zake zote alikuwa ameezeka bati na ikabidi ajenge vibanda vya miti na kueezeka majani. Nyumba zake za zamani walichoma moto kwa vile alikuwa hataki kuhama. Alikufa katika hali ya umasikini sana. Kule Tabora kuna watu wanaitwa Mgaya kumkumbuka mkuu wa mkoa wa wakati huo Philemon Mgaya ambaye alikuwa kinara wa kuchoma nyumba zao moto na wengi waliliwa na samba.
Kuna mtu anazungumzia kuwa wakati wa Nyerere hakuna " intelletuals" waliosomeshwa. Hiyo siyo kweli. Nitataja mmoja ambaye ndiye mtu mweusi wa kwanza kupendekezwa kupewa tuzo la Nobel kwenye Science, Dr. Hezekeiah Kamuzora ambaye alikuwa anafanya kazi kama Biochemist pale Muhimbili. Hata hivyo kielime Tanzania tulididimia sana wakati wenzetu walikuwa wanendelea. Mpaka miaka ya 80 Nyerere alikuwa hataki Watanzania wengi waingie kwenye elimu ya sekondari wakati majirani zetu walikuwa wanapanua elimu ya vyuo vikuu. Kwa mfano, alipinga sana mikakati ya kujenga shule za sekondari za tarafa kule wilayani Njombe ambazo zilijulikana kama NDDT akisema kuwa badala yake wajenge "vocational colleges"