Nyerere na Wanafunzi wa Chuo Kikuu waliopinga kwenda JKT.

Nyerere na Wanafunzi wa Chuo Kikuu waliopinga kwenda JKT.

Lycaon pictus

JF-Expert Member
Joined
Jan 31, 2021
Posts
9,189
Reaction score
16,128
Hotuba hii ilitolewa kama kijitabu TANZANIA ITAJENGWA NA WENYE MOYO. Unaweza kukisoma bure ndani ya app ya Maktaba Sauti. Inapatikana playstore.

Tanzania Itajengwa.jpg

Oktoba 23, 1966.

Wananchi,

Jana tumefukuza wanafunzi wapatao 393 kutoka katika vyuo mbali mbali vya Dar es Salaam baada ya maandamano yao ya kupinga mpango wa Serikali wa National Service. Tumeamua vijana hao, waliokuja mpaka Ikulu wakipinga mpango wa National Service, na kusema maneno machafu- machafu, waondoke warudi majumbani kwao.

Wanafunzi gani.

Kwanza nataka kuwaambieni, wananchi, kwamba wanafunzi hao wametoka katika vyuo mbali mbali, na majina ya vyuo hivyo yametangazwa. Baadhi yao wametoka katika Chuo Kikuu pale mlimani, wengine wametoka katika Chuo kile cha Ufundi hapo nyuma yenu, wengine wametoka katika Chuo cha Madaktari kule Mhimbili, na wengine wametoka katika Chuo cha Waalimu, kule Chang'ombe. Vile vile kuna waliotoka katika Chuo cha Biashara hapo nyuma ya Chuo cha Ufundi na wachache wametoka katika shule za sekondari. Lakini walio wengi, zaidi ya nusu ya wote wale waliokuja Ikulu, na ndio tuliowaambia warudi majumbani kwao, wametoka katika Chuo Kikuu kule mlimani.

Walio wengi walikataa.

Nataka kueleza pia kwamba katika Chuo Kikuu wamebaki vijana wengine wa Kitanzania waliokataa kuwaunga mkono wenzao katika maandamano yale. Walio wengi walikataa. Katika chuo hiki hapa cha ufundi, walio wengi walikataa. Katika chuo cha waalimu cha Chang'ombe walio wengi walikataa. Katika vyuo hivyo vingine vyote nilivyovitaja, walio wengi walikataa. Nataka kuwapa pongezi vijana hao wa vyuo hivyo vyote ambao najua walishawishiwa na wenzao kwa kukataa kuingizwa katika maandamano ya kupinga National Service. Pia nawapa pongezi vijana wa shule za sekondari wote, sio wa hapa Dar es Salaam tu bali na wa shule za sekondari za Tanzania nzima kwa kukataa kuingia katika jambo hili baya. Wengine nimesema nao mimi mwenyewe, na wengine wamehutubiwa na wenzangu Mawaziri, nao hawakubali upuuzi huu ambao umekaa miezi mingi sana katika Chuo chetu Kikuu. Jana upuuzi ule ukadhihirika uwanjani kule Ikulu.



Maana ya "National Service".


Vijana walikuja Ikulu kuja kupinga mpango wa National Service. Wananchi sasa nataka kuwaelezeni kwa utaratibu kadiri nitakavyoweza maana ya National Service. National Service maana yake nini? Najua wote vijana mliofanya maandamano haya ya leo ya kuniunga mkono, na vijana wengine kadhalika, mnaelewa maana ya National Service na mkapinga fikara za kuikataa—ndiyo maana muko hapa. Mnapinga upuuzi ule wa jana. Lakini hata hivyo nataka kuwaelezeni ninyi na nchi nzima, National Service maana yake nini.

Wananchi National Service hatukuanzisha sisi. Mataifa mengi duniani yana National Service. Taifa linawaambia vijana wake: Tunataka vijana mlitumikie Taifa lenu. Taifa linadai utumishi toka kwa vijana. Linadai huduma kwa vijana. Na vijana wanaitika. Taifa linawadai huduma vijana na vijana wanaitika wito huo kwenda kulihudumia Taifa, kwa kazi yo yote ambayo Taifa linahitaji ifanywe. Narudia nikisema mipango kama hiyo hatukuanza sisi. Mataifa mengi duniani yana National Service.

Kwa desturi "National Service" au huduma wanayoitiwa vijana hawa wa mataifa haya mengine duniani, ni huduma ya kivita. Wanaitwa vijana wafundishwe kwa kazi ya kivita. Ikiwa kesho na kesho kutwa hapana budi basi waende wakapigane, waue au wauawe—hiyo ndiyo National Service ya kawaida katika mataifa mengine duniani. Na wanapoitwa jinsi hiyo wakaingia katika National Service, vijana hao wote wanafanywa ni sawa sawa. Atakuja mwingine labda ametolewa katika ualimu, mwingine labda alikuwa fundi chuma, mwingine labda ni daktari. Huyu udaktari wake kasomea miaka saba, yule ualimu wake akasomea miaka mitatu, na kadhalika, lakini wote hao watakapoingia katika kundi lile la National Service, wakishafika pale basi wote sawa. Wote wanakuwa ni askari wa kawaida, hakuna mmoja anayehesabiwa digrii, la; japokuwa aingie na digrii ishirini. Ukisha fika pale wewe, na mwingine wote ni praivet, yaani ni askari wa chini kabisa. Pengine unaweza ukaambiwa wewe ni mwalimu, kazi ako utafundisha, lakini utafundisha kama praivet, askari wa chini kabisa. Pengine wewe ni daktari ukaambiwa adhali umesomea udaktari, sasa kazi yako hapa jeshini itakuwa kutibu askari, lakini utatibu kama praivet, askari wa chini kabisa. Kama umepata bahati ya kumzidi mwenzio, ni kwa sababu katika hali yako ya u-National Service umefanywa koplo. Hapo utamzidi mwenzio. Ukifanywa sajin ndiyo kabisa. Lakini kama wewe si koplo, wala si sajin, wala si meja, hata ungekuwa na digrii thelathini, wewe ni praivet tu, na hali yako pale ni ya ki-praivet tu, askari wa chini kabisa. Ndiyo kawaida ya National Service.



National Service yetu.

Na sisi wananchi, tumeanzisha National Service hapa. Tunayo National Service; vijana wale mnawaona pale, ni vijana wa National Service. Tofauti ya kweli baina ya National Service yetu na zingine ni nini. Kwanza, ya kwetu si ya kivita; ni ya ujenzi. Tumewaita vijana waingie katika National Service, na kazi tutakayowapa ni ya ujenzi katika nchi. Wamekwisha anza na tunao, wengine karibu watamaliza miaka yao miwili. Tunawafanyaje mle katika National Service? Wanatumika sawasawa. Wameingia katika National Service mle, wote wamehesabiwa kuwa sawasawa. Kila mmoja anapata posho Sh. 20/- kwa mwezi na tumekuwa tukiwapa hivyo tangu wameanza, siyo kwamba tutakuja kuanza baadaye. Tumekwisha fanya hivyo kwa miaka miwili yote waliomo katika National Service. Lakini hapo walipo katika National Service wanapitana. Wachache ni "leader", yaani viongozi, na wengine ni National Service tu, bila jina la zaidi. Lakini wote wale ni National Service na waulizeni wenyewe kama katika kupitana huko kuna apataye zaidi; mimi sijui.

Nilikuwa pale Ruvu juzi nikiwakagua vijana wale wa kike na wa kiume, wanaomaliza miaka yao miwili. Wengine wananiuliza, "Mwalimu iko ruhusa tukimaliza miaka miwili turudie tena?" Hao wanafanya kazi yao ya National Service ya kawaida. Halafu tangu mwaka juzi, mara tu baada ya maasi yale ya askari, ikawa tumepitisha vijana wetu katika National Service, ndiyo wakachaguliwa kutoka katika National Service kuingia katika jeshi la ulinzi.

Jeshi la ulinzi hili la sasa ni la wananchi wa Tanzania. Wamo mle vijana wa National Service. Baadhi ya wale vijana wenu waliomo katika jeshi la ulinzi ni vijana wa National Service. Wengine karibu watamaliza miaka yao miwili. Kule tunawafanya wote sawa.

Hawapati mishahara.

Ijapokuwa kule kuna mishahara-shahara, praivet mshahara fulani, koplo mshahara fulani, sajin mshahara fulani, lakini tangu tangu tumeanza mpango huu mpya, wao wanapata 40 kwa mia tu ya mshahara ule. Hatuwatofautishi hawa kwa namna yo yote, madhali ni vijana wa National Service.

Vijana wenye elimu hawaji.

Lakini tuliona kwamba vijana waliokwisha kuingia katika National Service hivi sasa ni vijana ambao, au wana elimu ndogo, au hawakusoma kabisa, au hawana kazi, au hawakusomea kazi yo yote. Hao ndio wanaoingia katika National Service. Na National Service ni kazi ya vijana, ni mahali pa vijana kwenda kutumikia Taifa. Tukaona vijana wenye elimu hawaji. Waliosomea kazi maalum hawaji. Mwenye kitumbua na kazi yake mahali, haji. Tukaona kuwa jambo hili lina kasoro. Vipi waliokwisha tumikiwa vizuri sana na Taifa wao ndio hawaji kulihudumia Taifa katika National Service, ila wale ambao hawakugharimiwa na Taifa wao ndio wanakuja? Tuligundua kwamba mpango huu una walakini.

Mpango una walakini.

Kwa hiyo tukaanza kutafuta njia ya kuwaleta wenye elimu na wenye kazi, nao waje wakalihudumie Taifa. Tukaamua kupitisha sheria, kwamba kijana ye yote anayetoka akimaliza masomo yake katika shule hizi kubwa, au akishamaliza kusomea kazi yo yote, kabla hajaanza kazi yake kwanza atumike katika National Service. Tukasema, tutawatumikishaje hao vijana waliosoma? Tukasema tutafanya hivi, kwamba tutaugawa muda wao vijana hawa wa kuwa katika National Service. National Service yenyewe ni miezi ishirini na minne, yaani miaka miwili. Lakini tutaugawa muda huo katika sehemu mbili; miezi sita kijana atakuwa yumo katika kambi, pamoja na wenzake wote. Kama ni mwalimu, au ni daktari, au ni fundi wa aina yo yote, atakuwa katika kambi katika muda wa miezi sita pamoja na wenzake wengine wote. Anapata posho ya shilingi ishirini kwa mwezi. Halafu akishamaliza yale mafunzo yake ya miezi sita ya kambini atakwenda kufanya kazi yake ya kawaida kwa muda wa miezi kumi na minane iliyobaki. Kama ni mwalimu, atakwenda darasani kufundisha; kama ni fundi wa aina nyingine yo yote, atakwenda kufanya kazi yake; nasi tutaukubali ule udaktari, au ualimu wake kuwa kama ni kazi ya National Service. Tutahesabu ile miezi yake kumi na minane pale Muhimbili kwamba ile ni National Service. Ikiwa yuko Muhimbili anatibu sawa sawa kama daktari mwingine tutahesabu ile kazi yake katika muda wa miezi kumi na minane ya kuwa ni National Service.

Posho yao.

Tukasema, posho je! Muda ule wa miezi sita ya kwanza anapokua kambini atapata posho ya kawaida. Lakini atakapokuwa anafundisha darasani mtu huyu, posho yake iweje? Tukasema kama yuko darasani anafundisha, au ni daktari katika hospitali, au yuko mahala pengine tutampa posho yake namna hii. Kwanza tutampa kima cha chini cha mtumishi wa Serikali Dar es Salaam ambazo ni shilingi mia moja na themanini kwa mwezi, hizo tutazichukua tutaziweka kando, kuwa fungu lake la kwanza. Sh. 180/- ana hakika atazipata. Halafu mathalani kama ni mwalimu, tunajua mshahara wa mwalimu asiyekuwa National Service. Katika mshahara huo tunazitoa zile Sh. 180/-. Tukishaziondoa zile Sh. 180/- zile zilizobaki tunampa 40 kwa mia.

Kwa mfano. Mwalimu atakayemaliza masomo yake pale Chuo Kikuu, na ambaye siyo National Service, kwa kawaida ni shilingi 1,320/- kwa mwezi. Sasa akienda katika National Service tutampa nini? Kwanza kabisa tutampa Sh. 180/-. Halafu zile tunazitoa katika shilingi 1,320/-. Katika zile zinazobaki Sh.1, 140/-, tunampa 40 kwa mia yake, ambazo ni Sh. 456/-. Kwa hiyo, anapata kwanza 180/- halafu 456/-. Ukijumlisha utaona anapata 636/-, hii ndiyo posho yake atakapokuwa anatumika katika National Service.

Lakini haijatosha, haiishii hapo hapo tu. Tunampa kwanza Sh. 636/-, posho, mwalimu aliyemo katika National Service; halafu tunampa nyongeza ya kodi ya nyumba, ambayo itafika kiasi cha Sh. 132/-. Halafu tunampa nguo za National Service, wanasema hii ni kiasi cha Sh. 26/- kwa mwezi. Kwa hiyo kwa jumla mwalimu huyo anapata Sh. 794/-. Na hiyo ni posho ya kijana wa National Service kila mwezi. Tuseme Sh. 790/-.

Nataka muelewe wananchi, nataka muelewe nini wasilolitaka vijana hawa! Huyu analihudumia Taifa anapewa Sh. 790/- posho tu, na bado haijatosha; wananchi, bado haijatosha! Katika hizo Sh. 790/- anazopata hatumkati hata senti moja ya kodi, hatumkati kodi ila kama amenunua bia, maana katika kila chupa ya bia kuna kodi ya Serikali. Lakini bila hivyo Sh. 790/- za posho ya kijana wa National Service hizi haziguswi; ni posho siyo mshahara. Siyo mshahara maana siku hizi Tanzania kwa waheshimiwa kama wale, hakuna mishahara midogo ya namna hiyo? Hakuna!

Wananchi, hivyo ndiyo National Service tunayoisema, ambayo waheshimiwa hawa wanaikataa. Kijana atakwenda kambini miezi sita pamoja na wenzake. Atatoka pale atakwenda darasani au hospitali kwenda kufanya kazi yake. Kama ni mwalimu nasema atakuwa anapata kiasi cha Sh. 800/-, posho, hazikatwi kodi hizo. Hiyo na ule ualimu wake au uganga wake ndiyo tutakaoupokea, kwamba ndiyo huduma anayohudumia Taifa. Hatumpeleki vitani au kumwambia akachimbe mfereji—atafanya kazi yake ile ile aliyoisomea. Wala hatutamchukua huyu kijana kabla hajamaliza masomo yake. Tulisema tuache kwanza amalize masomo yake. Tungeweza tukamchukua kwanza akamaliza National Service yake halafu ndiyo akaenda kule kumaliza masomo yake, lakini tukasema hapana, tusimkatishe masomo yake. Acha asome amalize, halafu ndiyo akafanye National Service. . . . . . . . .
 
Hoja ya wanafunzi ilikuwa na mantiki kubwa, kwamba mbona vigogo wa serikali na wanasiasa wanalipwa mishahara minono na marupurupu makubwa?

Wanafunzi wa siku hizi ni wajinga sana kwenye mwamvuli wa uzalendo. HESLB inawalipia 230K kama ada kwenye ada ya 2M hii ni kwa mujibu wa Allocation ya wanafunzi wengi wa mwaka jana. Mnashindwa kupambania mpate angalau asilimia 50 ya ada?
 
Hoja ya wanafunzi ilikuwa na mantiki kubwa, kwamba mbona vigogo wa serikali na wanasiasa wanalipwa mishahara minono na marupurupu makubwa?

Wanafunzi wa siku hizi ni wajinga sana kwenye mwamvuli wa uzalendo. HESLB inawalipia 230K kama ada kwenye ada ya 2M hii ni kwa mujibu wa Allocation ya wanafunzi wengi wa mwaka jana. Mnashindwa kupambania mpate angalau asilimia 50 ya ada?
Elimu ya Chuo Kikuu ilipaswa kuwa bure. Hili Serikali inaweza ila haitaki tu!
 
Hoja ya wanafunzi ilikuwa na mantiki kubwa, kwamba mbona vigogo wa serikali na wanasiasa wanalipwa mishahara minono na marupurupu makubwa?

Wanafunzi wa siku hizi ni wajinga sana kwenye mwamvuli wa uzalendo. HESLB inawalipia 230K kama ada kwenye ada ya 2M hii ni kwa mujibu wa Allocation ya wanafunzi wengi wa mwaka jana. Mnashindwa kupambania mpate angalau asilimia 50 ya ada?
Nyerere aliwajibu kwa kuanza kupunguza mshahara wake yeye mwenyewe na kupunguza mishahara ya mawaziri wake.

Tumetoka siku ambazo rais alichukua muda wake kuwaelezea wananchi mambo kwa kina, mpaka leo hata tukijibiwa tunajibiwa "kifo ni kifo tu".
 
HESLB inawalipia 230K kama ada kwenye ada ya 2M hii ni kwa mujibu wa Allocation ya wanafunzi wengi wa mwaka jana. Mnashindwa kupambania mpate angalau asilimia 50 ya ada?
Kuna dogo analia tu kalipa hio 230 na ada haitoshi imebaki 330 na bado wanataka alipe bima na ushenzi mwingine
 
Nyerere aliwajibu kwa kuanza kupunguza mshahara wake yeye mwenyewe na kupunguza mishahara ya mawaziri wake.

Tumetoka siku ambazo rais alichukua muda wake kuwaelezea wananchi mambo kwa kina, mpaka leo hata tukijibiwa tunajibiwa "kifo ni kifo tu".
Ndio maana nimeshangaa hapa jirani leo wamepika kuku pilau nikauliza kulikoni kwani Christmas imefika nikaambiwa kwani we haujui? Nikauliza kuna nini jirani? Wakaniambia wabunge wamepata ajali huko wakiwa wanaelekea Kenya sasa nikamwambia Mama watoto andaa pilau tule na yule Jogoo mkubwa nikamwita Ostadh Rajabu amchinje ili kusherehekea kidogo, nikashangaa kumbe ndipo tulipofika hapa kwamba sasa wakifa baadala ya kulia tunapika pilau aaha
 
Ndio maana nimeshangaa hapa jirani leo wamepika kuku pilau nikauliza kulikoni kwani Christmas imefika nikaambiwa kwani we haujui? Nikauliza kuna nini jirani? Wakaniambia wabunge wamepata ajali huko wakiwa wanaelekea Kenya sasa nikamwambia Mama watoto andaa pilau tule na yule Jogoo mkubwa nikamwita Ostadh Rajabu amchinje ili kusherehekea kidogo, nikashangaa kumbe ndipo tulipofika hapa kwamba sasa wakifa baadala ya kulia tunapika pilau aaha
Wajerumani wanaita "Schadenfreude".

Kifurahia matatizo ya wengine.
 
Hoja ya wanafunzi ilikuwa na mantiki kubwa, kwamba mbona vigogo wa serikali na wanasiasa wanalipwa mishahara minono na marupurupu makubwa?

Wanafunzi wa siku hizi ni wajinga sana kwenye mwamvuli wa uzalendo. HESLB inawalipia 230K kama ada kwenye ada ya 2M hii ni kwa mujibu wa Allocation ya wanafunzi wengi wa mwaka jana. Mnashindwa kupambania mpate angalau asilimia 50 ya ada?
Huko mbele utaona kuwa hiyo hoja aliikubali na kwa kuanza alipunguza buku kwenye mshahara wake. Kutoka 5,000 kuwa 4,000 kwa mwezi.
 
Hawataki. Kwanza, wengi ni vihiyo aka vilaza. Pili, wakiwa na wasomi wengi watawatabisha. Tatu, watashindana na watoto wao. Nne, watawaaibisha kwa kusoma kwa nguvu kuliko wao wanaoshobokea shahada za heshima wakati wengi wao hawana heshima yoyote zaidi ya kuzinunua.
 
Kuna dogo analia tu kalipa hio 230 na ada haitoshi imebaki 330 na bado wanataka alipe bima na ushenzi mwingine
Mambo ya hovyo sana yanaendelea huko HESLB. Pesa zinazoingia kwenye mfuko wanaishia kuandaa semina ili kujifaidisha wao
 
Anaendelea kusema Mwalimu.

Hawataki, wanadai haki yao.

Kumbe tumejipalia makaa ya moto. Wanapinga. Vijana wa Chuo Kikuu, wenye elimu, wanapinga; hawataki waheshimiwa hawa. Hawataki nini? Kwanza, hawataki kukaa katika kambi. Waheshimiwa hawa wanasema, mnataka kutufunza "discipline". Nani anasema hatuna "discipline". Sisi tunayo "discipline". Vijana wanasema, hawataki kwenda kambini. Pili wanataka wapate mapesa yao, wanasema yao! Wapate mapesa yao! Vijana wa Chuo Kikuu wanadai wakisema, tupate haki yetu. Haki yetu! Wanadai haki yao waheshimiwa hawa!



Nitawasomeeni barua yao. Niwieni radhi, nitawasomeeni wanavyosema, maana mimi sipendi kuwasingizia. Lakini kwa bahati mbaya wameeleza Kiingereza; barua yenyewe imeandikwa Kiingereza.

"Ultimatum on National Service"

Wananchi msioelewa, "Ultimatum" ni neno unalompa la mwisho mtu unayegombana naye. Unamwambia tenda usipotenda utakiona cha mtema kuni. Ndiyo maana ya neno hilo "Ultimatum". Nchi hutoleana “ultimatum”wakati kabla ya vita. Nchi moja huiambia nchi nyingine, “Ikiwa saa fulani kama hukukubali masharti haya, tutaanza vita." Ni onyo la mwisho kabla ya shari. Vijana walituletea jana hiyo kauli ya mwisho ya shari! Inasema hivi:-

"We, students of the National Union of Tanzania Students, Tanzania University Students Organization, (Dar Unit), Dar es Salaam Teachers College, Muhimbili Medical School, the Technical College Students Union, College of Business Education, Students Association, Aga Khan's, Pupils' Own Council, Azania Secondary School, Jangwani Girls Secondary School, and other educational institutions in Dar es Salaam and up-country issue this serious ultimatum to the Government through the Office of the 2nd Vice-President that we reject the way this major and controversial issue of national importance was mishandled in public and in the National Assembly. In public, the V.P. and other leaders have distorted the information as regard our grievances. As students, we strongly condemn the following points: 'The exploitation of a small group unestablished and new to life which has been maintained by the Government policy in the terms of reference of 60 per cent reduction contained in Government White Paper'.”

Labda ningetafsiri kidogo hayo. Wanalaani kitendo hiki, nia hii ya Serikali ya kunyonya kikundi cha wachache- Serikali ina nia ya kunyonya kikundi hiki cha wachache hawa ambao hata hawajaanza maisha.

"We feel that the President, the Ministers, M.P.s and the top civil servants are determined to throw the burden of financing this expensive scheme on the shoulders of young and helpless students."



Maneno haya yameandikwa na vijana hawa?

"We believe that our grief-stricken cry that we give today will affect the future generation with the same intensity. Therefore, the compromise is either we be paid our full right of earning. . .”-

Wanasema sasa mpango uwe hivi, au tulipwe, kila kitu, haki yetu yote.

“. . . either we be paid our full right of earning or else all those in the high income bracket should also be in our category which then could be interpreted as a sacrifice rather than a form of exploitation.”

Nitajitahidi nitaeleza vizuri: maneno hayo ni kusema au tupewe haki yetu kamili, au watu wote hawa wenye mishahara mikubwa huko juu na wao vilevile wakatwe, ili kusudi wote tujitolee isiwe ni kundi dogo tu.

Hayo maneno ya mwisho hayo wanayoyasema, siyachukii. Maneno hayo ya mishahara ya juu, mimi siyachukii. Ya pili, jambo la pili, “discipline". Sina haja ya kusoma hiyo. Hiyo "discipline" wanasema kwani shule hizo zote hazifundishi "discipline"? Halafu wanatuambia mwishoni kabisa:

"The curriculum of the subject taught during the National Service shows the Government hunger of indoctrination. In one breath we said, time for indoctrination has passed!"

Wanasema, muhtasari wa mafundisho ya National Service unaonyesha kwamba nia ya Serikali ni kwenda kutupakia, kutufundisha "indoctrination". Na mimi nakubaliana na watoto hawa. Wanasema wakati wa uchochezi, wa watu kupakiwa maneno yasiyokuwa na maana, wakati ule umekwisha. Na mimi nakubali, wakati umekwisha.

Wanasema jambo jingine. Wanasema; demokrasi gani hii, wabunge wametishwa-tishwa wakati wa kujadili jambo hili la National Service. Kwanza wamelipitisha haraka haraka. Halafu wabunge wametishwa. Wabunge wamenung'unika, wanasema:—

"And M.P.s have complained of threat and intimidation from among the members of Government."

Kwamba Wabunge, katika kulizungumza jambo hili, wametishwa na wakubwa wa Serikali ndiyo maana Wabunge wakalipitisha lile jambo. Mimi sijapata kusikia kundi la watu wetu wanatukana Bunge kama hivi. Eti Wabunge walipitisha jambo lile kwa kutishwatishwa na wakubwa wa Serikali, kwamba msipofanya msipopitisha hivi mtakiona cha mtema kuni. Halafu wabunge wananchi, wakaenda kwa wanafunzi wa University, kwenda kunung'unika, wakisema tumetishwa sana huko, tunaonewa sana huko. Wabunge Watanzania wakakimbia kwenda kwa vijana University na kuwaambia vijana, tumetishwa huko. Wabunge!

Eti, afadhali wakati wa mkoloni!

Juu ya yote hayo, nasema hawataki kwenda kambini; wanataka mapesa yao, haki yao wanaitaka yote isibaki. Sasa madhali hawataki, wanasemaje? Wanapita jana mjini, na makaratasi yao yameandikwa maneno mbali mbali, mengine machafu machafu! Baadaye mimi nilisikiliza redio ya B.B.C.-B.B.C. ni redio ya waheshimiwa Waingereza―nikavizia nisikie nini hasa kilichowapendeza katika maneno haya wakakichukua kile wakakitangaza. Wanasema hivi: Nimesikia wakisema hivi: "Mwalimu Nyerere leo amefukuza wanafunzi wapatao 390 kutoka University College, na vyuo vingine, baada ya vijana hao kuandamana mjini, na kusema hawataki masharti ya National Service, na kusema kwamba afadhali wakati wa mkoloni! Afadhali wakati wa mkoloni! Na Waingereza wakarudia maneno yale katika B.B.C. Afadhali wakati wa mkoloni. Ndivyo wasemavyo vijana wetu.

Wananchi, Wakoloni hawakuijenga ile University College. Ile University College imejengwa na sisi. (Makofi) Tuliingia Serikalini mwaka 1960, na wakati huo wa 1960 tukakuta mpango wa wakoloni ni kujenga Chuo cha Tanganyika labda mwaka 1967; labda. Sisi tukasema tutakijenga, na tutakianzisha sasa hivi. Wakasema, Mtaanzisha wapi, majengo hamna. Tukasema, lile liko pale, jengo la TANU. Wakasema, wanafunzi mtapata wapi. Tukasema, Vyuo havianzi na wanafunzi elfu, vinaanza na wachache; tukaanza na wanafunzi 17. Leo vijana wetu wananiambia, afadhali wakati wa mkoloni.

Mwaka 1960 tulianza na wanafunzi 17, leo Chuo kile pale, kabla ya jana, kilikuwa kina vijana wa Tanzania peke yake 480. Wanachuoni wanasema, afadhali wakati wa mkoloni.

Mkoloni hakujenga Chang'ombe; siyo mkoloni aliyejenga Chang'ombe. Tumejenga sisi; juzi juzi nimekwenda kufungua Chang'ombe. Haikujengwa na mkoloni. Vijana wanasema, afadhali wakati wa mkoloni.

Si mkoloni aliyejenga Chuo kile pale cha Madaktari. Tumejenga sisi wananchi, tumejenga sisi. Nimekifungua wakati tumekwisha kujitawala kile Chuo pale, siyo wakati wa mkoloni. Vijana wanaotoka katika Vyuo hivyo hivyo, leo wanasema, afadhali wakati wa mkoloni.

Mkoloni hakujenga kile Chuo pale cha mafundi. Tumekijenga sisi hapa, kwa msaada wa Majerumani, na tumekifungua juzi juzi tu. Halafu Majerumani waliponigomea, tukatimuana! Vijana wenye elimu wananiambia, afadhali wakati wa mkoloni. Na B.B.C. wanatangaza, wanaitangazia dunia nzima kuwa vijana wenye elimu wa Tanzania wanasema, afadhali wakati wa mkoloni.

Ulikuwapo wakati wanafunzi wetu hawapati nafasi kuingia katika shule za sekondari. Tulikuwa tuna shule za Wahindi, shule za Wazungu, na shule za Waafrika. Leo hakuna hii. Hakuna shule za Wazungu, shule za Wahindi, wala shule za Waafrika; shule zote za wananchi. Vijana wanaotoka katika Vyuo hivyo wananiambia, afadhali wakati wa mkoloni. Eti afadhali wakati wa mkoloni.

Wakati wa mkoloni tulikuwa tunajilipia gharama za masomo. Masikini alikuwa hawezi, tajiri anaweza kumsomesha mtoto wake kwa mapesa. Tulipoingia Serikalini tukasema mpango huu hauna maana. Tukitaka watoto wetu wasome barabara tufute gharama za shule hizi, ndipo masikini naye ataweza akapenya na kuingia shule za sekondari. Leo katika shule za sekondari wanakotoka hawa wanalipiwa kila kitu na Taifa. Katika shule zetu zote za sekondari, na katika Vyuo vyote hivy, katika Chuo Kikuu, gharama zinalipwa na Taifa. Leo vijana wanasema, afadhali wakati wa mkoloni.

Mimi nilipoanza ualimu mwaka 1946, natoka Makerere na Diploma, mshahara wangu ulikuwa shilingi 122/-. Leo, leo mshahara wa chini Dar es Salaam, wa kibarua, siyo "Makerere Graduate", ni shilingi 180/- kwa mwezi! Vijana wa Vyuoni hawa wanasema, afadhali wakati wa mkoloni, kwamba eti hali ilikuwa nzuri sana wakati wa mkoloni.

Baada ya kumaliza Makerere, nimefundisha miaka mitatu; nimekwenda Ulaya nimesoma tena miaka mitatu, nimerudi na "degree" yangu ya M.A., nimeanza tena ualimu mwaka 1953. Mshahara wangu, wananchi, ulikuwa shilingi 500/- kwa mwezi. Nikapiga kelele nikaongezwa zikawa shilingi 750/-. Leo posho ya mwalimu National Service, posho siyo mshahara, posho ya kijana, mwalimu wa National Service ni shilingi 790/- kwa mwezi. Vijana hao wanasema, afadhali wakati wa mkoloni. Ndivyo wasemavyo vijana waheshimiwa.

Mwaka 1961, mwaka tuliojitawala, Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki, Vyuo Vikuu vyote vya Afrika Mashariki pamoja vilikuwa vina wanafunzi wa Kitanganyika 261 tu. Leo tunao wanafunzi 930. Vijana hawa wanasema afadhali wakati wa mkoloni, mkoloni, na B.B.C. inawaunga mkono, inautangazia ulimwengu wote usikie, kwamba afadhali wakati wa mkoloni.

Mwaka 1961 huo huo tulikuwa na watoto 53 wanasoma nchi ya Amerika. Leo, leo hivi kuna watoto 201 kule wanasoma. Vijana hawa wanasema, afadhali wakati wa mkoloni.

Mwaka 1961 tulikuwa na watoto 462 wanasoma Uingereza. Leo tuna 698 kule. Watoto wetu jana wametuambia, eti afadhali wakati wa mkoloni, na B.B.C. inasaidia kuitangazia dunia, kwamba afadhali wakati wa mkoloni.

Mwaka 1961 tulikuwa na wanafunzi wetu wawili wanasoma katika nchi ya Urusi, wawili; leo tuna 204 wanasoma Urusi. Vijana wanasema, afadhali wakati wa mkoloni, na B.B.C. Sauti ya waheshimiwa, inawasaidia kuitangazia dunia nzima, kwamba jana vijana walituambia kwamba afadhali wakati wa mkoloni.

Wanafunzi wote hao niliowataja mwaka 1961 katika sehemu zote hizo nilizozitaja walikuwa 808. Leo ni 2,033. Vijana wanatuambia wananchi, kwamba afadhali wakati wa mkoloni.

Mkoloni hakujali ujinga wetu, mkoloni hakujali umasikini wetu, mkoloni hakujali maradhi yetu. Mkoloni aliutumia unyonge wetu kama kisa, kama sababu, kama hoja, ya kuendelea kututawala zaidi. Sikupata kumsikia hata mkoloni mmoja anatembeatembea anawaambia wananchi wa Tanzania, kazaneni mjitegemee kwa nguvu zenu wenyewe; sikumsikia hata mkoloni mmoja anatangaza hivyo. Vijana tunaowasomesha wenyewe wanasema, na wanasaidiwa kutangaziwa na wakoloni, kwamba afadhali wakati wa mkoloni!

Wakoloni walikuwa wananiambia ghali sana kumsomesha mtoto. Na ni ghali sana wananchi, ghali sana kumsomesha mtu katika chuo kile. Gharama ya nchi hii kumsomesha mtoto mmoja pale mlimani, kwa mwaka mmoja, ni Sh. 24,000/-. Ndizo fedha za wananchi zinazotumiwa na kila mmoja wa vijana hao, kila mwaka, katika Chuo Kikuu. Leo watoto wanaozitumia fadhili hizo za nchi wanadiriki kusema, afadhali wakati wa mkoloni.

Wananchi, wako watu katika nchi hii ambao nitafurahi kesho na kesho kutwa waseme, afadhali wakati wa mkoloni. Wapo, lakini siyo kabwela. Mimi sipendi kabwela aseme, afadhali wakati wa mkoloni. Lakini wako watu, makupe, wanyonyaji wakubwa, wanaovuna wasichopanda, wanaokula wasichopika; wapo watu hao, wapo, wapo, bado tunao katika Tanzania, tena wengi. Kesho nitafurahi sana nitakaposikia wanaanza kusema, lo! ya-Rabbi, afadhali wakati wa mkoloni. Wapo, lakini si vijana, si vijana wetu tunaowasomesha. Makupe na yaseme, afadhali wakati wa mkoloni, lakini si wajengaji wa nchi hii.

Ila huenda vijana hao wamekwisha chagua upande wao. Labda vijana hao wamekwisha kwenda upande wa wanyonyaji. Vipi watasema, afadhali wakati wa mkoloni? Labda wamekwisha laghaiwa na wanyonyaji, labda wanyonyaji ndiyo wanaowatuma: semeni, afadhali wakati wa mkoloni. Hayo ndiyo maneno wanayosema vijana wetu. Mengine wanasema hivi, nitasema kwa Kiingereza:-

"This means that no efficiency will be aimed at in all sectors of public service, in teaching, in medical service, legal services and all possible corners where students will be placed during those 18 months insisted in the White Paper. And strongly believe even our parents and relatives who regard us as the most important economic asset have and will give no moral support to this issue."



Tutakataa kutumika.

Nitajaribu kutafsiri. Maana yake wanayotuambia ni kwamba hawatakuwa na shabaha ya kufanya kazi vizuri katika sehemu zote za utumishi wa Serikali, katika ualimu, katika matibabu, katika uanasheria na katika kona zo zote ambazo serikali itawaweka katika muda huo wa miezi 18. Wanasema wanaamini kabisa kwamba hata wazazi wao na jamaa zao ambao wanawaona vijana hao kwamba ndio chombo chao kikubwa cha uchumi kupita vyombo vingine vyote walivyo navyo hawataunga mkono jambo hili la Serikali.

Nitawaelezeni maana yake kidogo, vijana wetu wanavyosema. Wanasema, Watakataa kufanya kazi zao vizuri Serikalini. Kwamba tutamchukua miezi ile 18 tukamweka Serikalini hatakataa. Lakini hatakuwa na shabaha ya kufanya kazi vizuri. Atapokea hiyo posho tunayompa, lakini hatafanya kazi yake kwa vizuri. Tutamwambia kafundishe darasani, atakwenda darasani, lakini atakataa kufundisha vizuri; tutampeleka hospitali kwa wagonjwa, lakini anasema atakataa kuwatibu wagonjwa vizuri. Anasema, katika sehemu yo yote ya serikali, ambako tutamweka afanye kazi, atakataa kufanya kazi yake vizuri.

Kama ni mwalimu mheshimiwa huyu, ana ugomvi gani na wanafunzi wake, hata akatae kufundisha wanafunzi vizuri? Kama ni daktari, kijana wetu, tumemsomesha mpaka amehitimu, tukamkabidhi wagonjwa tunamwambia watibu wagonjwa hawa; anasema nitakataa kuwatibu vizuri. Ana ugomvi gani na wagonjwa hao! Anasema, po pote mtakapomweka kazi yake hataifanya vizuri. Wananchi wakimwendea kumtaka msaada, pengine ni mwana sheria anamtetea mtu, au anaitetea serikali, anasema kazi hatafanya vizuri.

Maana baba maskini.

Na zaidi wanasema vijana hawa kwamba wanaamini kuwa wazazi wao na jamaa zao watawaunga mkono. Mimi vile vile mzazi wananchi, mimi vile vile mzazi wananchi. Na mimi vitoto vyangu vimechelewa kidogo, lakini vinasoma. Na wakati wao ukifika nao wataingia National Service. Hivi wakikataa, mimi niwaunge mkono! Sasa wazazi mnaonisikiliza, na jamaa za watoto hawa, nawauliza hivyo kweli mnaweza mkawaunga mkono?

Na eti kisa chenyewe ambacho kitafanya wazazi wakatae, ni kwa sababu wazazi wanawaona watoto hawa ndio chombo chao kikubwa cha uchumi, na bila ya wao watakufa!

Ndugu zangu, wote tunafanya kazi. Mimi sijui kama hawa vijana wa jana wao ni watakatifu zaidi kuliko sisi. Nadhani sisi wote sawa. Sisi wa mishahara tuko wengi, tunajuana. Na wote tumetoka kwa baba masikini, mama masikini, mjomba masikini, jamaa zetu wote masikini; wote tumetoka kwa masikini. Mimi nimezaliwa katika nyumba ya mbuzi. Ijapo Mzee Nyerere ni chifu, lakini uchifu wenyewe wa ovyo. Nyumba hizi hizi zetu za msonge imegawanywa katikati; upande wa kule ndiko kuliko na kitanda na jiko, na upande wa huku ndipo tunaweka vigingi na kufungia ndama na mbuzi. Mimi ndimo nilimozaliwa katika nyumba ya namna hiyo. Na kuku humo humo. Mimi nimezaliwa na kukulia katika nyumba hiyo. Sijui hali yenu, wenzangu, lakini nadhani wengi wetu hali yetu ni ile ile.

Nchi yetu Maskini.

Sisi wote watoto wa masikini. Katika watoto wale walionijia pale wote watoto wa masikini, isipokuwa mmoja mmoja. Wote masikini na hali yetu wanaijua. Lakini wanasema kwa sababu sisi ni watoto wa masikini, ndiyo maana tunataka mapesa yetu yote hayo ili kusudi tumsaidie baba, maana baba ni masıkini; tumsaidie mama, maana mama ni masikini; tumsaidie mjomba, maana mjomba ni masikini. Ndugu zangu, nyinyi wenzangu tunaopata mishahara, wote sisi watoto wa masikini. Mimi nataka kusikia toka kwa wazazi mnaonisikiliza ni wangapi wazazi wanaopokea fungu kila mwezi, kwa wakati wetu huu? Na wazazi watajua mtoto ambaye akishakuupata mshahara, anajua hili fungu la baba, hili fungu la mama, hili fungu la mjomba, hili la shangazi! Ni wangapi wafanyao hivyo? Maneno ya kudanganya haya.

Nimtoze nani.

Na hata kama ingekuwa ni kweli, kwamba ninapopata mshahara wangu mimi hugawa, nikasema huu wa mama Nyerere, huu wa mjomba, huu wa shangazi, na huu wa yule. Nathubutuje kuliambia Taifa hili linilipe mshahara ambao hauwezekani? Alipe nani? Atozwe nani? Hao watoto na wengine wote wanaodai mambo haya, wanapodai haki yao, wanataka mishahara mikubwa, wanataka mapato makubwa, wanamdai nani? Wanamdai President, mimi nina pesa? Mimi nitazitoa wapi! Wanasema nizitoe wapi wanaposema mimi Sh. 1,000/- hazinitoshi, Sh. 3,000/- nizichukue kwa nani nimpe. Huyu anaposema Sh. 700/- hazimtoshi nataka maradufu, nataka Sh. 1,400/-, hizo Sh. 700/- nyingine nikamtoze nani? Hata kama akiniambia. “hizo utakazonipa nitampa mama.” Nimtoze nani kodi!

Nani aende atozwe kodı! Watu wa Tanzania wote masikini, isipokuwa wachache: na wachache hao ndio wanaokuja kunipigia kelele wanasema wanataka kunyonya damu ya watu. Nitazipata wapi pesa za kuwapa hawa? Hoja gani hii, uwongo gani huu, wananchi wa Tanzania, wananchi wa Afrika.

Tunadai mishahara minene, maana nchi yetu masikini.

Sababu hii inatoka wapi? Watu wachache wanasema sisi nchi yetu masikini: baba masikini, mjomba masikini, shangazi mtu masikini, ndiyo maana nataka mshahara mkubwa sana. Dunia nzima watu wenye akili husema jama nchi yetu masikini, mama masikini, baba masikini, shangazi masikini, wadogo zangu masikini, na wakubwa zangu masikini, nchi yetu yote ni watu masikini kwa hiyo, jamani, tuchukue mshahara kidogo kidogo. Hawasemi kwa hiyo basi kila mtu ajinyakulie kiasi anachotaka, maana sisi masikini.

Mawazo haya yanageukaje leo! Wanasema vijana hawa mawazo haya yanatoka kwa baba zao, na kwa mama zao. Hata kidogo! Baba, baba Mtanzania anasema mwanangu utakapokuwa katika miezi 18 yako hiyo, utakuwa unapata posho ya Sh. 790/-, mimi sikubali hata kidogo. Nenda mpelekee Serikali, uwaambie Serikali, kama asipogeuza atakiona cha mtema kuni! Wazazi wetu wakatuma watoto wanasema hivyo? Hata kidogo! Haya maneno hayatokani na vijana wetu, wala na mama zao, wala na baba zao, wala na shangazi zao, yanatoka mahali pengine. . . . . .
 
Anamaliza kwa kusema

Elimu si mali ya mtu binafsi.

Taifa husomesha watu wake kwa faida ya Taifa. Wanangu wanasomeshwa sasa. Wamepenya wawili katika msukosuko ule wa mwaka jana. Wamo katika sekondari sasa. Serikali inawalipia gharama zao zote. Siyo kwa faida yangu, siyo kwa faida ya mke wangu, hata kidogo. Wanalipiwa siyo kwamba kesho na kesho kutwa waje wanihifadhi mimi, hata kidogo, waihifadhi nchi. Kama ingekuwa kunihifadhi mimi basi Serikali iniwachie niwasomeshe wanangu. Angeachiwa kila mtu asomeshe watoto wake. Basi tunakamuana wote kwa pamoja kuwasomesha watu. Tunakamuana kodi, halafu wanasomeshwa watu wachache ili wakitoka walitumikie Taifa, kwa faida ya Taifa, siyo ya baba, au ya mama, au ya mjomba, au ya shangazi.

Ndiyo maana Taifa zima linawasomesha watoto hawa. Kama isingekuwa hivyo, kama ingekuwa ni kwa faida yake yule anayesoma peke yake, na kwa faida ya baba yake, na ya mama yake, si kwa faida ya Taifa, hapo angetujia na elimu yake kama mwenye mahindi, tunaanza kugombea bei. Kama ingekuwa hivyo ndivyo, na kwamba tulikuwa hatumsomeshi kwa faida ya Taifa, zile Sh. 24,000/- kila mwaka zingekuwa ni deni tunamkopesha yule mwenye elimu. Halafu akishatoka katika Chuo Kikuu angekuwa na deni la Sh. 72,000/-. Mbona tunafanya hivyo kwa wakulima wa mbolea, kwa wakulima wa mahindi, tunamkopesha mbolea, tunahesabu tunamvizia mpaka kwenye mavuno, tunamtoza. Japo mbolea ilikuwa mfuko Sh. 50/-, tunamtoza kwa sababu mahindi yale mali yake. Kama huyu kijana naye elimu vile vile ni mali yake, sio mali ya Taifa, ile ingekuwa ni mkopo sawa sawa kama wa mbolea, au kama wa “tractor”.

Hatukuwapa wakulima matractor bure. Kama anakwenda kujilimia shamba lake mwenyewe. Hatuwapi watu plau bure, kama haja yao ni kwenda kulima shamba lao wenyewe. Mtu aweza akaja akatuomba mbuzi, akatuomba nyavu tumpe za bure, kama anakwenda kuvua samaki zake mwenyewe, tutampa za bure kwa nini? Kwa hiyo watoto tunawasomesha kwa faida ya nchi nzima. Siyo kwa faida yake mwenyewe. Leo hawa watoto wanakuja kutuambia ni kwa faida yao. Wanadhani ni haki yao! Haya mawazo wameyapata wapi? Hayakutoka kwa baba zao. Yametoka kwa watu wakubwa. Mawazo haya hayawezi kuwa yametoka kwa baba zao. Moyo wao haumo.

Neno lao la mwisho wanalosema vijana ni hili. Ikiwa tutang'ang'ania mambo haya, basi wao huko katika National Service watakwenda mwili tu. Lakini moyo hautakwenda. Kisa kitakachofanya waende mwili huko, kwa sababu pesa zao, haki yao hawakupata. Moyo hautakuwamo. Ndio ule mpango walioueleza kwamba utamweka darasani, hatafanya kazi vizuri, moyo haumo, hataki. Utampa wagonjwa hatawatibu vizuri, moyo haumo, hataki, liko limwili tu. Akiwa mwana sheria, utamfanya atetee vizuri, hatatetea vizuri, limwili limwili tu, moyo tu, moyo haumo, hataki. Atawaacha watoto wale wataumia; wagonjwa wataumia na nchi itaumia. Sababu hajapata pato lake, mshahara wake, haki yake.

Mchunga mwema.

Wale waheshimiwa wanaojua habari za Injili watakumbuka Bwana Yesu aliwasema watu wa namna ile. Alisema iko tofauti baina ya mchunga aliye mwema, na yule aliye mbaya. Yuko mchunga, ambaye ana kondoo ni mali yake mwenyewe. Anawachunga kondoo wale kwa sababu ni wake. Akipotea kondoo atamtafuta kwa dhati, anawaangalia kweli kweli, maana ni kondoo wake. Halafu yuko mchungaji mwingine kondoo wale si wake, yeye kaajiriwa tu kuifanya kazi; huitwa kwa Kiingereza, “hire- ling". Moyo wake haumo katika uchungaji wa kondoo wale, anataka pesa tu. Akiona mbwa wa mwitu anakuja, mchungaji huyu hukimbia, hawezi kupigana naye. Moyo wake haumo. Lakini yule mchungaji ambaye kondoo wale ni mali yake, atapigana na mbwa mwitu, ijapo anajua ni hatari kubwa. Hivyo ndivyo kwa kondoo. Kondoo, siyo binadamu. Na Bwana Yesu kataja kondoo minyama, ina manyoya. Ni kweli kama kondoo ni mali yake mtu atapambana na mbwa mwitu humwachii. Hata kitoto kidogo cha kondoo humwachii mbwa mwitu akachukua, mtachubuana, madhali ni mali yako. Lakini kama wewe umeandikwa pale kwa mshahara tu, anaweza akaja mbwa mwitu akachukua mmoja akaenda akatafuna, wala hutajali. Nasema, hao ni kondoo.

Watu, si kondoo.

Hawa waheshimiwa wa leo hawazungumzi habari za kondoo, wanazungumza habari za watu binadamu, ndugu zao. Wanasema moyo wetu hautakuwamo, utakuwamo mwili tu, basi. Watoto hawatasomeshwa vizuri, wagonjwa hawatatibiwa vizuri. Kazi yo yote katika muda ule wa miezi 18 wanaopata posho haitafanywa vizuri. Moyo haumo, limo limwili tu, kama la maiti. Kisa, pesa. Wanasema vijana hao ukitaka nisomeshe barabara nipe fedha zangu zote. Ukitaka nitibu, nimpe dawa na kumwangalia huyu mgonjwa barabara basi nipe fedha zangu zote, nipe haki yangu yote. Kama hukunipa simpi dawa ya kweli wala simwangalii. Ndivyo wanavyosema vijana hao. Moyo wangu haumo madhali fedha zangu sipati.

Wananchi, maneno hayo yanasemwa na vijana wetu. Na sisi tunasema hivi. Nchi yetu itajengwa na watu wenye moyo, moyo umo ndani. Yule ambaye anatuambia kwamba mimi mkiniambia nikajenge nchi, na pato langu sipati nitaweka limwili tu, tunamwambia, Kwaheri. Kwa hiyo jana tukawaambia vijana wale, madhali mioyo yenu haitakuwamo, tunapoteza wakati wetu, na pesa zetu kuwasomesheni. Tukawaambia vijana nendeni majumbani, ahsanteni sana.



Nchi itajengwa kwa moyo.

Wananchi, nchi yetu hii, nchi masikini, haiwezi kujengwa kwa fedha, ziko wapi fedha? Nchi hii itajengwa kwa moyo. Niambieni fedha za kujenga Tanzania ziko wapi wananchi nionyesheni, kama si moyo! Wako wakubwa wenye fedha, labda tuwaite, waje. Lakini hata hivyo walikaa hapa miaka kadha. Siyo kwamba hawakuwapo hapa wenye fedha, walikuwapo. Sikuona kama wameijenga nchi hii. Na ndio hao hao wanaoshawishi semeni afadhali wakati wa mkoloni.

Enyi wananchi, nchi hii tutaijenga kwa moyo, kwa kila mmoja wetu aseme jama nina kapato fulani, sasa nijifunge moja kwa moja pamoja na wenzangu, tuijenge nchi yetu. Vijana wanakula, wanashiba, na wamepata elimu. Tunachowataka vijana hawa wafanye ni kazi ya kujenga nchi. Tunawaambia, vijana, sasa shikeni sururu; shikeni vyombo; nendeni madarasani, nendeni mashambani, nendeni viwandani, kila mahala. Kila mmoja afanye kazi, madhali anashiba, vijana hawataki.

Haimkini tena tukae na vijana wetu wenyewe tunabishana, anauliza "how much", yaani atalipwa kiasi gani! Tumetamka, Bwana, kwa miezi hii ya kwanza, miezi ile 18 tutakupa Sh. 790/- posho. Anang'aka kijana, anasema hii ni "forced labour", yaani utumwa!

Nakubali, mishahara minene mno.

Nimewaambia vijana wale walipoanza kunitajia habari za mishahara, kwamba nakubali habari za mishahara, kuwa mikubwa mno. Walifikiri wanaweza kututisha, sijui. Wakasema punguzeni mishahara yenu. Nikasema, kweli vijana. Nilitaka kusahau hili neno la mishahara mikubwa. Alhamdu-Lillah, watoto wamenikumbusha habari ya mishahara mikubwa. Niliwaambia jana mishahara yetu ni mikubwa, kweli. Wananchi nataka kuwakumbusheni mishahara yetu kweli mikubwa. Mishahara yetu mikubwa mno wananchi. Niwieni radhi niwaelezeni ukubwa wake.

Nimerudi hapa kutoka Ulaya mwaka 1952 halafu nikaanza kazi mwaka 1953. Kama nilivyowaambieni nikapata mshahara wangu Sh. 500/- kwa mwezi. Nikapi- gapiga kelele, nikaongezwa zingine Sh. 250/- zikawa Śh. 750/- kwa mwezi. Kabla ya kutoka Uingereza nilikuwa nimejaribu kupata kazi Uingereza, kwa hiyo nilielewa kama ningebaki Uingereza wakati ule, ningepata mshahara huo huo Sh. 500/- nilizozipata hapa. Au kama "degree" yangu ingekuwa ni "honours" (maana wananchi “degree” yangu siyo "honours", ni ya kawaida), na ni ya sayansi, ningeweza nikapata kazi nikapata Sh. 9,000/- kwa mwaka, ndiyo hizo shilingi 750/- nikazipata hapa kwa mwezi. Nikarudi nikijua mishahara ya Uingereza, na ningebaki kule siyo kwamba ningekuwa napewa mshahara wa ubaguzi, la. Mwingereza ye yote, mwenye elimu yangu, alikuwa anapata Sh. 500/- hizo, au kama "degree" yake si ya namna yangu, inaizidi ina kiheshima-heshima, anapata Sh. 750/-. Nikaja hapa, nilipofika hapa wananchi nawaambieni nikapata Sh. 500/-, nikapiga kelele, nikaongezwa zikawa Sh. 750/-. Zile za Uingereza ningekuwa nalipa income tax, kama ningekuwa nazipata niko Uingereza, lakini hapa nilikuwa silipi income tax. Kwa nini? Kwa sababu huku walijitengenezea wakoloni mishahara. Mshahara unaolipa income tax ni mkubwa sana; huo wangu ulikuwa mdogo haulipi income tax. Juu ya mshahara wangu huo wa Sh. 750/- kwa mwezi (ambao mwenzangu Mwingereza aliyebaki Uingereza haupati, mimi hapa naupata, bado wake unalipa income tax; wangu haulipi); nilikuwa napewa inaitwa "cost of living allowance" 35 kwa mia. Naongezwa Sh. 35/- kwa kila Sh. 100/- za mshahara huo. Mwenzangu aliyebaki Uingereza hazipati hizo, mimi napata. Mwenzangu zake zinalipa kodi, za kwangu hazilipi. Ndio mshahara niliokuwa naupata pale Pugu, mimi nikafurahi.

Niliona dhuluma tupu. Lakini sio kuwa nikafurahi tu, nikaona dhuluma hii, kwa sababu mimi mshahara ule ambao wakati huo unauzidi ule wa Uingereza kwa hali zote hizi nilizowaeleza, wa kwangu ulikuwa ni sitini kwa mia ya mshahara wa Mwingereza anayefanya kazi Tanzania, yaani Mwingereza ye yote tuliyesoma naye pamoja, na kuja naye hapa angepata zaidi.

Wanyonyaji wakubwa.

Walikuwa wanyonyaji wakubwa wale! Kwao walikuwa hawalipwi mishahara minene namna ile; hapa wanalipwa! Halafu bado niko Pugu, wakati nashangaa juu ya mishahara hii, ukaja uchunguzi wa mishahara inaitwa "Salary Commission". Mishahara yote ile minene ya wanyonyaji, walikuwa bado wanafikiria kuongeza tena! Nikasema tutatambuana, wanataka kujijazia tena misha- hara; mishahara hii inatoka kwao au inatoka hapa ? Kila senti ya mshahara ule anaolipwa inatoka hapa Tanzania, hakuna hata senti moja inayotoka kwao. Hawana uchungu nazo. Wangeongeza tena mishahara hii, na hata wa kwangu mimi, ambao ni 60 kwa mia ya mishahara yao, lakini juu ya hivyo unazidi wanavyolipwa kwao, tena wanataka kuongeza!

Zikapitikana hila.

Wakati huo nilikuwa Member wa Legco, wa muda, namshikia Mheshimiwa Kidaha ambaye alikuwa hayuko. Nikaingia mimi kama mwenda wazimu, naropoka mno, nasema, Majizi haya, yanataka tena kuongeza mshahara, watu wabaya sana, ngoja nitakapokwenda katika Legco, mimi nitapiga makelele. Na kweli Wazungu, walioitwa "unofficial", wao vile vile hawataki, maana wao walikuwa hawapendi wale watumishi wa Serikali. Nikaona barabara, Wazungu hawataki, na ikiwa Waafrika vile vile tutakuwa tumekataa, nadhani tunaweza kupata Wahindi vile vile wakatae, kusudi Wakoloni waweze kujinyakulia wenyewe, na nchi nzima ijue kwamba hatukubali. Nikapiga kelele namna hiyo, nikaambiwa ngoja tu, utaona. Habari ikapita, ikafika kwa bwana wakubwa. Mheshimiwa Kidaha akapakiwa kwa ndege, kurudi haraka haraka. Nikajikuta nimeshatolewa, simo tena katika Legco! Nikasema kilimilimi changu kimeniponza, afadhali ningelijinyamazia.

Na legco ikakubali.

Lakini hata hivyo sikuacha. Nikaonana na Waafrika wa Legco, nikawashawishi, Jamaa mkatae! Basi tukakubaliana; pingeni, hii mishahara mibaya, haifai jamaa; anayelipa ni masikini! Bahati mbaya hawakupinga, mishahara ikapitishwa, mishahara mikubwa-mikubwa!

Na sasa zamu ya Wazungu weusi.

Sasa Waafrika tunanung'unika, mbona hatulipwi na sisi. Sisi haki yetu ni kulipwa mishahara ya Kizungu, mbona hatulipwi ya Kizungu? Basi mishahara ikapita, mishahara minene-minene. Na sasa sisi Waafrika tunasema, Ngoja sasa, saa yetu itakapofika tujitawale, na sisi tutaipata hiyo mishahara ya Kizungu. Muipate kutoka Ulaya, au muipate kutoka wapi?

Kwa hiyo, wananchi, kweli tunayo mishahara mikubwa, mpaka sasa tunayo. Mpaka sasa tunayo mishahara mikubwa-mikubwa ya ajabu. Anatoka mwalimu chuoni pale, tunamlipa Sh. 1,320/-, mtoto wa shule tu! Nikawaambia jamaa hawa, kweli mishahara mikubwa mno, ipunguzwe, nitaanza na wangu, Vijana wakang'aka. Nikasema kweli, nitaanza na wangu; mishahara mikubwa mno hii. Nikawaambia mnajua mshahara wangu Sh. 5,000/- kwa mwezi ?

Pengo kubwa.

Ngoja niwaelezeni habari ya mshahara kama huu, Sh. 5,000/- kwa mwezi, maana yake nini? Maana yake, kama yuko miongoni mwenu hapa kibarua ambaye yeye anapata Sh. 200/- kwa mwezi, mimi napata Sh. 5,000/- kwa mwezi, itamchukua kibarua huyo miaka ishirini na mitano kupata mshahara wangu wa mwaka mmoja! Hiyo ndiyo maana ya tofauti yake na mimi. Nasema nchi yo yote iliyo na tofauti ya namna hiyo haijawa ya ujamaa!

Basi si afadhali wewe unayepata Sh. 200/- kwa mwezi. Mchukue mkulima, ambaye pengine hukusanya vyake vyote, hukusanya visenti vyake atakavyouza, uhesabu na mihogo, uhesabu na kunde, uhesabu na kisamvu, ukusanye vyote pamoja, pengine kapato kake ukikajumlisha ni Sh. 100/- kwa mwezi. Fedha nitakazopata mimi za mshahara wa mwaka mmoja, yeye itamchukua miaka hamsini ndio azipate! Nasema kweli mpaka amekufa hawezi kuzipata! Maana nani anaweza kufanya kazi miaka hamsini? Atakuwa amekwisha, hawezi kuzipata. Na nchi yo yote duniani, na hasa katika Afrika, kama ina tofauti kubwa namna ile, kati ya pato la mtu na mtu mwingine, japo, ni kati ya mkulima na Rais, nchi ile haina haki ya kujivuna hata kidogo. Ina haki gani ya kujivuna nchi ya namna ile, kama mimi mshahara wangu wa mwaka utamchukua masikini wa Tanzania miaka hamsini kuupata, tunajivunia nini? Ni nchi ya aibu! Mishahara yetu kweli ni mikubwa, mikubwa sana, ipunguzwe!

Tuanzie mshahara wangu.

Kwa hiyo, vijana waliponiambia jana mishahara ya Mawaziri ikatwe nilikubali kabisa nikasema, naam, nitaanza na wangu. Nikawaambia. Pale pale wakasema, "Lakini ikatwe miezi ishirini na nne, ikatwe miezi ishirini na minne tu". Nikashangaa, nikauliza, kwa nini iwe miezi ishirini na minne? Wakaruka, Vijana wale wakaruka, Hapana. Wakaruka, maana nawakatia ugali wao moja kwa kwa moja tena. Na sasa nawaambieni maana nilikuwa sitanii hata kidogo na wala sitanii. Nikamwambia Waziri wa Fedha, Mshahara wangu tangu jana, tarehe ishirini na mbili, mshahara wangu upunguzwe kwa Sh. 1,000/-. Tutazungumza ile mingine iliyobaki baadaye, wananchi, tutajuana wenyewe huko huko.

Tuendavyo si sawa.

Lakini nasema, wananchi, tuendavyo si sawa. Tutakaa tunafikiria mishahara, mishahara, ni wale wenye kipato tunaohusika, sio yule mkulima, au kabwela. Vijana waongo hawa, wanasema sisi tunafikiria baba zetu, wakulima masikini. Ungemfikiria mkulima husingedai hizo pesa. Anatozwa nani ulipwe, kama siyo masikini? Ukitaka kufikiria masikini wanasema tumekuwa makomunisti. Watu tuache kufikiria habari za watu masikini tukae tunafikiria kujijazia mali, mali, mali, hivyo tutakwenda nayo wapi hiyo mali, wananchi?

Wananchi wa Tanzania, ikiwa ninyi viongozi, mtakaa mnadai binafsi mali, mali tu, basi nchi hii haijengeki, ng'o! Wananchi mnasema, kwanza tuanze na raha, ndio tujenge nchi; kwanza tupate majumba mazuri, na magari mazuri, na kitumbua chenye asali, halafu ndiyo kazi ianze. Lakini duniani haiwi hivyo. Duniani mnapoipokea nchi yenu masikini kama hii, mnaanza kwanza kwa kazi ya kuijenga, raha inakuja baada ya kazi. Hata tukisema wachache waanze kwa raha, sasa tunasema wengine wawe ni watumishi wa wachache? Maana haiwezekani wote waanze kwa raha hata kidogo; lazima wengine wote wabaki katika taabu.

Mbona Watanzania wengine wanashukuru.

Juzi juzi nikaambiwa wafanyakazi wa bandarini, wamepita mjini Dar es Salaam wakifurahi kwa sababu wamepata masai mbili! (Masai ni ile noti ya shilingi mia, ina picha ya mmasai, kwa hiyo kwa mkato huitwa masai). Makuli wanafurahi wamepata masai mbili, yaani shilingi mia mbili; wanafurahi mno. Wanafurahia nini masikini wale? Hivyo shilingi mia mbili zina kumfurahisha mtu? Lakini wao zimewafurahisha. Kwa sababu, watu masikini, watu hao masikini wanapata kima cha chini kizuri pale, Sh. 330/-. Na hizo Sh. 330/- hazifikii hata nusu posho ya Mheshimiwa huyu anayedai haki yake. Lakini masikini hawa wanafurahi, wanapita humu wanashangilia.

Hawa wanafunzi wenu wenye elimu kubwa, wao posho tu, posho ya kufundisha darasani, karibu Sh. 800/-. Wanatuambia, tusipoziongeza tutakiona cha mtema kuni! Ndugu zangu, wenye elimu, tutaijenga nchi namna hiyo? Tutakuwa majibwa kupora na kunyang'anya tu mali ya wananchi? Nasema namna hiyo haiwezekani. Wananchi, tuijenge nchi yetu.

Maana ya ujamaa.

Maana ya ujamaa ni kwamba watu wote wanaishi pamoja, wanafanya kazi pamoja, kwa manufaa ya wote, siyo watu wengi wanafanya kazi, wanyonywe na watu wachache, huo si ujamaa hata kidogo. Hata kama wachache hao, wengine wanajiita Rais, wengine wanajiita Makamu, hao ni wanyonyaji wakuu.

Basi, wananchi nimechukua muda mrefu sana kuwaelezeni jambo hili, siyo tu kwa sababu tumewafukuza wanafunzi 390, la! Mwenzangu, Waziri wa Elimu aliniambia, loo! Wanafunzi wangu wengi watakwenda, sasa waalimu tutapata wapi? Nikamwambia kweli tumepata hasara, lakini kazi yetu sisi siyo kufundisha waalimu, au kufundisha waganga, tunajenga nchi. Nchi, inajengwa kwa tabia, kwa moyo. Tukikubali masharti tuliyopewa na na wanafunzi hawa tutakuwa kweli tuna waalimu, na madaktari; lakini tutakuwa tumekubali moyo wa namna gani, na tutakuwa tunajenga Tanzania ya namna gani? Kwa hiyo, nikasema: Acha tupate hiyo hasara na hata kama nchi ikisituka, na isituke, halafu tutawaeleza wananchi kwa nini hatua hii imechukuliwa.

Nendeni muone.

Leo ziko nchi duniani, watu wanakwenda kuona jinsi watu wanavyojenga nchi zao. Viongozi na wananchi wote wameshikana moja kwa moja, wanajenga nchi yao, kwa faida ya nchi yao. Matumaini yangu, wananchi, ni kwamba kesho na kesho kutwa watu watasema: Nendeni, muone Watanzania wanavyojenga nchi yao.

Ahsanteni sana.
 
Haya maneno yaliwafanya vijana wengi kuwa kama vichaa miaka ya 60 to 70s

"Tunataka kuona katika Taifa hili, vijana jeuri na wenye kujiamini, si vijana waoga, akina "ndiyo bwana mkubwa", vijana wanaohoji na kupiga vita mifumo ya jamii isiyoshabihiana na matakwa na matarajio ya jamii ya kitanzania. Tunataka vijana waasi dhidi ya mifumo kandamizi, ubwana na ufisadi katika Taifa"

Mwl J.K. Nyerere, Rais wa Kwanza wa Tanzania
 
Back
Top Bottom