SoC04 Nyumba na makazi bora kwa raia yenye kuleta tija kwa maendeleo ya taifa letu

SoC04 Nyumba na makazi bora kwa raia yenye kuleta tija kwa maendeleo ya taifa letu

Tanzania Tuitakayo competition threads

ZMK24

Member
Joined
May 2, 2024
Posts
6
Reaction score
48
UTANGULIZI
Ningependa kumshukuru Mwenyezi MUNGU kwa fursa hii muhimu kwa kuleta mapendekezo na mawazo bunifu yatayoimarisha nchi yetu kwenye sekta ya nyumba na makazi bora kwa raia wa Kitanzania.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokua kwa kasi kiuchumi, hii inafanya kuwa na ongezeko kubwa la maeneo mengi ya mjini ukilinganisha na kipindi cha nyuma. Idadi kubwa ya ongezeko la watu kwenye maeneo ya mjini, huathiri kwa kiasi kikubwa soko la nyumba na makazi ambapo mahitaji huwa juu kuliko uzalishaji (ujenzi). Kulingana na tafiti iliyofanywa na shirika la (Shelter Afrique – Tanzania Housing Sector 2012) inakadiriwa Tanzania ina upungufu wa nyumba milioni 3, huku uhitaji wa nyumba ukiongezeka takribani laki 2 kila mwaka. Pia ongezeko la watu nchini kunachangia kuwa na muundo wa soko la nyumba na makazi yasiyo rasmi, ama nyumba zilizojengwa kiholela bila kufuata utaratibu, ama nyumba zilizojengwa kwa viwango duni, na upangaji holela wa bei kwenye soko.

Tofauti na kikwazo kikubwa cha uhaba wa nyumba, pia tuna changamoto kubwa ya nyumba zisizo na viwango stahiki kwa makazi ya watu. Tukichukua mfano Dar es salaam maeneo kama vingunguti, manzese, mbagala, gongo la mboto, na mengineyo, ni kawaida kuona chumba kimoja wanaishi zaidi ya watu wa 3, pia ni kawaida kuona nyumba moja yenye vyumba zaidi ya 5 wanatumia choo kimoja, na matatizo mengi ambayo kwa kweli yanaathiri shughuli za kuiuchumi pia ata maadili ya vizazi vyetu.

Screenshot 2024-06-04 at 17-01-46 Photo album - Photo album.pdf.png
(Picha kwa hisani ya mtandao, na tovuti binafsi)
JITIHADA ZA SERIKALI KUTATUA TATIZO LA NYUMBA NA MAKAZI NCHINI
  • Serikali kupitia shirika la Nyumba la Taifa (NHC), linatekeleza miradi mingi ya ujenzi wa nyumba na makazi ya watu, mfano miradi ya nyumba 1000 za Iyumbu na Chamwino, Dodoma, pia mradi wa Samia Housing Scheme (SHS), Muheza Afforadable Housing Project – Tanga, na miradi mengineyo.
  • Kuanzishwa kwa Tanzania Mortgage Refinance Company limited (TMRC), inayomilikiwa kwa hisa na Taasisi za kibenki na zisizo za kibenki, kuhakikisaha mikopo ya uhakika na yenye riba nafuu kwa watanzania kupata nyumba zenye viwango bora.
Pamoja na jitihada nyingine nyingi za Serikali kuweka na kutekeleza sera wezeshi za uwekezaji wa ujenzi wa nyumba nchini, ushirikiano na sekta binafsi, na juhudi nyingine. Bado wawekezaji binafsi na Serikali wanakimbia kwenye tatizo sugu la kuboresha makazi kwa wananchi, na kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye upanuzi na ujenzi wa nyumba mbali na mijini au maeneo yaliyojitenga.

Kwahiyo ni bora kuwekeza nguvu kwenye maboresho ya nyumba na makazi ya watu, kuliko kuanzisha miradi mikubwa ya ujenzi wa nyumba na makazi mengine.

MAPENDEKEZO KWENYE SEKTA YA NYUMBA NA MAKAZI
1. Kutumika kwa Mafao na Pensheni za Wastaafu kuwajengea au kuboresha nyumba za kuishi.

Serikali kupitia mifuko ya hifadhi za jamii kama NSSF, PSSF, itoe mapendekezo kuwa nyumba na makazi bora ni haki na wajibu kwa kila Mtanzania. Kila mwajiriwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii aweze kumiliki nyumba yake.

Mfano Serikali inaweza kuweka utaratibu kwa waajiriwa wenye zaidi ya miaka 20 kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, wapeleke hati zao za nyumba ili kiasi cha fedha kilichopo kiweze kukarakabati nyumba kwa viwango vilivyoweka nchini, na wasio na nyumba waweze kununua kwenye miradi ya Serikali.

2. Taasisi za serikali na binafsi, ziwe na majengo yao binafsi pamoja na nyumba za wafanyakazi.
Kuondokana na tatizo la uhaba wa majengo na makazi ya kuishi, Serikali yetu ichukue jukumu la kupitisha sheria kuwa kila kampuni na taasisi za kiserikali na binafsi kujenga makazi na nyumba za kuishi kwa watumishi wao.

Kampuni nyingi binafsi zinavuna faida kubwa zikiwa zimepangisha ofisi huku wafanyakazi wake wakiishi maeneo binafsi, biashara zikifunga au vibali vikiisha nchi yetu inabaki na miundombinu mibovu ya nyumba na makazi. Pia mashirika mengi ya kiserikali yanayojiendesha kibiashara hapa nchini na kuingiza mapato makubwa kwa serikali bado wanakodisha ofisi kwa ajili ya shughuli zao, na nyingine hazitoi huduma ya makazi kwa watumishi wake.

3. Utaratibu wa mfumo wa soko la nyumba na makazi nchini kwa kiasi kikubwa utawaliwe na Serikali
Soko la nyumba na makazi limekuwa soko lisilo rasmi kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na masoko mengine kama soko la fedha au soko la bidhaa na huduma, hili limefanya kuwe na ujenzi holela wa nyumba na makazi nchini. Yafuatayo yafanyike kutoka kwa serikali:
  • Kwanza, sheria madhubuti zitungwe kwenye soko. Kama sheria za ubora wa nyumba mjini na vijijini, Udhibiti wa bei kwenye soko la nyumba, Wawekezaji binafsi wote wasajiliwe.
  • Pili, Serikali ihakikishe kuna wadhibiti ubora kwenye ujenzi wa nyumba mpya, hasa kwenye maeneo hatarishi hasa mijini.
  • Tatu, Wizara ya Ardhi ihakikishe upatikanaji wa ramani zenye muundo bora wa usanifu za makazi ya watu ambapo TMRC na washirika wake (Mabenki), na NHC na sekta binafsi, zitumie ramani kuboresha nyumba zilizopo au kujegwa upya kwa nyumba kwa mikopo nafuu.
4. Mipango ya kimkakati ya Kuboresha nyumba na makazi uwe kwa vipindi tofauti tofauti kwa kila mkoa nchini.
Ni wazi kuwa hatuna bajeti toshelezi ya kutekeleza ujenzi wa nyumba na makazi kwa wakati mmoja nchi nzima. Hivo kwa Tanzania tuitakayo miaka 5-25, Tuhakikishe kila mwaka tuna wekeza nguvu kwenye mkoa mmoja, Mpaka ifikapo miaka 25 mikoa 25 itakuwa imefikiwa na ahueni ya nyumba na makazi bora.

Screenshot 2024-06-04 at 16-29-20 Photo album - Photo album-1.pdf.png

Picha kutoka ukurasa wa mtandaoni (NHC na TMRC)

HITIMISHO
Nyumba na Makazi bora ni silaha tosha kushinda vita dhidi ya Umaskini, Maradhi na Ujinga. Miundombinu bora ya makazi ni mazingira wezeshi ya kufikika kwa huduma za kijamii kama maji, umeme, elimu, na miundombinu mengine kama barabara. Pia inaweza kuwa suluhisho la matatizo mengine kama foleni kwenye maeneo ya mjini, kwasababu ujenzi bora kwa makazi hutengeneza barabara nyingi za kufika mijini, Pia ni faida kwa vyombo vya usalama kufika kwa urahisi kwenye matukio ya kiuhalifu na huduma za dharura kama majanga ya moto na faida nyingi lukuki. Tanzania Tuitakayo yenye nyumba na makazi bora inawezekana.
 
Upvote 13
Back
Top Bottom