Intaneti Afrika: Ni wapi Serikali zimefungia mtandao na hufanikiwa vipi kuubana?
- Peter Mwai na Christopher Giles
- BBC Reality Check
14 Aprili 2019
Imeboreshwa 2 Novemba 2020
Nchini DRC Internet ilifungwa mwanzoni mwa mwaka 2019
Hakuna Facebook, Twitter wala WhatsApp.
Ndilo jambo linalozidi kuwa la kawaida katika baadhi ya mataifa ya Afrika, ambako serikali zimezima mtandao wa intaneti mara kwa mara au kuzuia mitandao ya kijamii.
Wanaharakati wa kutetea haki katika dijitali wanasema ni kubana taarifa, lakini serikali zinadai inasaidia kuimarisha usalama.
Je, ni wapi Afrika mtandao umekuwa ukibanwa na mataifa hufanikiwa kufanya hivyo vipi?
Ni mataifa gani Afrika yanabana matumizi ya intaneti?
Serikali inaweza kubana matumizi ya intaneti kwa kuagiza makampuni yanayotoa huduma za intaneti (ISPs) kudhibiti au kubana uwezo wa wateja kuingia katika mitandao.
Mara nyingi huwa kuna kizuizi kinachowekwa kuwazuia wateja kuingia katika mitandao ya kijamii inayotumika kwa sana.
Kwa hatua kali zaidi, serikali inaweza kuagiza kufungwa kabisa kwa huduma nzima ya intaneti.
Visa vya kufungiwa au kubanwa kwa mtandao Afrika vimekuwa vikiongezeka.
Tanzania ilibana matumizi ya intaneti na mitandao ya kijamii wakati wa uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa Oktoba.
Na Juni mwaka huu, Ethiopia ilizima intaneti kwa karibu mwezi mmoja kutokana na fujo na mauaji yaliyofuatiwa kuuawa kwa mwanamuziki na mwanaharakati maarufu wa jamii ya Oromo Hachalu Hundessa.
Zimbabwe, Togo, Burundi, Chad, Mali na Guinea pia zimefunga au kubana matumizi ya mtandao katika kipindi fulani mwaka huu.
Mnamo 2019, kulikuwa na visa 25 ambapo intaneti ilifungwa kwa kiwango fulani au kabisa, ikilinganishwa na visa 20 mnamo 2018 na visa 12 mnamo mwaka 2017, kwa mujibu wa kundi la uangalizi la kujitegemea la Access Now.
Na shirika hilo linasema kwamba mwaka 2019, mataifa saba kati ya 14 yaliyozima mtandao hayakuwa yamefanya hivyo awali.
Mataifa hayo ni Benin, Gabon, Eritrea, Liberia, Malawi, Mauritania na Zimbabwe.
Ni mtindo unaodhihirika dunani. Mnamo 2019, kulikuwa na visa 213 vya intaneti kubanwa ikilinganishwa na 188 mnamo 2018, na 106 mwaka 2017.
Shirika la Access Now linasema visa vingi Afrika huhusisha kuzimwa au kufungiwa kwa intaneti au mitandao ya kijamii nchi nzima badala ya maeneo fulani.
Ni Sudan na Ethiopia pekee zilizozima mtandao maeneo fulani mwaka uliopita.
"Hii inaashiria kwamba visa vya kufungiwa na kubanwa huku kwa mtandao vinaendelea kuongezeka lakini pia idadi ya watu wanaoathirika Afrika inaongezeka," shirika hilo linasema.
Intaneti hufungiwa vipi?
Katika kila nchi, huwa ni makampuni yanayotoa huduma hiyo ya intaneti kutekeleza maagizo ya serikali ya kubana intaneti.
Mfumo mmoja unaotumika unafahamika kama 'URL-based blocking', ambapo huwa wanazuiwa viunganisho fulani kwenye mtandao.
Huu ni mfumo unaohusisha kuweka kizuizi, kama kichujio hivi, kinachowazuia wateja kuingia katika mitandao iliyopigwa marufuku.
Mteja anayejaribu kuingia katika mitandao hiyo hupata ujumbe "server not found" (sava haipatikani) au "tovuti hii imezuiwa na msimamizi wa mtandao.
Mfumo mwingine unafahamika kama 'throttling', kwa maana ya kubana au 'kunyonga'..
Mbinu hii huzuia kwa kiwango kikubwa idadi ya wateja wanaotembelea mtandao fulani, na kutoa hisia kwamba kasi ya huduma ni ndogo na kuwafanya wateja waelekee kwingine.
Mbinu hii huwa vigumu kwa anayetumia mtandao kubaini kwamba inafanyika, kwa sababu ni vigumu kubaini iwapo mitandao inauiwa wazi au kupungua kwa kasi ya mtandao ni kutokana na mapungufu ya miundombinu.
Kama hatua ya mwisho, makampuni ya mawasiliano yanaweza kutakiwa kufunga kabisa huduma kwa ujumla na kuzuia wateja kupokea data yoyote.
CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES
Maelezo ya picha,
Mawasiliano ya intaneti yalifungwa wakati wa maandamano Zimbabwe
Je makampuni ya kutoa huduma yanaweza kusema Hapana?
Uwezo wa serikali kubana intaneti unategemea uwezo wao kudhibiti makampuni ya mawasiliano nchini.
Makampuni ya kutoa huduma ya mawasiliano yanapewa vibali na serikali, jambo linalomaanisha kwamba huenda wakatozwa faini au wakapoteza vibali vya kuhudumu.
CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES
Maelezo ya picha,
Watu wengi hutumia simu za kisasa barani Afrika kupata huduma ya intaneti
Kampuni hizi zinaweza kuwa na haki ya kukata rufaa mahakamani, lakini katika uhalisia huwa nadra sana kwao kuamua kutumia njia hiyo.
Mapema mwaka jana mahakama nchini Zimbabwe iliamua kurudishwa huduma ya intaneti baada ya serikali kuagiza ibanwe.
Kwa upande wake serikali ya Zimbabwe nayo baadaye iliidhinisha sheria mpya zinazoipatia udhibiti mkubwa katika matumizi ya intaneti.
Waziri wa habari Zimbabwe Monica Mutsvangwa alisema hili "litahakikisha kwamba intaneti na teknolojia zinazohusika zinatumika kwa manufaa ya jamii, na sio kukiuka usalama wa kitaifa."
Lakini kuna mifano pia ambapo serikali zinazotaka kufunga intaneti zinakuwa na urahisi wa kulitekeleza hilo.
"Kuna mataifa kama Ethiopia ambapo sekta ya mawasiliano ya simu bado iko chini ya serikali", anasema Dawit Bekele, mkurugenzi wa ofisi za Afrika za jamii ya Intaneti.
CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES
Maelezo ya picha,
Kuzimwa kwa Internet imekua kawaida Afrika.
Isipokuwa tu iwapo intaneti itafungwa kabisa, kuna namna ambazo wateja wanaweza kutumia kuepuka vizuizi vilivyopo na kuingia katika mitandao.
Mbinu inayofahamika sana ni ya kutumia huduma zinazoruhusu kuruka vizuizi (VPNs).
Huduma hizo hutumia teknolojia inayowezesha kuficha asili na alipo mtu anayetumia mtandao. Kwa mfano unaweza kuwa upo Tanzania lakini kwenye mtandao asili yako inachukua ya taifa moja la Ulaya. Hilo huifanya vigumu kwa makampuni ya kutoa huduma za intaneti kuweka vizuizi kwa mitandao iliyopigwa marufuku.
Serikali zinaweza pia kuzuia VPNs, lakini mara nyingi hujizuia kufanya hivyo kwasababu hutatiza pia shughuli za wanadiplmasia na makampuni makubwa yanayotegemea intaneti kwa shughuli zao.
Baadhi ya mataifa yametaja sababu ya kusambaa kwa "habari za uongo" katika mitandao kama sababu ya kuidhinisha vikwazo kwenye matumizi ya mtandao.
Lakini wachambuzi na viongozi wa upinzani wanataja hii kuwa njama tu ya kukandamiza makundi yanayozikosoa serikali, ambayo hutumia mitandao kama Facebook na WhatsApp kuratibu na kuendeleza shughuli zao.
"Kabla, wakati na baada ya uchaguzi, mataifa mengi hufunga mtandao kwa sababu ya upinzani," anasema Bw Bekele.
bbc swahili