Ombi la mtoto kwa baba yake mzazi (SHAIRI)

Ombi la mtoto kwa baba yake mzazi (SHAIRI)

Urban Edmund

JF-Expert Member
Joined
Mar 20, 2018
Posts
2,250
Reaction score
3,607
watoto (wanafunzi) wanaendelea na story zao za hapa na pale huku wanasimuliana jinsi siku ilivyokuwa nzuri shuleni.
watoto hao wanaagana na kila mmoja anaenda nyumbani kwake, Huyu mmoja anakaribia kwake na anamkuta baba ake akiwa ana furaha sana.
baba anamuita mtoto wake na kumuambia jinsi alivyonunua maeneo mengi kwa ajili yake mifugo na uwekezaji mkubwa alioufanya kipindi cha hivi karibuni kwa ajili ya mtoto wake mpendwa lakini pia Baba anamuuliza mwanae kitu gani kingine anachotaka Mtoto anamwambia (Kitu nachotaka Baba ninahitaji kusoma)

KITU NACHOTAKA BABA NINAHITAJI KUSOMA
Hodi hodi naingia, baba bora umekuja
kuna jambo kukwambia, nisikize mara moja
shairi nakusomea, sikiliza zangu hoja
kitu nachotaka baba, ninahitaji kusoma

wala 'sinipe kibaba, na shamba la kulima
eti unipe mbaba, na ndoa ya mapema
so niishie la saba, itanikuta nakama
kitu nachotaka baba, ninahitaji kusoma

sitaki watu kukaba, wala kwa watu kulima
eti mbeba kiroba, na kuwa mtu wa njama
sitaki kuwa kahaba, niwe wa nyumbani mama
kitu nachotaka baba, ninahitaji kusoma

sihitaji lako shamba, na mbuzi wako bandani
wala usinipe mavumba, sivitaki asilani
ukitaka mi kutamba, nipeleke tu shuleni
kitu nachotaka baba, ninahitaji kusoma

elimu kiniachia, kamwe haitaondoka
pesa zitaniishia, naweza kufirisika
mbuzi wataniibia, mashamba yatauzika
kitu nachotaka baba, ninahitaji kusoma

baba yangu mi mwanao, naomba nisikilize
sitaki yako makao, na tena usipuuze
shika nisemayo leo, kwenye kichwa uyatunze
kitu nachotaka baba, ninahitaji kusoma

niache tu napambana, baba nipe mahitaji
utafanya cha maana, utakuwa mwekezaji
vilabuni utajivuna, hawatakunywa maji
kitu nachotaka baba, ninahitaji kusoma

niweze jitegemea, nifanikiwe chuoni
utapata manufaa, utajua tu mbeleni
ufukara kuzuia, kuondoa maishani
kitu nachotaka baba, ninahitaji kusoma

kama kweli wanipenda, elimu weka ya kwanza
iwe moshi na mpanda, na usukumani mwanza
popote nitakapoenda, elimu itanitunza
kitu nachotaka baba, ninahitaji kusoma

baba leo ukienda, kwa Mungu kitangulia
malengo niliyounda, nani tanitimizia
sio nasema napenda, hebu jaribu fikiria
kitu nachotaka baba, ninahitaji kusoma

basi niachie mali, mbayo haiathiriwi
mali hiyo ni daftari, mali hiyo hailiwi
hii ni kubwa siri, wengi wao hawajuwi
kitu nachotaka baba, ninahitaji kusoma

leo hapa naishia, siwezi kuendelea
ukweli nimekuambia, ujumbe mekufikia
baba nakutegemea, elimu yangu simamia
kitu nachotaka baba, ninahitaji kusoma
 
Back
Top Bottom