Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,352
- 15,876
Shughuli hiyo ilifanyika mnamo Juni 18, 2026, katika Kisiwa cha Gana kilichopo Kijiji cha Kamasi, Kata ya Ilangala, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kulinda rasilimali za Ziwa Victoria.
Cde. Ngubiagai amesisitiza umuhimu wa jamii kuachana na mbinu haramu za uvuvi zinazoharibu mazalia ya samaki.
Kiongozi huyo amewahimiza wananchi kuongeza thamani ya mazao ya samaki kupitia usindikaji na uhifadhi bora badala ya kutegemea mauzo ya samaki pekee.
Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Vicent Mbua amewapongeza wananchi na wajumbe wa kamati kwa ushirikiano wao wa dhati, hatua ambayo inachochea ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo katika ushiriki wa zoezi hilo.
Amesema, ili kukuza mapato ya halmashauri, kila mvuvi azingatie sheria na wajibu wake kwa kuvua samaki na dagaa kwa nyavu zinazostahili.
Amesema "Kila mvuvi azingatie sheria zinazomuongoza katika utekelezaji wa majukumu yake, sisi kama halmashauri, tutaendelea kudhibiti uvuvi haramu ambao unaondoa na kuua masalia ya samaki kwa kiwango kikubwa, jambo ambalo litatukosesha mapato na wananchi kukosa samaki bora."
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Vicent Mbua akizungumza na wananchi wa Gana kuachana na uvuvi haramu.
Katika ripoti yake ya utekelezaji, Katibu wa Mwalo wa Gana, Bwana Charles Gunda amebainisha kuwa zana zilizoteketezwa zinajumuisha timba pisi 1627 na nyavu za makira inchi 3 pisi 80.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ilangala, Petro Majura ametoa onyo kwa yeyote atakayeendelea kujihusisha na uvuvi haramu kuwa mkono wa sheria hautasita kuchukua mkondo wake.
Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo, na Uvuvi, Godfrey Ayako, amethibitisha kuwa serikali imejipanga kutatua changamoto ya upimaji wa mizigo ya dagaa ili kukuza sekta ya uvuvi.