Hakubadiliki kitu kwa sababu wahusika wametiwa upofu. Wanaamini kwa vile wamefanya uovu mwingi huko nyuma, na hakuna aliyewahi kuwagusa, basi itaendelea kuwa hivyo hivyo. Wasichokijua ni kuwa wanaweza kubananishwa katika nyakati wasizozitarajia. Na hali hiyo imewahi kutokea kwa wengi.
Kule Liberia, Samwel Doe aliwahi kuwatesa na kuwaua watu wengi, hakuamini kuna mtu atakayeweza hata kumgusa, lakini wakati alipoamini amejiimarisha ndipo walioumizwa walipoinuka, hata hakuamini waliokuwa wanamlinda wameenda wapi, alikimbia kwa miguu kwenda mashambani, ambako nako alikamatwa na kutandikwa na kila aliyetaka. Baadaye aliwekwa juu ya kichanja cha mahindi, kila aliyetaka kumfanya chochote aliruhusiwa, wapo waliomfinya, waliomtandika makofi, waliomtemea mate, na wengine waliamua kumvua nguo zote na kumbakiza kama alivyozaliwa, mwingine akaona wanamchelewesha, akamtandika na jiwe kichwani, akapoteza uhai, waliokuja baadaye wakawa wanachukua tu picha mbalimbali za maiti iliyoachwa utupu.
Hata uwe na nguvu kiasi gani, kinachoweza kukuhakikishia mwisho wa maisha yako, ni kutenda haki. Ukiwa mtenda haki, hata watu wakaudhulumu uhai wako, bado kuna wengi watauheshimu na kuukumbuka mwisho wako kwa kumbukumbu iliyo njema itakayovifanya vizazi vyako viendelee kupendwa na kuheshimika.