Wafuasi wa Ponda jela
Ijumaa, Machi 22, 2013 05:46 Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
*Ni kwa kuandamana kwenda kwa DPP kulazimisha Ponda apewe dhamana
*Yeye aendelea kujitetea mahakamani Kisutu, adai hakuchochea Waislamu
MAHAKAMA jijini Dar es Salaam imewahukumu kifungo cha miaka mitatu jela kila mmoja, watu 54 walioandamana kwenda kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) wakitaka Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda aachiwe kwa dhamana.Hukumu hiyo iliyotolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu Sundi Fimbo, kwa Salum Makame na wenzake 53 baada ya upande wa mashtaka na utetezi kufunga ushahidi mwanzoni mwa wiki.
Ponda na wenzake wanakabiliwa na mashtaka ya kuingia kwa nguvu, kujimilikisha uwanja wa Markaz uliopo Changombe na kuiba vifaa mbalimbali vya ujenzi vyenye thamani zaidi ya Sh milioni 59, mali ya Agritanza Limited.
Kesi dhidi ya Ponda na wenzake inaenedelea kusikilizwa katika Mahakama hiyo ya Kisutu wakati Ponda akiwa mahabusu baada ya kunyimwa dhamana.
Akisoma hukumu dhidi ya watu hao 54 jana, Hakimu Fimbo alisema, Upande wa mashtaka ulileta mashahidi 10 mahakamani, mashahidi walitoa ushahidi wa kuonyesha kwamba washtakiwa walikula njama kutenda kosa la kuandamana, walikusanyika na kufanya maandamano, walikaidi amri halali ya polisi iliyowakataza kufanya hivyo na shtaka la mwisho ni kwa ajili ya mshitakiwa wa kwanza hadi wa tatu ambao wanadaiwa kufanya uchochezi.
Katika shtaka la kula njama upande wa mashtaka umethibitisha bila kuacha shaka kwamba washtakiwa walikutana, wakakubaliana kufanya maandamano hivyo mahakama inawatia hatiani kwa kosa hilo.
Shtaka la pili la kukusanyika na kuandamana pia limethibitika ingawa washtakiwa walijitetea lakini utetezi wao ulikuwa unajikanganya hivyo mahakama inawatia hatiani kwa kosa hilo.
Mahakama iliangalia ushahidi kwa kosa la tatu la kukaidi amri halali ya polisi na imeona kwamba washtakiwa walipeleka maombi ya kufanya maandamano ya amani.
Polisi waliyazuia kwa sababu hawakuwa na polisi wa kutosha lakini maandamano hayo yalifanyika baada ya kutoka msikitini kama barua yao ilivyokuwa ikijieleza
shtaka hilo limethibitika nawatia hatiani washtakiwa wote.
Hakimu Fimbo alisema kwa shtaka la nne la uchochezi washtakiwa hawana hatia kwa sababu upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha shataka bila kuacha shaka.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Ladislaus Komanya uliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa washtakiwa kwa mujibu wa sheria.
Hakimu Fimbo akisoma hukumu alisema kwa kosa la kwanza la kula njama washtakiwa watakwenda jela mwaka mmoja, shtaka la pili pia watakwenda jela
mwaka mmoja na shataka la tatu watatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela.
Adhabu hiyo itakwenda kwa pamoja na kama kuna mshtakiwa anaona hakutendewa haki anaruhusiwa kukata rufaa, alisema Hakimu fimbo.
Washtakiwa walikamatwa Februari 15 mwaka huu na kufikishwa mahakamani wakituhumiwa kufanya maandamano haramu.
Wakati huohuo, KATIBU wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Ponda Issa Ponda amedai kwamba hajawachochea Waislamu kuvamia kwa nguvu uwanja wa Markaz ulioko Changombe.
Alidai mijadala yake na polisi ilianza tangu enzi za uongozi wa Hayati Mwalimu Nyerere.
Ponda alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Victoria Nongwa akiongozwa na Mawakili wake, Juma Nassoro na Yahya Njama.
Ponda na wenzake wanakabiliwa na mashtaka ya kuingia kwa nguvu, kujimilikisha uwanja wa Markaz Changombe na kuiba vifaa mbalimbali vya ujenzi vyenye thamani zaidi ya Sh milioni 59, mali ya Agritanza Limited.
Kwa mujibu wa Ponda, yeye na wezake, walifika katika uwanja wa Markaz Changombe kwa ajili ya kujenga msikiti wa muda kwa ridhaa ya Agritanza Limited ambaye pia alichangia Sh 500,000.
Tulitumia diplomasia kumaliza mgogoro wa uwanja baada ya kusikia Agritanza walibadilishana na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA)
tulikuna na Hafidh Suleiman wa Agritanza tukazungumza na kukubaliana ndani ya siku saba tuwatafutie uwanja mwingine Mkuranga, na eneo la Markaz tuendelee kujenga msikiti wa muda.
Tulikubali kutafuta eneo tukifikiria kutatua mgogoro, taarifa za kujenga msikiti wa muda tulizitoa misikitini na waumini walijitokeza kwa wingi kwa nyakati tofauti kwa ajili ya kushiriki ujenzi,alidai Ponda.
Alidai ujenzi ulifanyika kuanzia Oktoba 12 na kumalizika Oktoba 14 mwaka jana na kwamba ujenzi huo ulikuwa unafanyika asubuhi hadi jioni na kuondoka.
Ponda alidai wakati washtakiwa wengine wakikamatwa hakuwapo eneo hilo lakini alisikia walikuwapo waumini ambao walifika eneo hilo kwa ajili ya kufanya ibada ya Itikafu.
Shtaka la wizi hilo halipo kwa sababu hata Suleiman alipofika mahakamani alidai hakukuwa na wizi. Ili kuthibitisha huo wizi Jamhuri ilitakiwa kutumia busara kwa kuhamisha mahakama hadi eneo la tukio kisha Agritanza waangalie matofali yaliyoibwa kwao na kujengewa msikiti wa muda ni yapi.
Suala la kuingia kwa nguvu katika uwanja wa Markaz halipo. Tuliingia vizuri, kila mtu aliruhusiwa kuingia, hakuna aliyekataliwa kuingia katika eneo hilo na kushiriki ujenzi,alidai Ponda.