Wakati wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wakiendelea na pilikapilika zao za kila siku, hali ya ulinzi na usalama imeimarishwa katika maeneo mbalimbali, huku askari wa Jeshi la Polisi wakionekana kufanya doria na kuweka ulinzi katika vituo na makutano muhimu ya barabara.
Mwananchi imezunguka maeneo mbalimbali ya jiji na kushuhudia askari wakiwa wamepangwa katika vikundi kwenye vituo vya mabasi ya mwendokasi na makutano ya barabara zinazoelekea katikati ya jiji, ikiwemo Mtoni kwa Azizi Ally, Tazara, Buguruni, Uhasibu, Ubungo, Mwenge, Magomeni, Mnazi Mmoja na Fire.
Mbali na askari waliokuwa na silaha, wengine walionekana wakiwa wamevalia vifaa vya kutuliza ghasia, huku magari ya polisi ya kuwatawanya waandamanaji (maarufu washawasha) na magari ya doria yakizunguka kutoka eneo moja hadi jingine kama sehemu ya kuimarisha usalama.