Kwa niaba ya The Civic United Front (CUF Chama cha Wananchi), ninatoa mkono wa pole kwa kifo cha ghafla ya msomi wetu, Profesa Haroub Othman wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kilichotokea asubuhi hii mjini Zanzibar.
Binafsi nimeshtushwa sana na kifo hiki ikizingatiwa kwamba ni jana tu Prof. Haroub alishiriki katika uzinduzi wa kitabu kinachokhusu maisha yangu katika harakati za siasa za Zanzibar na akafanya uhakiki wa kitabu hicho. Huu ni ushahidi kwamba hata katika saa zake za mwisho, Profesa Haroub alikuwa anafanya kazi zake za kisomi, kwani huyu alikuwa ni msomi hasa aliyeuvaa usomi wake kwa kila hali na mali.
Kwa kuondokewa na Profesa Haroub, chuo chake, Zanzibar, Tanzania, Afrika na ulimwengu kwa ujumla, tumeondokewa na hazina kuu ya elimu na maarifa ya siasa na sheria. Tumeondokewa na mchambuzi wa historia. Mchango wake utakumbukwa daima katika masuala kadhaa ambayo aliyasimamia, kuyachambua na kuyawekea misimamo, likiwemo suala la haki za binaadamu na sheria, Zanzibar, kufikia hadi kuanzisha kituo cha kwanza cha Haki za Binaadamu na Sheria visiwani humu na pia kuendeleza ile azma ya Afrika Moja kama ilivyoanzishwa na waasisi wake, Dkt. Kwame Nkrumah, Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wengine wa ukombozi wa Bara la Afrika. Kwa hakika, Profesa Haroub ameishi maisha yake kwa ukamilifu!
Sisi, katika CUF, tunamuomba Mwenyezi Mungu ampokee akiwa amemsamehe makosa yake na aufanye mwema ujira wake. Tunaungana na familia ya marehemu, jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Wazanzibari, Watanzania na Waaafrika wote katika wakati huu mgumu wa maombolezo.
Mwenyezi Mungu aipe familia ya marehemu nguvu na subira za kuweza kukabiliana na msiba huu. Amin!
Innalillahi wainna ilayhir raajiun. Sisi sote ni wa Mwenyezi Mungu na Kwake tutarejea!
The Civic United Front (CUF Chama cha Wananchi)