WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema Bajeti ya mwaka 2025/2026 kipaumbele kikubwa kitakuwa ni utekelezaji wa miradi mikubwa kwa ushirikiano na Sekta Binafsi na Umma (PPP), ili kukuza uchumi kwa kasi.
Prof. Kitila Mkumbo, amesema hayo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bajeti ya Bunge ambapo amenukuu kanuni ya 113(1) na (2) ya kanuni za kudumu za Bunge iliyochapishwa Februari 2023, ambapo mapendekezo hayo yanawasilishwa kwa kamati ili kukusanya maoni kutoka kwa wabunge wakati wa maandalizi.
Amesema Serikali imejipanga kutumia mfumo wa PPP katika utekelezaji wa miradi mikubwa, hivyo katika bajeti ijayo wataweka nguvu huko kibajeti.
"Katika mwaka wa fedha 2025/26 kipaumbele cha bajeti kitaelekezwa kwenye PPP kwani ndio njia inayoweza kutekeleza miradi mikubwa inayochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo," amesema.
Amesema mapendekezo hayo yameweka mazingira ya mpango wa maendeleo wa taifa, unaozingatia kuimarisha uwekezaji katika sekta mbalimbali, kujenga uchumi imara, kuongeza uzalishaji wa viwanda na kuboresha huduma za umma.
“Mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa taifa wa 2025/26 yanaongozwa na dira ya maendeleo ya taifa 2025, ambayo inalenga kuiweka Tanzania kati ya nchi za kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 na kufikia viwango vya juu vya maendeleo ya binadamu,” amesema.
Soma Pia: Miradi ya PPP iliyopo katika tovuti ambayo yahitaji wawekezaji wa nje, kwanini wawekezaji wakimbilia Tanesco pekee ambayo haimo hata kwenye orodha?
Waziri Kitila amesema mapendekezo hayo yanajikita katika kuendeleza na kutekeleza mipango ambayo inatoa matokeo katika maeneo matano ya kipaumbele yaliyoainishwa katika mpango wa tatu wa miaka mitano.
Pia ametaja maeneo muhimu ambayo yatatekelezwa kwa mfumo wa PPP ni miundombinu ya usafiri na uzalishaji wa viwanda.
Amongeza kuwa jumla ya miradi 17 bora imepangwa kutekelezwa katika mwaka ujao wa fedha, huku akibainisha mafanikio kutoka kwa mpango wa sasa wa maendeleo wa 2023/24.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Oran Njeza ameipongeza serikali kwa kuja na mpango huo na kwamba matarajio yao ni kuona miradi inatekelezwa kwa ufanisi.
PPP iliyochini ya kituo cha Ubia nchi PPP-CETRE chini ya Mkurugenzi wake Bw David Kafulila na katika Serikali ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan wameonesha wazi nchi inaweza kutekeleza miradi mingi na mikubwa bila kutumia Kodi Wala Mikopo toka katika taasisi na mashirika tofauti tofauti ya ndani na nje ya nchi kwenye miradi hasa yenye sura ya kibiashara na hivyo kuopa nafuu nchi kutekeleza miradi mingine isiyo na sura hiyo ya kibiashara.