Mbunge alieteuliwa na Rais Magufuli mapema leo tayari amekula kiapo mbele ya Spika Ndugai kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Prof. Manya anatarajia kuapa tena baadae leo kuwa naibu waziri wa Nishati na madini.
Baada ya kuapa kama Mbunge, Prof. Manya alitoa neno la shukraan
Prof. Manya: Kwanza kabisa napenda kumshukuru mwenyezi Mungu ambae yeye ndie hupanga majira na nyakati katika maisha ya wanadamu. Nasema hivyo kwa sababu Ijumaa inakuwa safari yangu ya mwanzo mpya ambao sikupanga mimi, majaliwa ya Mwenyezi Mungu.
Pili nipende kumshukuru mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa heshma aliyonipa ya kuniteua kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania, ninapenda tu kusema kwamba, nitafanya majukumu yangu ya ubunge kwa uadilifu ili kwamba kwa pamoja tuweze kulisukuma gurudumu la maendeleo la nchi yetu na Taifa letu na tukimtanguliza Mwenyezi Mungu, asanteni sana.
SPIKA JOB NDUGAI: Kama nilivyoeleza mapema, sisi kama Bunge hatupendi kuwa kikwazo, lazima tuendane na Serikali yetu na Spidi ya Awamu ya Tano na ndio maana tukayafanya mambo tukikimbia pamoja. Nitoe wito kwa wabunge wengine wowote wale, nafikiri kumbukumbu zangu zinaonyesha tuna wabunge wa ACT-Wazalendo wanne ambao bado hawajaapa, napenda kutoa wito wakiwa tayari kutumikia nchi yao kama kweli waliomba ubunge kutumikia wananchi hawana sababu za kuendelea kuzurula huko waliko.
Watoe taarifa kwa spika haraka, tuwapangie ili wapate kiapo waweze kufanya kazi ya mbunge kama ambavyo wananchi waliwaamini, nadhani ni watatu.