Treni iliyobeba wanajeshi na vifaa vya Urusi imewasili Belarus huku kukiwa na wasiwasi kwamba Moscow inaweza kutumia eneo la mshirika wake kushambulia Ukraine kutoka kaskazini.
Wizara ya ulinzi ya Belarus ilithibitisha kuwasili kwa kikosi hicho siku ya Ijumaa na kusema kuwa Rais Alexander Lukashenko alikuwa ametembelea kambi ya kijeshi ambapo tayari wanajeshi wa Urusi wameweka kituo.
Wakati wa mkutano huo, Lukashenko na mwakilishi ambaye hakutajwa jina kutoka kwa jeshi la Urusi walijadili mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya nchi hizo mbili, ilisema taarifa. Vikosi vya Urusi "viko tayari kufanya kazi kama ilivyokusudiwa", mwakilishi huyo alisema.
Haya yanajiri baada ya Belarus, ambayo imeunga mkono Urusi kuhusu vita vyake nchini Ukraine, kusema siku ya Alhamisi kwamba itapokea silaha zaidi na vifaa kutoka kwa jirani yake huku wawili hao wakiendelea kuimarisha ushirikiano wa kijeshi.
Wizara ya ulinzi ya Belarusi ilisema lengo la kuunda kikosi cha pamoja ni "kuimarisha ulinzi wa Jimbo la Muungano [Russia na Belarus]". "Wafanyikazi, silaha, kijeshi na vifaa maalum vya jeshi la Shirikisho la Urusi vitaendelea kuwasili katika Jamhuri ya Belarusi," ilisema taarifa hiyo. Nchi hizo mbili zinajiandaa kwa mazoezi ya pamoja ya jeshi la anga, wizara ilisema, bila kutoa maelezo zaidi.
Serikali ya Belarusi imesema mara kwa mara nchi hiyo haitajiunga na vita vya Urusi nchini Ukraine. Lakini Moscow ilipeleka maelfu ya vikosi katika eneo la Belarusi kwa kisingizio cha mazoezi ya kijeshi kabla ya kuzindua mashambulizi yake na kisha kuwaingiza wanajeshi Ukraine wakati uvamizi wake ulipoanza Februari 24.
Kwa mujibu wa Kyiv, Urusi inaendelea kutumia anga ya Belarus kwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora.
Shambulio lolote jipya dhidi ya Ukraine kutoka Belarus litafungua mkondo mpya katika vita hivyo, ambavyo vimeua makumi ya maelfu ya watu.
Lukashenko ameyalaumu mataifa ya Magharibi kwa vita hivyo akiyashutumu kwa kutaka makabiliano na Urusi na kuchochea umwagaji damu unaoendelea.
Marco Polo Russia will never back down NEVER!!!!