Nimefuatilia mjadala huu na kusoma kila post moja moja na kuna hoja nyingi na za msingi. Naomba, niseme machache kuhusu mada nzima katika maudhui yake.
a. Uongozi wa Taifa ni jambo nyeti.
Kuongoza Taifa siyo sawa na kuongoza chama, familia, biashara, au klabu fulani ya watu. Si sawa hata kidogo na jambo jingine lolote ambalo mtu hata awe na sifa zipi, elimu ipi, kipaji cha namna gani, anaweza kuandaliwa kwacho. Hivyo, hakuna mtu mwenye qualification rasmi ya kumuwezesha kuwa Rais ambayo ukiingalia unaweza kuhisi kuwa atakuwa Rais mzuri au mbaya. Hakuna.
Kuwa na shahada za udaktari na kuwa mwaminifu katika ndoa siyo guarantee kuwa mtu atakuwa kiongozi mzuri wa Taifa, kuwa tajiri au maskini haiwezi kuhakikisha Rais atakuwaje n.k So, kwa wale wanaojaribu kuangalia mtu sifa zake na kujaribu kuprejudge kuwa atakuwa Rais mzuri au mbaya wana overestatement their own assumptions.
b. Uongozi wa Taifa ni uongozi wa ukingano
Kuongoza Taifa ni kuongoza vitu vinavyokinzana; maslahi yanayogongana, na matamanio yanayogongana. Kuongoza watu wenye maslahi tofauti, hamu tofauti, na mitazamo tofauti ili kuweza kufikia lengo moja si jambo rahisi. Kuna maslahi ya makampuni, maslahi ya taasisi binafsi, maslahi watu binafsi, maslahi ya viumbe vingine nk
Hivyo yeyote mwenye jukumu la kuwa Rais anakabiliwa na mgongano usiokwepeka na kazi yake kubwa ni kuhakikisha kuwa maslahi yote yanapata nafasi kwa kiwango kikubwa bila kugonganisha maslahi ya watu wengine au vyombo vingine. Hivyo, kama nilivyosema kwenye (a) hakuna anayeandaliwa kwa hilo.
Mfanyabiashara kama Mengi, Waziri kama Mkapa, Waziri kama Kikwete, Mwalimu kama Mwinyi, Mwalimu kama Nyerere hakuna aliyeandaliwa kushika nafasi hiyo.
c. Uongozi wa Taifa ni mzigo usiotafutwa
Hakuna mwenye haki ya kuwa kiongozi wa Taifa na tuwaogope sana watu wanaotafuta nafasi ya kwenda Ikulu. Nikiwa mwanafunzi mzuri wa Mwalimu naamini kabisa kuwa Ikulu si mahali pa kutafutwa. Na hasa siyo mahali pa kutafutwa kwa "udi na uvumba". "Kuna nini Ikulu?" ni swali ambalo kila mwenye kutamani nafasi hiyo lazima ajiulize.
Hofu yangu ni kuwa Ikulu pamegeuzwa kuwa kisima cha faida, na chimbuko la Biashara. Nyerere pamoja na mapungufu yake mengi ambayo yamesemwa sana, alijaribu sana kuiheshimu Ikulu. Ni wale waliokuja baada yake ndio wamegeuza nyumba hiyo kuu ya watanzania kuwa genge la biashara na kitovu cha ufisadi.
Hivyo binafsi naogopa kabisa na kutetemeka nikisikia mtu anataka kwenda Ikulu au anataka Urais kwani najiuliza kwanini? Hilo peke yake halinitishi sana lakini inapotokea mtu anatumia mbinde kupata nafasi hiyo basi hofu yangu ya mtu huyo inaongezeka mara 180!
Mtu mwenye akili timamu hatamani kubebesha mzigo huo; mzigo huo atabebeshwa kwa kuombwa na watu wenyewe, hautafuti.
d. Uongozi wa Taifa humbadilisha mtu
Kama kuna kitu cha ajabu kinachotokea kwenye Urais ni kuwa una nguvu ya kumbadilisha mtu kwa uzuri au kwa ubaya. Na hapa si urais wa Tanzania tu bali uongozi wa nchi yoyote ule; unaweza kumfanya mtu awe "mwokozi" au "mwovu".
Kile ambacho kinajulikana sana kama "trappings of power" ni kitu kikubwa sana ambacho kinaweza kumfanya mtu mwadilifu kugeuka na kuwa fisadi numero uno. Mtu anapojua ana nguvu fulani au uwezo fulani kama yeye mwenyewe hana proclivities of humility basi mtu huyo ni rahisi sana kupotea katika saluti, ving'ora, makofi, na shangwe.
Lakini uongozi huo huo unaweza kumgeuza mtu dhaifu na mwoga kuwa shujaa, na asiyeweza kusema kuwa msemaji wa ajabu. Urais haujaribiwi kama kwa mtihani wa Mock na kuona kama mtu atafanya vizuri kwenye mtihani kamili. Mtu ambaye anaweza kufeli Mock ukashangaa ukija mtihani wenyewe akapasua vile vile na yule aliyedhaniwa kuwa "kinara" akaanguka.
Sidhani siko peke yangu katika kumjua mtu ambaye darasani kuanzia form one hadi form four alikuwa kati ya mtu wa kwanza na wa tatu, na hata wakati wa mtihani wa Final alikuwa anawaandaa wanafunzi wenzie kusoma na alikuwa msaada sana.
Matokeo yanapokuja mnaweza kupigwa na mshangao kuwa wale wote aliowasaidia wanatoka na Division 1 na 2 halafu yeye anatoka na division three au hata four na hakuna kiumbe duniani kinachoweza kuelezea hilo. Kwa mtu ambaye anaangalia maisha ya nyuma angeweza kutabiri kuwa mtu huyo angetoka na daraja la kwanza la point 7! Lakini matukio ya mtihani na majaribio ya wakati yalimbadilisha.
Kwa maneno mengine, Rais mzuri hajulikani nje ya Urais na Rais mbaya hajulikani nje ya Urais. Tunaweza kuhisi tu itakuwaje lakini kuhukumu by proxy haiwezekani. Kwa hili niko very pragmatic.
Nitawapa mfano; Rais Luiz lula da Silva wa Brazil si msomi wa aina yoyote na maisha yake yamezungukwa na mambo mengi ikiwemo kuzaa nje ya ndoa. Kati ya kazi alizowahi kufanya ni pamoja na ufundi viatu na umachinga (street vendor). Lakini leo hii kutokana na mang'amuzi yake ya maisha na kujifunza kwa makosa amekuwa Rais wa Brazil na sasa yuko katika kipindi chake cha pili, huku uchumi wa Brazili ukikua kwa kasi, akilipa madeni ya IMF miaka miwili mbele, na akiliongoza Taifa lake kuelekea kwenye anga za juu!
Yote hayo yamefanywa na mtu ambaye kwa kwa kuangalia tu maisha yake ya nyuma tunaweza kusema ni failure, si msomi, si mwaminifu katika ndoa yake, na kwa hakika uongozi wake wa chama cha wafanyakazi si kigezo cha kutosha.
On the other hand however, kuna mfano wa Rais Chiluba wa Zambia. Kwa namna yoyote ile ni mtu ambaye ilikuwa rahisi kuamini kuwa atakuwa Rais. Amejisomesha mwenyewe kwa njia ya correspondence na kushika nafasi mbalimbali , kutiwa kizuizini na Kaunda n.k Na yeye naye akawa na kashfa za ngono vile vile. Kwa wengine alionekana ni Mlokole (Nakumbuka niliwahi kumuona kwenye programu ya TBN some years back). Lakini alipotoka ndiyo siri yake ikajulikana, alikuwa ni fisadi tu kwani madaraka yalimbadilisha au alikubali kubadilishwa na madaraka.
e. Uongozi wa nchi ni utumishi.
Kiini cha Urais ni kuelewa, kukubali, na kupokea pasipo utata kuwa uongozi wa nchi ni utumishi kwa Taifa. Anayetaka kuwa kiongozi wa Taifa au anayedhaniwa kuwa anapaswa kuwa kiongozi wa Taifa ni lazima hili lieleweke kwake. Kama mtu anataka kuwa kiongozi ili amalizie miradi yake na ya rafiki zake, au anataka kuwa kiongozi ili alipize kisasi, au anataka kuwa kiongozi ili apigiwe saluti au kukata tepe za ufunguzi huyo mtu hatufai!
Tunataka mtu ambaye kitu pekee na pekee kinachomsukuma kukubali ombi la wananchi wenzake kuwa kiongozi ni utumishi kwao. Nje ya hapo hakuna kigezo kingine kinachomfaa mtu kuwa kiongozi.
f. Uongozi ni timu
Nimetolea mfano wa Lula hapo juu, ukweli ni kuwa mafanikio yake yanatokana na timu aliyojizungusha nayo. Kiongozi mzuri ni yule anayejua mapungufu yake na akayaziba kwa kuweka watu ambao watafanya kile ambacho hana ujuzi au ufundi nacho. Kiongozi mzuri asingemteua Mramba kuwa waziri wa Viwanda au Msolla kuwa waziri wa Elimu ya Juu! Kiongozi mzuri hawezi kumrudisha Wassira kwenye Kilimo wakati taifa linakabiliwa na njaa, na kwa hakika kiongozi mzuri asingeweza kumuweka Lowassa katika nafasi yake.
Hata hivyo, kiongozi mzuri ni yule anayetambua makosa yake na kuyasahihisha.
g. Uongozi ni uadilifu siyo ukamilifu
Mojawapo ya mitego tunayoingia ni ya kujaribu kumtafuta mtu mkamilifu kuliko wote ndiye atufaye kuwa kiongozi wetu. Tunapoangalia maisha ya watu mbalimbali tunajikuta tunakatishwa tamaa kwani mtu anaweza kuwa msomi lakini mtongozaji mno, anaweza kuwa na kipaji sana cha kuzungumza lakini dhaifu, anaweza kuwa tajiri sana lakini si mwanasiasa, n.k n.k Yaani tunajikuta kila tunayemwangalia kwa ukaribu tunajikuta ana mapungufu kibao.
Mwisho tunaanza kuwa kama watu wanaotaka kumla bata, aidha umnunue na kumshughulikia lakini usiende sana kumtafuta kila anachokula na wapi anakunywa maji, vinginevyo hutamla. Tunapowaangalia wanasiasa wetu kuna mambo hatuna budi kuyaweka mbele na mengine kuyaweka nyuma.
Madai ya mtu kutokuwa mwaminifu kwa ndoa yake ni dogo sana ukilinganisha na mtu ambaye siyo mwaminifu kwa fedha za umma. Hakuna direct relation yoyote ile kati ya nani mtu analala naye kitandani na nini mtu anafanya ofisini. Je wezi wote wa fedha za umma ni malaya? Je wale wote wanaofanya ubadhilifu kwenye mashirika na taasisi zetu wana vimada au wanaenda nje ya ndoa zao? Je wala rushwa wote ndoa zao zimevunjika?
Tunachohitaji ni mtu mwadilifu na si mkamilifu. Mtu mkamilifu hayupo duniani lakini mwadilifu tunaweza kumtafuta na kumpata. Mkamilifu hafanyi makosa, mwadilifu hutambua makosa; mkamilifu hasemi uongo, mwadilifu anagundua uongo wake na kuusahihisha; mkamilifu hatamani utajiri wa bure, mwadilifu anatamani utajiri lakini anataka kuufanyia kazi; mkamilifu hatamani kiwowo cha pembeni mwadilifu anakitamani na anakikwepa; mkamilifu hapotezi hata senti moja ya fedha za serikali, mwadilifu anagundua amepoteza fedha na halali hadi ajue ziko wapi na zinarudi; mkamilifu haogopi kufanya kitu kwani anajua atakachofanya kitakuwa kizuri na kitapendwa, mwadilifu anaogopa kufanya kitu hivyo anapima na kuchagua kilichokizuri na anatumaini kitapendwa. Mkamilifu anapatikana mbinguni, mwadilifu anapatikana duniani.
h. Uongozi ni hulka kama ya simba
Niseme mwisho kwamba, uongozi wa Taifa ni kwa mtu mwenye hulka (instinct) kama za simba. Hauna elimu lakini huna instinct ya mwindaji. Hakuna mtu anayeweza kumfundisha simba kuwinda isipokuwa instinct zake zinaandaliwa pole pole na asili na matukio. Simba hata umtunze peke yake zile instinct zake hazifi.
Kiongozi wa Taifa anatakiwa awe na hizo zinazojulikana kama "killer instinct" asiyekuwa nazo hafai kwani hatojua ni wakati gani wa kuunguruma kwa tishio, ni wakati gani wa kunoa kucha zake na kutuma ujumbe "don't play" na pia ni wakati gani wa kuvamia na kurarua!
Ni kwa sababu hiyo basi walioandika Katiba yetu waliamua kuja na sifa chache tu za mtu anayeweza kuwa Rais. Wao wakasema hivi kuwa mtu hatokuwa na sifa za kugombea Urais isipokuwa kama:
a) ni raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano kwa
mujibu wa Sheria ya Uraia.
(b) ametimiza umri wa miaka arobaini;
(c) ni mwanachama, na mgombea aliyependekezwa na
chama cha siasa;
(d) anazo sifa za kumwezesha kuwa Mbunge au Mjumbe
wa Baraza la Wawakilishi,
(e) katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya
Uchaguzi Mkuu hajawahi kutiwa hatiani katika
Mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kulipa
kodi yoyote ya Serikali.
kwa msingi huo basi, tunapomuangalia Mengi au mtanzania mwingine yeyote tujiulize je anatimiza sifa hizo? Nje ya hapo ni kujiumiza kichwa kusiko kwa lazima kwani mengine ni sifa za kututuliza akili tu na kutufanya tuwe na hisia ya kuwa salama kwa vile mgombea wetu "ni msomi, anaenda swala au kusali, ana pesa nyingi, ana mvuto, anapenda kucheka cheka n.k".
Hiyo inatosha kwenye somo la Uongozi wa Taifa.