JUZI Rais John Magufuli alikuwa mtu wa kwanza kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda la kuhakiki silaha, ambapo bunduki zake mbili aina ya shotgun na bastola zimehakikiwa Ikulu, Dar es Salaam.
Uhakiki huo uliogeuka gumzo na jana picha zake zipamba vyombo vya habari nchini, ulifanywa na maofisa wa Jeshi la Polisi wakiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa uhakiki huo, Rais Magufuli alimpongeza Makonda na Jeshi la Polisi kwa kuendesha kampeni ya uhakiki wa silaha, huku akitoa mwito kwa watu wote wanaomiliki silaha nchi nzima kuhakikisha zinahakikiwa.
Aidha, Rais Magufuli pia ametaka Jeshi la Polisi kuongeza juhudi za kukabiliana na watu wanaojihusisha na uhalifu ili kutokomeza kabisa vitendo hivyo. Rais Magufuli pia alielezea kushangazwa na vitendo vya askari kunyang’anywa silaha na majambazi, huku mara kadhaa akirudia kusema ‘Ni aibu’.
Alisisitiza lazima wabadilike na kukabili kwa vitendo uhalifu., Tunampongeza Rais Magufuli kwa kuunga mkono kampeni iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ya kuhakikisha kila anayemiliki silaha anaimiliki kihalali.
Kama ambavyo Makonda alieleza wakati akitangaza mpango huo, dhamira ni kuhakikisha vitendo vya uhalifu vinavyotokana na matumizi ya silaha haramu katika Jiji la Dar es Salaam, vinatokomezwa na hatimaye Jiji linakuwa salama kwa raia na mali zao kama ilivyo asili ya jina la Dar es Salaam, yaani Bandari ya Salama.
Hivyo kwa kuwa Rais ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu ameonesha kwa vitendo kuunga mkono utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ni vyema wengine watumie miezi mitatu iliyotolewa na Mkoa kuhakiki silaha zao.
Hatua hii ikifanikiwa, itachangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa matukio ya kihalifu yanayoonekana kuota mizizi kiasi cha majambazi kuvamia popote wanapotaka, hata vituo vya Polisi na kusababisha hofu kuu kwa wananchi.
Ni dhahiri wananchi hujikuta wakikosa majibu na kujiuliza kama Polisi wanavamiwa na kuuawa, hali itakuwaje kwa raia wa kawaida ambao kwa kiasi kikubwa hutegemea ulinzi wa Polisi? Ifike mahali kila mkazi wa Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla, washiriki kikamilifu katika kampeni hii yenye lengo la kudhibiti silaha holela mitaani.
Udhibiti wa silaha una maana kubwa sana kwetu, kwani ni dhahiri matukio ya kihalifu yatapungua na kufanya wananchi wawe huru katika shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo.
Kwa kutambua umuhimu wa utulivu, amani na usalama, tunaamini juhudi za Makonda na Jeshi la Polisi za kutaka kuiona Dar es Salaam isiyo na uhalifu, zikiungwa mkono kama alivyoonesha Rais Magufuli, hakuna kitakachoshindikana.