Tumeisikiliza hotuba ambayo Rais Magufuli ameitoa ya kulivunja Bunge letu na kuwaaga rasmi wabunge wanaporejea kwenye majimbo yao kwenda gombea tena, kwa nia ya kurejea tena kwenye Bunge lijalo
Rais Magufuli ametoa uhakikisho kwa Ulimwengu kuwa tutakuwa na uchaguzi ulio huru na haki.
Hata hivyo kuna tofauti kubwa ya kuutangazia Ulimwengu kuwa tutakuwa na uchaguzi mkuu utakaokuwa wa ihuru na haki na kutekeleza kwa vitendo kuendesha uchaguzi ulio huru na wa haki.
Mazingira ya uchaguzi wetu bado hayatoi matumaini kuwa tutakuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki.
Zipo sababu za kusema kuwa kwa mazingira tuliyonayo, hatutakuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki.
Sababu zangu ni kama hizi zifiatazo:-
1. Kilio cha muda mrefu cha vyama vya upinzani vya uundwaji wa Tume huru ya uchaguzi, inaelekea watawala wetu wameendelea kuziba masikio yao kwa pamba.
Hivi inawezekanaje tuwe na uchaguzi huru na wa haki, wakati mgombea mmojawapo wa Urais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, akiwa ndiye anayeteua Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi na wajumbe wake?
2. Zimelazimishwa kuwekwa kanuni na Tume ya uchaguzi ya Taifa, ambazo zina lengo la kuufanya uchaguzi mkuu usiwe huru na haki
Hivi unawezaje kuwa na chaguzi huru na haki, wakati wasimamizi wa uchaguzi hawatalazimika kuwapa mawakala wa vyama nakala za matokeo?
Kama huo siyo mkakati wa CCM kufanya wizi wa kura, tunaweza kuita hiyo mbinu ya kutotoa nakala ya matokeo kuwa ina nia gani haswa?
3. Hivi Rais kupiga mkwara kuwa hataruhusu matusi kwenye uchaguzi mkuu ujao ina maana gani?
Hivi ni nani atakayeona kuwa lugha hii iliyotolewa kwenye majukwaa ya kisiasa ni matusi au laa?
Je ni Polisi wetu ndiyo watakaoamua kuwa lugha iliyotumiwa kwenye majukwa ya kisiasa ni matusi?
Ninavyojua mimi kwenye siasa za ushindani, ni kushindana kwa hoja kwenye majukwa ya kisiasa na wala hatushindani ubabe!
Chama kimoja kinapotaka kujibu upotoshaji unaofanywa na chama kingine, ni kwa kutumia majukwaa hayo hayo ya kisiasa kujibu hoja hizo na wala siyo kulitumia Jeshi la Polisi kuwanyamazisha na kutumia ubabe kwa kuwaweka ndani viongozi wa vyama vya upinzani, kwa madai kuwa wametumia lugha ya matusi!
Niseme wazi kuwa Rais wetu Magufuli ameshindwa kukabiliana na siasa za ushindani na badala yake yeye amekuwa mtu wa kutumia vitisho kwa kuvitumia vyombo "vyake" vyote vya dola kwa kukandamiza vyama vya upinzani
Kama kweli Rais wetu ana nia ya dhati ya kuufanya uchaguzi ujao kuwa huru na haki, ni kwanini anaziba pamba masikioni, kutotaka kusikia maoni ya vyama vya upinzani, ya kuundwa kwa Tume huru ya uchaguzi, ambayo ni maoni yenye maslahi mapana kwa Taifa letu na yenye kuleta mustakabali mwema kwa Taifa letu?