Kwa nini mnamuita meko? Dikteta uchwara?
Unasema kwa nini huwa tunamwita Dikteta uchwara au Meko - sijui unamaanisha ni nani hao ambao huwa wanamwita hivyo.
Sidhani kama kuna kundi lolote kwa misingi ya aina yoyote, waliwahi kukaa na kukubaliana kuwa Rais Magufuli aitwe Meko au dikteta uchwara. Ndiyo maana hata ukiwatafuta wapinzani au wanaomkosoa Rais Magufuli, wengi sana hawajawahi kumwita kwa majina hayo.
Lakini pia hakujawahi kuwa ns mkutano wa kukubaliana kuwa wanaCCM waitwe mataga au wanaCHADEMA waitwe nyumbu. Lakini pia katika ushindani, jokes na vitimbwi, hunogesha mijadala na upinzani.
Ukiwa kiongozi, huwezi kukwepa majina bandia, mengine ni ya kukukejeli lakini yapo pia kwa nia ya kukusifu.
Mwalimu Nyerere alikuwa akiitwa Mchongameno na majina mengine, lakini la Mchongameno lilifahamika kwa watu wengi. Mwalimu hakuwahi kukataa wala kukubali, na wengine walidhani hajui. Lakini baadaye wapo walianza kumwita Musa, hapo ndipo Mwalimu alipokemea. Kwa maneno yake alisema, 'mmeniita majina mengi, nimekubali. Mnaweza kuendelea kuniita kwa hayo majina, mara mchongameno, na mengine. Lakini hili la kuitwa MUSA, nalikataa'. Mwalimu alijiona hamkaribii kwa namna yoyote ile nabii Musa, aliyewaongoza wana wa Israel kutoka Misri kuelekea nchi ya ahadi.
Mzee Mwinyi alikuwa akiitwa Mzee Ruksa. Wapo waliomwita hivyo kama namna ya kumsifu alileta demokrasia, lakini wapo waliomwita hivyo kumkejeli kama mtu aliyeruhusu mambo yote yafanyike holela. Lakini Mwinyi, siku moja alipohojiwa kuwa anajisikiaje anapoitwa Mzee Ruksa? Alijibu nafarijika sana. "Maana unapita sehemu unaitwa Mzee Ruksa, Mzee Ruksa. Nafarijika kwa sababu wakati ule tulisema watu wasibanwebanwe, wawe huru".
Magufuli aliwahi kutamka mwenyewe kuwa yeye ni Jiwe, wapo baada ya pale wanaomwita hivyo. Wengine kwa kutaka kuonesha ni mtu asiyeyumbishwa, lakini wapo wanaomwita hivyo, wakimaanisha mtu asiyepokea ushauri. Lakini Rais mwenyewe anapoitwa Jiwe, anajisikiaje, hakuna aliyewahi kumwuliza. Hatujui anafurahia au anachukizwa.
Lakini ukiacha hoja za hapo juu, Rais Magufuli huenda ndiye Rais atakayeongoza kwa kuitwa majina mengi bandia. Ukumbuke, mwanzoni mwa utawala wa Rais Magufuli, wapo waliomkosoa Rais Magufuli kwa kumwandika jina lake halisi yaani Rais Magufuli, baadhi ya watu hawa walikamatwa, baadhi waliokuwa na bahati walishtakiwa, wengine mateso waliyoyapitia wanayajua wao. Lakini ikumbukwe mmojawapo alishinda kesi mahakamani kwa vile alimwandika Rais Magufuli kama Magu. Alishinda kwa sababu kisheria Magu, hakuna uthibitisho kuwa ni Rais Magufuli. Hiyo iliongeza sana tabia ya watu kumwita Rais Magufuli kwa majina mbalimbali ili tu kisheria wasionekana wanayemsema ni Rais Magufuli.
Ukitaka jambo liondoke au lipungue, ni watu kuwaacha wawe huru. Anayekosea ashtakiwa kwa kosa alilolitenda na siyo kumbambikia makosa ambayo hakuyatenda. Mtu amemkashfu Rais, halafu anakamatwa, mahakamani anashtakiwa kwa kosa la uhujumu uchumi ili tu akae ndani asipate mdhamana. Mambo hayo yanazidisha chuki na kuongeza lugha zisizo na staha.
Tukubaki tu kuwa Rais kuna wakati, nadhani kwa ghadhabu, anatumia lugha zisizo na staha. Mfano kule Tunduma, mama anamweleza Rais kero ya maji, yeye akamjibu, aende akamwombe mume wake! Jibu kama hilo halijengi mazingira ya chuki na lugha zisizo na staha? Lakini huenda Rais naye, alikuwa tayari ameaudhiwa na mambo mengine, ndiyo maana ile hekima ya uvumilivu ilimwondoka.
Mimi nimewahi kushuhudia, watu wanamwuliza mkuu wa wilaya maswali, mkuu wa Wilaya badala ya kujibu, anaanza kuwatukana waliouliza maswali na kuwaita wapumbavu na kuamuru wawekwe ndani. Kiongozi wa namna hii, nani atamheshimu? Nani atatumia kugha ya heshuma dhidi yake?
Kama tunataka kuanza upya, kila mmoja kuna mahali na namna ya kujirekebisha. Viongozi wawe wa kwanza kuonesha njia kwa kujirekebisha, raia watafuata. Na wale wabishi, watashtakiwa kwa haki kwa mujibu wa sheria kwa makosa yao hakisi waliyoyatenda, na siyo ya kuwatengenezea.
Kuna wakati niliwahi kutamka kuwa, binafsi, kidhamira naweza kupuuza mengi ambayo nahisi viongozi wamekosea (maana nia wao ni binadamu, lazima kuna makosa watafabya), lakini siwezi kuouuza wala kusamehe mambo ya kuteka watu, kuwapoteza, kuwaua, kuwatesa au kuwabambikia kesi. Huo ni unyama na ushetani ambao haustahili kuwepo kabisa katila jamii ya watu waliostaarabika, tena ambao zaidi ya 80% ni watu wanaomjua Mungu kuoitia imani mbalimbali. Nashukuru sana, na ninafarijika sana, kuwa hayo mambo kwa kiasi kikubwa mengine yamekoma, na mengine yamepungua.