Kutoka Zanzibar, maandalizi yameshakamilika kwa ajili ya kumuapisha Makamu wa kwanza wa Rais, Maalim Seif Shariff Hamad kutoka chama cha ACT-Wazalendo. Kuwa nami kukujuza yatakayojiri kutoka visiwa hivi vya karafuu punde kutoka sasa.
PIA, SOMA=> Rais Dkt. Mwinyi amteua Maalim Seif kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
==========
6:00 Mchana: Wageni wameshawasili na anaesubiriwa kwa sasa ni Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi. Miongoni mwa waliofika kwenye hafla hii ni kiongozi mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe pia makamu wa kwanza wa Rais anaesubiri kuapishwa, Maalim Seif.
6:11 Mchana: Rais wa Zanzibar ameingia ukumbini na Maalim Seif amekabidhiwa na kuapa kuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa mujibu wa katiba.
MAALIM SEIF: Mheshimiwa Rais, kwa upande wetu uamuzi wa kuingia katika serikali, baraza la wawakilishi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haukuwa uamuzi rahisi na mwepesi.
Ulikuwa ni uamuzi uliotufikirisha sana, tumejadili sana na tumepishana sana hatimaye tukafikia uamuzi. Moja ya sababu iliyotufanya kufikia uamuzi huo ni imani yetu kwako wewe binafsi, maneno yako, vitendo na ishara zako ambazo zimetushawashi kuwa unayo nia njema na dhamira safi ya kututoa tulipokwama na kuibadilisha Zanzibar yetu katika nyanja zote.
Tumeona wewe ni mtu tunaeweza kufanya nae kazi, tumeweza kusikilizana na tunaweza kukupa nafasi uthibitishe nia yako njema mabyo ndio iliyotufanya sisi tutangulize nchi kwanza licha ya madhila yote yaliyojitokeza katika uchaguzi uliopita.
Wenzangu walipokuja na wazo hili la sisi kuungana na wewe na baada ya kushikiana na wanachama wetu, niliwashauri kuwa sasa ni wakati wangu mimi kupumzika na kupeleka jina la damu mpya, hawakunikubalia, waliniambia wewe ndio ulioongoza maridhiano na Rais Amani Abeid Karume mwaka 2009 na ndie ulishiriki serikali ya kwanza ya umoja wa kitaifa na Rais wa wakati huo, Dkt. Ali Mohammed Shein.
Serikali ya umoja wa kitaifa na katiba ya Zanzibar ilikusudiwa kuwa chombo cha kusimamia, kuratibu na kuongoza juhudi za wazanzibari katika maridhiano na umoja wa kitaifa.
Haikuwa na bado sio leongo la serikali ya umoja wa kitaifa kuwa chombo cha kugawana vyeo kwa kambi za kisiasa, ni vyema jambo hili tukalikumbuka kila wakati.
Katika kuwasaidia wale wenye imani na ufahamu potofu juu ya serikali ya umoja wa kitaifa, napenda kutumia mfano rahisi, serikali ya umoja wa kitaifa ni sawa na chombo cha usafiri, kwa msafiri yeyote, awe wa baharini, angani au nchi kavu. Lengo lake sio kuingia katika meli, ndege au gari, lengo lake ni kufika safari aliyoipanga.
Safari ya wazanzibari ni maridhiano ya kweli, mshikamano na umoja wa kitaifa. Chombo chetu cha kufika safari hiyo kwa wakati ni serikali ya umoja wa kitaifa hivyo ni wajibu wa viongozi sote ambao tumepewa jukumu la kuongoza serikali kuhakikisha kwamba tunaitekeleza au tunakifanikisha chombo hiki katika safari yetu hiyo.
********
RAIS MWINYI: NATARAJIA TUTAWEKA PEMBENI TOFAUTI ZETU KUIJENGA ZANZIBAR
-
Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi amesema yeye ni muumini wa Umoja wa Kitaifa, mshikamano, udugu na maridhiano akiamini ni njia nzuri ya kujenga umoja na ustawi wa nchi.
-
Amesema maridhiano ya kweli yanajengwa kwa Dhamira, Uvumilivu na Kuaminiana akiongeza kuwa, Viongozi hawana budi kufahamu maslahi ya wananchi ndio jambo la msingi.
-
Ameongeza, tofauti zao zisiwe kikwazo cha maendeleo huku akihimiza wananchi wote kuwa kitu kimoja na kuunga mkono juhudi hizo zinazolenga kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.
Rais Mwinyi: Maridhiano ya kweli yanajengwa na mambo makuu matatu.
1. Dhamira ya kweli 2. Kuvumiliana, kustahimiliana na kusahau yaliyopita 3. Kujenga utamaduni wa kuaminiana.
Mafanikio ya Maridhiano yatategemea Wananchi kuzipa kisogo tofauti zetu. Mimi na Seif tumeridhiana.