Sisitizo la Rais wa Tanzania kwa mkutano wa COP26: Tunapimwa kwa vitendo vyetu, si kwa ahadi kubwa kubwa tunazotoa
Nov 02, 2021 07:39 UTC
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaeleza viongozi wa mataifa ya dunia wanaohudhuria mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi COP26 huko Glasgow, Scotland, kwamba mshikamano na juhudi zao kama viongozi katika kukabili mabadiliko ya tabianchi vitapimwa si kwa ahadi kubwa wanazotoa kwenye mkutano huo bali kwa jinsi watakavyotekeleza vipengele vyote vya mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.
Rais Samia ametaja vipengele hivyo kuwa ni pamoja na kupunguza makali ya mabadiliko ya tabianchi, kuhimili mabadiliko hayo sambamba na uchangiaji wa fedha kulingana na kiwango cha changamoto zilizoko hivi sasa.
Rais wa Tanzania amefafanua kwa kusema ,“mabadiliko ya tabianchi ni suala la dunia nzima na hivyo majawabu yake ni lazima yawe ya kimataifa; na hivyo tunatoa wito kwa nchi zilizoendelea ambazo ndizo zinazoongoza kwa uchafuzi, zitekeleze kwa vitendo ahadi zao za kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa kutoa fedha za kutosha kutuwezesha sisi nchi za kipato cha chini kufanikisha malengo yetu kwenye michango ya kitaifa ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa uendelevu.”
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Samia amesisitiza kuwa, fedha za kutosha hususan kupitia misaada ya fedha itakuwa ni msingi katika mikakati ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa COP26 Glasgow, Uskochi
Amesema nchi yake ya Tanzania na nyingine za kipato cha chini zimeandaa mipango ya kina ya NDCs ikiwa na mikakati dhahiri ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
Aidha ametahadhrisha kuwa bila kuchukuliwa hatua sasa tena kwa mshikamano, lengo la kuwa na kiwango cha joto katika nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi litatoweka punde na halitafikiwa.
Viongozi kutoka nchi zaidi ya 100 duniani wanahudhuria mkutano huo wa 26 wa kujadili mabadiliko ya tabianchi, ulioanza tarehe 31 Oktoba na kuendelea hadi tarehe 12 ya mwezi huu wa Novemba mjini Glasgow, Uskochi.../
Tags