Doctor Mama Amon
JF-Expert Member
- Mar 30, 2018
- 2,089
- 2,725
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akila kiapo cha kuilinda katiba ya Tanzania
Hapo awali nimefupisha hotuba ya Mbowe kama ilivyotolewa kwa waandishi wa habari pale Mwanza jana.
Sasa niko tayari kuifanyia uchambuzi kulingana na taarifa za ziada nilizozikusanya kutokana na wadatishaji wangu walioko sehemu mbalimbali nchini.
Katika uchambuzi huu nakusudia kumshauri Rais Samia kuchukua mazuri, na kuacha mabaya, yaliyomo katika hotuba ya Mbowe ya jana. Kuna faida nyingi kwake kama Rais kufanya hivyo.
Kwa ajili hii, naorodhesha mazuri katika hotuba ya Mbowe, mabaya katika hotuba ya Mbowe, na hatimaye kuweka mapendekeazo yangu mwishoni.
Mazuri katika hotuba ya Mbowe
Kuna mambo matatu naona ni mazuri katika hotuba ya Mbowe ya jana: Mosi, ni haki ya kujumuika, kuwasiliana na kujadiliana.
Pili, ni kufichua tetesi zinazofanana na ukweli kuhusu kinachoitwa kuibwa kwa uchaguzi mkuu wa 2020.
Na tatu ni utata katika uamuzi wa kuvunjwa kwa jiji la Dar es Salaam na kuanzisha "Jiji la Ilala".
Nitaeleza kwa ufupi kila moja.
1. Haki ya kujumuika, kuwasiliana na kujadiliana: Mbowe amekosoa msimamo wa serikali ya awamu ya sita dhidi ya haki ya kukusanyika, kujieleza na kuwasiliana.
Amerejea kauli ya Rais Samia kwamba, "mikutano ya hadhara isubiri kidogo". Hoja ya Mbowe ni nzuri kwa sababu nyepesi.
Rais Samia aliapa kulinda Katiba ya nchi. Uhuru wa kujumuika na kujieleza ni sehemu ya Katiba hiyo. Kwa hiyo, Rais Samia anawajibika kulinda haki za kujumuika na kujieleza na majukumu yanayoendana na haki hizo.
Tofauti kati ya utawala wa sheria na utawala wa hisani ni nyepesi lakini muhimu sana, kiasi kwamba ustaarabu katika dola inayoitwa Jamhuri unaanzia katika tofauti hii na kukomea kwenye tofauti hii.
Katika mfumo wa utawala unaozingatia haki na majukumu ya kisheria (human rights based governance framework), kila haki inajumuisha mambo manne: madai, mdai, mdaiwa na uhalali wa madai.
Madai ni stahiki, mdai ni mnufaika wa stahiki, mdaiwa ni mtu mwenye jukumu la kutimiza stahiki, na uhalali wa madai ni sababu inayothibitisha uwepo wa madai.
Kwa kuzingatia aina ya kitendo kuna madai ya aina mbili. Kuna madai yanayohusiana na kitendo chanya (positive action), kwa maana ya hali ya kutekelezwa kwa jambo.
Na kuna madai yanayohusiana na kitendo hasi (negative action), kwa maana ya hali ya kujizuia kutotekeleza jambo.
Hivyo, kuna madai yanayohusiana na kitendo chanya (positive rights), kwa mfano haki ya kunununa gari. Pili, kuna madai yanayohusiana na kitendo hasi (negative rights), kwa mfano haki ya kutonunua gari.
Kwa kuzingatia aina ya mtendaji kuna madai ya aina mbili pia. Kuna madai yanayohusiana na mtendaji anayeshughulikiwa (passive agent), kwa maana ya mtu anayenufaika na jambo linalotekelezwa na mtu baki. Mfano wa mtendaji anayeshughulikiwa ni mgonjwa anayedungwa sindano.
Na kuna madai yanayohusiana na mtendaji anayejishughulikia (active agent), kwa maana ya mtu anayenufaika na jambo linalotekelezwa, sio na mtu baki, bali yeye mwenyewe. Mfano wa mtendaji anayejishughulikia ni mtu anayejikata kucha za vidole.
Kwa hiyo, kuna madai yanayohusiana na mtendaji anayejishughulikia (active rights), kwa mfano haki ya mtu mzima kujilipia karo ya shule. Na kuna madai yanayohusiana na mtu anayenufaika na jambo linalotekelezwa na mtu baki. (passive rights), kwa mfano haki ya mtoto kulipiwa karo ya shule na baba yake.
Kwa ujumla haki zote zinazofahamika zinaweza kugawanywa katika makundi makuu manne yafuatayo:
- Haki chanya ya kujishughulisha (positive active rights), mf. haki ya kufanya mkutano;
- Haki hasi ya kutojishughulisha (negative active rights), mf. haki ya kutofanya mkutano;
- Haki chanya ya kushughulikiwa (positive passive rights), mf. haki ya kupatiwa ulinzi wa mkutano;
- Haki hasi ya kutoshughulikiwa (negative passive rights), mf. haki ya kutozuiwa kufanya mkutano halali.
Kwa ujumla neno HAKI linataja mambo manne kwa mpigo. LInatwambia kuwa, kama kuna watu wawili, mtu A na jirani yake B, ambapo mtu A anayo haki dhidi ya jirani yake B, basi, watu hawa wawili wanaunganishwa na tendo (T) kwa mujibu wa kanuni ya kisheria au ya kimaadili (K).
Yaani, tunapaswa kuongelea haki nne zilizotajwa hapo juu kwa njia zifuatazo:
- Haki chanya ya kujishughulisha (positive active rights): Mtu A atakuwa na haki ya kufanya tend T, bila hofu ya kubughudhiwa na mtu baki B, endapo kuna kanuni K inayoonyesha kuwa mtu B anakatazwa kumzuia mtu A kufanya tendo T;
- Haki hasi ya kutojishughulisha (negative active rights): Mtu A atakuwa na haki ya kutofanya tend T, bila hofu ya kuuliziwa na mtu baki B, endapo hakuna kanuni K inayoonyesha kuwa mtu A anapaswa kufanya tendo T, hata kama tendo T ni kwa faida ya mtu B;
- Haki chanya ya kushughulikiwa (positive passive rights): Mtu B atakuwa na haki ya kufanyiwa tend T kupitia utendaji wa mtu baki A, endapo kuna kanuni K inayoonyesha kuwa mtu B anapaswa kufanya tendo T akiwa amemlenga mtu A;
- Haki hasi ya kutoshughulikiwa (negative passive rights): Mtu B atakuwa na haki ya kutofanyiwa tend T kupitia utendaji wa mtu baki A, endapo kuna kanuni K inayoonyesha kuwa mtu B anapaswa kutofanya tendo T akiwa amemlenga mtu A;
Hapa hakuna mtu mwenye kubeba jukumu. Huu ni utawala unaoongozwa na kanuni ya huruma.
Yaani, kuna kanuni ya matakwa binafsi, kama itampendeza mtekelezaji. Huu ni utawala unaoongozwa na huruma ya mtawala.
Kwa mujibu wa Katiba na sheria zetu, pamoja na mapungufu yake, Tanzania sio nchi inayopaswa kuongozwa na mfumo huu.
Kwa hiyo, katika mipaka hii, hoja ya Mbowe inapaswa kukubaliwa na serikali.
2. Utata katika uamuzi wa kuvunjwa kwa jiji la Dar es Salaam na kuanzisha "Jiji la Ilala"
Mbowe amekosoa utaratibu uliotumiwa kuvunja jiji la Dar es Salaam la zamani na kuwateua Meya na Mkurugenzi wa Jiji JIpya.
Lakini kuna tatizo kubwa zaidi. Yote mawili yana matatizo. Hoja ya kuwa na madiwani wa Jiji ambao hawajachaguliwa moja kwa moja inakubalika. Lakini mengine mawili hayana umantiki: Kuifanya Ilala na Temeke Jiji na kuibagua Kinondoni. Ni kutuko.
Enzi za Charkes Keenja kulikuwa na mfumo bora zaidi. Profa Tibaijuka anaweza kushauri zaidi katika eneo hili. Lakini huu mfumo wa sasa wa jiji ni aibu inayopaswa kumalizwa haraka.
3. Kufichua tetesi zinazofanana na ukweli kuhusu kinachoitwa kuibwa kwa uchaguzi mkuu wa 2020: Mbowe amesema wazi wazi kuwa kuna watumishi wa umma waliiba uchaguzi.
Kauli hii ni majumuisho ya kauli zake kwenye vikao vya ndani wakati wote wa opereshenui haki. Utafiti wangu mdogo umenionyesha mambo yafuatayo:
(a) Kauli hii inaakisi picha iliyoota mizizi kwenye vichwa vya wananchi wa kawaida huko vijijini.
(b) Sababu moja iliyoleta picha hii ni ukweli kwamba, katika baadhi ya maeneo karatasi za kupigia kura zenye mhuri halali wa NEC zilitolewa kwa mawakala wa Chadema waliokuwa wamejifanya ni wakereketwa wa CCM. Siri ikafichuka hivyo.
(c) Sababu ya pili iliyoleta picha hii ni ukweli kwamba, katika baadhi ya maeneo wagombea wa Chadema waliteuliwa na NEC, na baadaye kutenguliwa bila sababu yoyote halali. Wasimamizi wa uchaguzi wa Wilaya (yaani ma-DED) walisimamia kikamilifu uhalifu huu, tena wazi wazi. Na baadhi ya watendaji wa NEC bila kujua walirekodiwa na audio clips zao zenye kuonyesha wazi kwamba walikuwa wanahujumu uchaguzi kusambazwa duniani.
(d) Katika baadhi ya maeneo matokeo ya wagombea wa Chadema yalibadilishwa na wasimamizi wa vituo, lakini, baada ya vijana wenye mapanga, mikuki na visu kuzingira vikosi vya Kamati ya ulinzi na usalama vya wilaya, wasimamizi wa vituo husika walilazimishwa kurudisha matokeo waliyokuwa wamechakachua. Katika maeneo hayo, wagombea wa Chadema walitangazwa washindi. Mfano hai ni Kata ya Kanoni, WIlayani Karagwe, Mkoani Kagera.
(e) Ma-DSO katika baadhi ya maeneo walitumia uchaguzi mkuu wa 2020 kukusanya mamilioni kutoka kwa wafanya biashara na wagombea udiwani kwa hoja kwamba walikuwa wanakusanya fedha ya kulinda kata za kimkakati.
Kwa hiyo, hata Idara ya Usalama wa Taifa ilichafuka tena wazi wazi. Fedha nyingine walikuwa wanarushiana kidijitali utadhani hawakusoma lile somo la electronic evidence collection.
Mifano ni mingi. Lakini, kwa hapa itoshe kusema haya. Mchezo huu unaonekana ulifanyika sehemu nyingi, ikiwemo Hai kule kwa Mbowe. Kwa hasira Mbowe akaamuru mawakala wake waondoke vituoni kabla ya majumuisho kwa sababu ya hoja kwamba, "hakuna uchaguzi hapa."
Hali kama hii ilijitokeza sehemu nyingi. Kwa hiyo, Chadema hadi leo hawana ushahidi wa kisheria wanaoweza kuutumia mahakamani. Kwa hiyo, wanachoweza kufanya chadema kwa sasa ni kukusanya "retrospective evidence."
Lakini, ushahidi wa kimazingira umezagaa katika vijiji vingi kuashiria kwamba CCM waliiba uchaguzi. Kwenye siasa, ushahidi wa kimazingira unatosha.
Na kwa maoni yangu, imani kwamba "CCM waliiba uchaguzi mkuu wa 2020" imejikita kwenye vichwa vya watanzania wengi zaidi ya 80%.
Kwa hiyo, kwa kuzingatia ukweli nilioueleza hapo juu, kuna haja ya Rais Samia kufanyia kazi sintofahamu hii kwa njia mbalimbali.
Njia ya kwanza, na ambayo, kwa hakika, alitarajiwa kuwa ameifuata ndani ya siku zile 100-200 za kwanza ofisini ni kuwaweka pembeni watendaji ambao wanatiwa hatiani na ushahidi wa kimazingira kiasi kwamba hata wauza nyanya sokoni wanaimba wimbo huu kila siku.
Hata hivyo, jambo hili linavyo vigingi kadhaa. Katika baadhi ya maeneo zoezi la kuandaa,kutunza na kusambaza zile kura tata lilishirikisha kambi za jeshi, magari ya magereza, watumishi wa halmashauri waliokuwa wanatumikia NEC, ma-DSO, na kadhalika.
Kwa hiyo, Rais Samia anayo kazi. Itabidi afanye maamuzi ambayo ni arbitrary ili kuchora mstari wa kuwatenganisha wale atakaobaki nao na wale anaopaswa kuwaweka kando.
Kwa ufupi,mawili haya hapo juu ndio naona kama mazuri katika hotuba ya Mbowe ya jana huko Mwanza.
Mabaya katika hotuba ya Mbowe
Kuna mabaya matano nimeyaona katika hotuba ya Mbowe. Haya ni:
- Kukejeli uzuri wa Katiba ya sasa kana kwamba haina loolote zuri;
- Kushindwa kutofautisha kati ya vipaumbele vya Taifa na vipaumbele vya chama cha siasa;
- kumtaka Rais aingilie mhimili wa Bunge kuwatoa kina Mdee Bungeni kinyume cha kanuni ya mgawanyo wa madaraka yanayotambuliwa na Katiba ya sasa;
- Kujjianya hajui kuwa Ilani ya Chadema ya 2020 ilikiuka misingi ya usalama wa nchi;
- Kufanya siasa zenye harufu ya udini.
1. Kukejeli uzuri wa katiba ya sasa
Katiba ya sasa unakataza jinai mbali mbali, zikiwemo zile zilizotendeka wakati wa enzi za Magufuli. Inaweka wazi dira ya kitaifa kuhusu majukumu ya serikali.
Mfano ni ibara ya 9(i) inatamka kwamba kila tone la rasilimali litumike katika kuwahudumia wajinga, wagonjwa na maskini, kwa maneno mengine, rasilimali zitumike kuwahudumia watu wanyonge katika Taifa hili.
Kwa hiyo, hoja ya kudai Katiba Mpya haipaswi kuanzia kwenye ulaghai kwamba Katiba ya sasa ni bure kabisa.
Ubaya wa Katiba ya sasa haufuti uzuri wake katika maeneo kadhaa.
Na madai ya Mbowe kwamba watafanya makongamano na mikutano ya hadhara yanaanzia kwenye uzuri wa Katiba ya sasa.
Ni kosa kuwachanganya wananchi kwa kuwafanya washindwe kuona ukweli huu.
2. Kuilazimisha serikali kuvuruga ratiba yake ya kujenga nchi:
Kazi ya kujenga nchi inapitia katika mzingo wenye hatua kadhaa.
Kuna kuandaa ilani, kufanya uchaguzi na kutangaza mshindi, kutafsiri ilani na kuweka mipango ya maendeleo na kuipitisha bungeni, kutekeleza mipango, kutathmini utekelezaji, na hatimaye kuanza mduara huu upya katika uchaguzi unaofuata.
Kwa sababu ya mantiki hii, serikali hailazimiki kupokea hoja iliyo nje ya utaratibu huu ambao kwa kiingereza unaitwa statecraft cycle.
Serikali inaweza kushawishiwa kwa hoja zenye ushahidi thabiti, lakini sio kulazimishwa, kama ambavyo nimeona Mbowe anakusudia kufanya.
Kama Mbowe anasema kuwa, hoja ya kuheshimu mduara wa ujenzi wa nchi haikubaliki kwa sababu serikali iliyopo iliiba uchaguzi, inabidi ajenge hoja yake kwa kuweka ushahidi mezani, ili angalau 51% ya ushahidi huo umpendelee yeye.
Hana uwezo huo kwa kuwa aliamuru mawakala waondoke vituoni kabla ya majumuisho kufanyika.
Kwa hiyo, analazimika kutambua uhalali wa serikali iliyopo madarakani hadi hapo ushahidi wa kisheria utakapoonyesha vinginevyo.
Ama sivyo, anaweza kujikuta anaanguka kwenye mtaro wa uhaini.
3. Kushindwa kutofautisha kati ya kipaumbele cha kwanza cha Taifa na kipaumbele cha kwanza cha Chadema:
Kwa mujibu wa Ilani ya uchaguzi ya 2020 na mipango ya sasa ya Chadema, kweli Katiba Mpya ni kipaumbele namba moja.
Lakini hakuna Ratiba ya Kitaifa inayoonyesha kuwa Katiba Mpya ni Kipaumbele namba moja kitaifa.
Hoja hii lazima ijengwa na ushahidi uwekwe bayana, ili kuleta mwafaka juu ya madai kwamba Katiba Mpya ni Kipaumbele namba moja cha Kitaifa.
Mbowe hajafanikiwa kujenga hoja hii pamoja na siku zote alizozunguka katika operesheni haki.
Hata Jaji Warioba nimemsikiliza lakini hakufanikiwa kuongea jambo hili kama Jaji.
4. Kumlazimisha Rais Samia avunje Katiba kwa kuingilia shughuli za Bunge
Mbowe amemlaumu Rais Samia kwa kutochukua hatua za kuwatoa kina Mdee Bungeni. Anasema hawa ni "wabunge haramu wa Chadema."
Lakini hapa kuna matatizo mawili. Kwanza, kiutaratibu Rais hapaswi kuwamuru Spika afanye maamuzi gani. Tunamkosoa Magufuli na Ndugai kwa sababu kama hii. Kwa hiyo kama kuna lawama kuhusiana na kina Mdee sio za Rais Samia.
Lakini pili, kina Mdee wamekata rufaa wanasema maammuzi ya kuwafukuza yalitokana na vifungu vya kanuni za chama vinavyopingana na Katiba ya chadema.
Hivyo, wanaona mchakato uliotumika kuwafukuza ni batili. Baraza Kuu litakaa mwezi huu kuamua rufaa yao.
Na hapa ndipo utayari wa Chadema katika kusimamia misingi ya KIkatiba itakapodhihirika. Lakini, Rais Samia hahusiki huku pia.
Jaji Mtungi ameksiwhatoa maoni yake kuashiria kuwa Chadema waliwaonea kina Mdee.
Mbowe hajajipambanua kwa kuongelea hukumu ya Jaji Mtungu. Sababu iko wazi--Jaji Mtungi aligusa sehemu mbaya sana.
Chadema haitapata uhalali wa kisiasa wa kupigania Katiba Mpya ya nchi kabla haijaeleza ni kwanini iliamua kwa makusudi kukanyaga Katiba yake kama Jaji Mtungi alivyoonyesha.
5. Mbowe Kujjifanya hajui kuwa Ilani ya Chadema ya 2020 ilikiuka misingi ya usalama wa nchi
Ilani ya Chadema ya uchaguzi mkuu wa 2020 ilitamka kuwa kama Chadema itashinda uchaguzi itaweka rehani madini ya nchi yetu katika mabenki ya kigeni kama dhamana ili kutafu mitaji ya kujenga miundombinu hapa nchini.
Chadema haikueleza patatokea nini pale serikali itakaposhindwa kulipa madeni hayo. Literary, na hasa kisalama, huu ulikuwa ni mpango wa "kuuza" nchi.
Hakuna Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa aliyefundishwa, akafundishika, na kufuzu anayeweza kuruhusu chama chenye ajenda ya kuuza nchi kushika dola, hata kama nchi inayo Katiba nzuri kiasi gani.
6. Kufanya siasa zenye harufu ya udini
Mbowe ameonekana kufanya siasa zenye harufu ya udini. Anajaribu kujenga hoja kuwa viongozi wa dini wako juu ya sheria za nchi.
Mboowe anahoji, "juzi umewatoa mashehe wa uamsho sasa unawaingiza ndani maaskofu".
Ushehe na Uaskofu sio hoja ya maana katika ajenda ya utawala wa sheria.
Kwa historia zake, every religion is a double agent of good and evil.
Kwa hiyo, lazima sheria ifuate mkondo wake bila kujali kofia za kidini.
Lakini pia, hii habari ya kumwalika Askofu kutoa mada kwenye kongamano la Katiba halafu anamalizia uwasilishaji wake kwa kibwagizo cha "MWANAKONDOO AMESHINDA" ni kutumia dini kufanya siasa zinazogawa nchi kidini.
Sasa huku mitaani watu wamenaza kutania kwamba CHADEMA ni kifupi cha CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MWANAKONDOO AMESHINDA.
Kazi moja ya vyombo vya ulinzi na usalama ni kuhakikisha kuwa dini haigeuki chanzo cha mpasuko katika nchi. Lakini, siasa za Chadema zinatia shaka katika eneo hili.
Majumuisho na mapendekezo
Kwa sababu nilizozitaja hapo juu, sasa namshauri Rais Samia kuchukua maamuzi ya kuwaondoa kwenye utumishi wa umma wafuatao, kama hatua ya kwanza ya kutuliza vumbi la ukiukwaji wa haki za kisheria, kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa 2020:
- ma-DED wote;
- ma-DSO wote;
- ma-DAS wote;
- ma-OCD wote;
- ma-WEO wote;
- Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC na waandamizi wake;
- mawaziri waliobariki au kufumbia macho utekaji, utesaji, na mauaji ya holela;
- ma-RC, ma-DC na ma-RAS walikuwa wenyeji wa matukio ya utekaji, utesaji, na mauaji ya holela.
- Na Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa.
Ni pendekezo ambalo linayo faida kubwa kwake kama mkuu wa nchi, mkuu wa serikali na mgombea Urais katika uchaguzi ujao wa 2025. Hili la mwisho ni sababu muhimu zaidi.
HATIMAYE KWAKO MHE. DIWANI OTHMAN MSUYA: Yafaa umsaidie Rais Samia kwa kumpatia taarifa sahihi kuhusu mambo haya.
Wewe unayajua vizuri mambo haya kwa mujibu wa nafasi yako.
Kwa mujibu wa katiba, Makamu wa Rais anafanya kazi alizopangiwa na Rais. Na mazingira ya uendeshaji wa nchi enzi za Magufuli yalikuwa ni yenye kutumia kanuni ya mbele kwa mbele.
Hivyo, nahisi kuwa huenda Rais Samia anazo taarifa kidogo kuhusu baadhi ya masuala ya kitaifa yaliyotokea wakati wa enzi za Magufuli.
Nasema hivyo kwa sababu, kuna maamuzi Rais Samia alitarajiwa, anaweza na anapaswa kuyachukua kama sehemu ya ajenda yake ya "kusimsmisha nchi" lakini anachelewa sana, ama kwa kuwa hajapewa mkanda mzima wa classified intelligence briefings au kwa sababu nyinginezo.
Katika eneo hili, ni maoni yangu kwamba, dozi ya ukweli ulioshiba itamweka huru Rais Samia Suluhu Hassan.
Kazi iendelee kwa kasi na viwango.