Suala la katiba mpya lisitazamwe kwa fikra za upenzi wa vyama bali kwa fikra za upenzi wa Taifa letu.
Katiba inatakiwa imfae mwananchi yeyote awaye bila ya kujali itikadi. Watu wanaofikiria kuwa katiba ni suala la vyama vya upinzani, wanafanya makosa makubwa. Wasichojua, hata kama leo wewe ni mwanaCCM kindakinda, au kiongozi wa Serikali, bila katiba bora, huna uhakika na lolote katika maisha yako.
Tunataka watu wawe na uhakika na maisha yao. Wajione wapo salama kama hawajavunja sheria. Wajione wana fursa alimradi wana uwezo na nia ya kuzitumia fursa zilizopo. Watu wasiishi kwa hisani, wasizitumia fursa mbambali za maisha kama hisani. Thamani ya utu na ubinadamu wao isiwe ni kwa hisani ya kiongozi/mtawala.
Wazambia walikuwa na katiba iliyokuwa inampa madaraka makubwa Rais. Vyama vya upinzani na wanaharakati mbalimbali walilalamika, lakini walipuuzwa. Kaunda na Serikali yake wakaanguka kwenye uchaguzi. Chiluba, japo wakati wa kampeni aliahidi akishinda, atabadilisha katiba, alipoingia madarakani, hakubadilisha. Aliitumia katiba ile ile ya Kaunda, kumweka ndani Kaunda na mwanasheria wake mkuu wa Serikali. Kilio kikabadilika.