WAKATI Rais John Magufuli akionesha mfano kwa kubana matumizi katika safari za nje, nchini Kenya, Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake, William Ruto wamepunguza safari za nje ya nchi kwa asilimia 79 ndani ya miezi tisa.
Kwa Rais Magufuli aliyeingia madarakani kuiongoza Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania kuanzia Novemba 5, mwaka 2015, mpaka sasa hajatoka nje ya ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), licha ya kuripotiwa kuwa na mialiko ya zaidi ya nchi 100.
Ametembelea kikazi Rwanda, Uganda na Kenya ambazo ni sehemu ya nchi za EAC, nyingine zikiwa Tanzania, Burundi na Sudan Kusini.
Kazi nyingine za ndani na nje ya Afrika amekuwa akiwatuma ama Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan au Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na wakati mwingine viongozi wengine waandamizi serikalini. Mathalani, katika kipindi cha miezi tisa wametumia Sh milioni 36.5 za Kenya kufikia Machi mwaka huu.
Taarifa kutoka kwa Mdhibiti wa Bajeti nchini Kenya zinaonesha kuwa, safari hizo zimeokoa zaidi ya Sh milioni 143.7 za Kenya, kutoka Sh milioni 180.2 zilizotumika katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Uamuzi wa kupunguza safari umeonekana kushika kasi zaidi tangu Rais Kenyatta aanze kuitawala Kenya katika awamu yake ya pili mwishoni mwa mwaka jana. Wakati anaingia madarakani Aprili mwaka 2013, Kenyatta alitumia Sh milioni 75.9 za Kenya kwa safari za nje.
Na tangu hapo, bajeti ya safari ilipaa. Kufikia Machi, 2016, alitumia Sh milioni 167.5 za Kenya kwa safari za nje, ikiwa ni ongezeko kutoka Sh milioni 138.5 zilizotumika katika kipindi kama hicho mwaka 2015.
Aidha, safari za mawaziri, wakuu wa mashirika na taasisi za umma nazo zimeshuka kwa asilimia 33 hadi Sh bilioni 3.07 za Kenya ikilinganishwa na Sh bilioni 4.6 za nchi hiyo zilizotumika mwaka uliopita, jambo linaloashiria kuwa, kazi ya kubana matumizi kwa safari za nje inazaa matunda.
JPM aokoa matrilioni Kwa mujibu wa Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kati ya Nonemba 2015 na Novemba 2016, serikali iliokoa kiasi cha Sh bilioni 902 kutokana na kusitisha safari za nje ya nchi kwa watumishi wa serikali. Ripoti hiyo ilionesha kuwa, Tanzania ilitumia kiasi cha Sh trilioni 1.7 katika safari za nje ya nchi, ikiwa ni sawa na punguzo la trilioni 1.2 ambapo kwa kipindi kama hicho Novemba 2014 hadi Novemba 2015, serikali ilitumia kiasi cha trilioni 2.64 kwa safari za nje ya nchi.
Novemba 6, 2015 ikiwa ni siku moja tangu aapishwe kuishika Ikulu ya Tanzania, Rais Magufuli alisema safari za nje ya nchi zilikuwa zikiigharimu Tanzania fedha nyingi ambazo zingeweza kutumiwa katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Mbali na kuzuia safari za nje ya nchi, Rais Magufuli pia alifuta semina elekezi kwa viongozi, alipiga marufuku kufanyia mikutano kwenye kumbi za hoteli, kufuta sherehe za uhuru na kadhalika na badala yake, fedha za shughuli hizo zilitumika kwa shughuli nyingine za maendeleo.
Kagame, Museveni Wakati Magufuli na Kenyatta wakionekana kushika hatamu katika kubana matumizi ya fedha za umma kwa safari za nje, marais wengine wa ukanda huo, nao wana mtazamo sawa.
Hata hivyo, Rais Paul Kagame wa Rwanda anaonekana kuwa na safari nyingi za nje kutokana na kuwa pia na majukumu ya kimataifa, kwani kwa sasa ndiye Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).
Kwa Museveni, pia safari zake za nje kwa sasa zinachangiwa pia na nafasi yake ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inayohitaji safari za mara kwa mara za kikazi kwa ajili ya jumuiya hiyo yenye zaidi ya wakazi milioni 160.
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi hajaonekana kuwa na safari za nje kwa takribani miaka miwili sasa, wakati Salva Kiir wa Sudan Kusini, naye amekuwa na safari chache, ukiondoa nyingi za safari za ndani ya jumuiya zinazolenga kumkutanisha na wadau wengine katika mchakato wa kusaka amani ya kudumu katika taifa hilo changa zaidi duniani.